Alhamisi, 26 Juni 2025

RC KATAVI ATEMBELEA UJENZI WA JENGO LA KITUO JUMUISHI CHA UTOAJI HAKI

·      Aziagiza Tanesco, Mamlaka ya Maji kutatua changamoto za Maji na Umeme

Na ALLY RAMADHANI – Mahakama Katavi

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko, ameitaka Mamlaka ya Maji na Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) mkoani humo kutatua changamoto za maji na umeme kwenye eneo la mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoa wa Katavi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Akizungumza wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo hilo la Mahakama, Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa Mahakama mkoa wa Katavi alisema jengo hilo linalojengwa na Kampuni ya M/s AZHAR Construction Co. Ltd. linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu mpaka minne ijayo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema ujenzi wa Kituo hicho hauna budi  kukamilishwa kwa kwa wakati na kwa viwango na ubora uliokusudiwa kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi wa jengo hilo.

“Kukamilika kwa Kituo Jumuishi cha Utoaji haki Katavi, kutasogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa adha wanayopata ya kutoka Mkoa wa Katavi Kwenda Sumbawanga mkoani Rukwa kufuata Huduma za Mahakama Kuu, ”alisema Mkuu wa Mkoa.

Akitoa taarifa ya  maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo hilo kwa Mkuu wa mkoa, Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Victor Vedasto Ntungamo, alisema mradi huo umefikia asilimia 57 na kwa upande wa jengo umefikia  asilimia 60. Aliongeza kuwa mradi huo unahusisha sehemu tatu ambazo ni jengo Kuu, eneo la nje (uzio, mgahawa, chumba cha ulinzi) pamoja na Manzari ( Landscaping).

Aidha, Mhandisi huyo alimweleza Mkuu wa Mkoa wa Katavi kuwa mradi huo unakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa umeme na maji ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia kupunguza kasi ya ujenzi wa jengo hilo.

Nguzo ya pili ya Mpango Mkakakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania inasisitiza Utoaji Haki kwa wakati. Mahakama ya Tanzania inatekeleza mpango huu kwa kuboresha mazingira ya utoaji haki na kusogeza huduma za utoaji haki kwa wananchi kwa kujenga miundombinu bora na wezeshi itakayochangia ufanisi mzuri wa utekelezaji wa nguzo hii.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko (mwenye miwani) akiwa kwenye eneo la ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki mkoa wa Katavi alipotembelea hivi karibuni.

Mhandisi Victor Ntungamo, akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mkoa wa Katavi kwa Mkuu wa mkoa huo Mhe. Mwanamvua Mrindoko.

(Habari hii Imehaririwa na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni