Ijumaa, 27 Juni 2025

VIONGOZI KANDA YA MOSHI WAKAGUA MRADI WA UJENZI MAHAKAMA YA WILAYA SIHA

  • Jaji Mfawidhi amtaka Mkandarasi kuzingatia muda wa ukamilishwaji wa mradi huo  
  • Wazungumza pia na Watumishi wa Mahakama za Wilaya Siha, Hai
  • Wawakumbusha watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma

Na PAUL PASCAL, Mahakama-Moshi

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi imehitimisha ziara ya ukaguzi katika Mahakama za Wilaya za Hai na Siha sambamba na kufanya ukaguzi wa Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Siha. 

Ukaguzi huo ulifanyika tarehe 24 Juni, 2025 na kuongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella aliambatana na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje pamoja na Mtendaji wa Mahakama-Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala. 

Baada ya ukaguzi wa Mahakama za Wilaya ya Siha na Hai, Jaji Mfawidhi pamoja na wajumbe alioambatana nao katika ukaguzi huo walipokea taarifa na maelezo ya kina kutoka kwa mkandarasi anaetekeleza mradi huo sambamba na kutoa maelekezo ya aliyoyaona wakati akikagua mradi huo.

“Nimepita nimejionea yote yanayoendelea kazi ni nzuri ila changamoto iko kwenye kasi ya kukamilisha kazi hii. Mkandarasi ongeza kasi ya utendaji kwa taarifa mradi huu unapaswa kukabidhiwa ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu ila kwa kazi ambazo hazijafanyika sidhani kama siku hizi sita zilizosalia mtaweza kukamilisha,” alisema Mhe. Dkt. Mongella.

Kwa upande wake, Mkandarasi anayetekeleza mradi huo, ‘Pioneer Construction’ kupitia Mhandisi anayesimamia mradi huo, Mhandisi Mike Laswai alibainisha kazi zilizosalia kukamilisha mradi huo.

“Mhe. ‘Jaji Mfawidhi’ nikushukuru sana kwa maelekezo yako naahidi kuongeza kasi katika kukamilisha kazi hii kwa sasa nguvu kubwa tunaweka katika kazi za nje yaani kutengeneza bustani, kuweka usawa wa ardhi pamoja na kukamilisha uzio tutajitahidi ipasavyo kuendana na muda ili kampuni yetu isikwamishe matakwa ya mteja wetu,” alisema Mhandisi Laswai.

Katika hatua nyingine wakati wa ukaguzi huo, viongozi hao walizungumza  na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Siha na Hai pamoja na Mahakama za Mwanzo Ngarenairobi na Bomang’ombe kwa nyakati tofauti ambapo Mhe. Dkt. Mongella aliwakumbusha watumishi kufanya kazi kwa weledi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kutunza rasilimali za Mahakama kufuatia uboreshaji unaofanywa na Mahakama ya Tanzania.

“Kwanza kabisa niwapongeze watumishi wote wa Mahakama hizi kwa kutimiza majukumu yenu ya msingi hali inayowezesha kuondokana na mashauri ya mlundikano katika vituo vyenu, vilevile niwasihi kuendelea kuchapa kazi kwa weledi, kutunza rasilimali zetu zinazotuwezesha kutekeleza majukumu yetu, hivi karibuni tunakwenda kuwa na majengo ya kisasa niwaombe tuyatunze,” alisema Jaji Mongella.

Naye, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje alisema, “nawasihi watumishi wa Mahakama za Wilaya za Hai na Siha kutambua na kuiishi Dira ya Mahakama ya Tanzania na kuongeza ufanisi katika matumizi ya TEHAMA ili kuongeza kasi ya utoaji haki kwa wakati.”

Mhe. Mwaiseje aliwapongeza watumishi wa kada zote na kusema kuwa anaamini utendaji mzuri waliouona katika vituo hivyo ni kufuatia ushirikiano uliopo.

Aidha, Naibu Msajili huyo, aliwahishi watumishi wote kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na kasi ya mabadiliko kuboresha utoaji haki.

“Sote ni mashahidi kwa sasa suala la matumizi ya teknolojia halina mbadala hivyo hatuna budi kila mmoja kwa nafasi yake kuhusika katika mabadiliko haya ili tuweze kuwahudumia wananchi ipasavyo kwa Mahakama za Mwanzo ni lazima tusajili na kutoa mashauri yote katika mfumo wetu wa ‘primary courts App’ kama ilivyo kwa Mahakama za Wilaya kwenye mfumo Wa e- CMS  na Mahakama Mtandao,” alisema Naibu Msajili huyo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala aliwahimiza watumishi wa Mahakama za wilaya Hai  na Siha kutambua umuhimu wa kutunza rasilimali zote za Mahakama pamoja na kuwa na maadili ya utumishi wa umma.

“Kama ambavyo wamekwisha sema mengi mazuri watangulizi wangu niwaombe kila mmoja wetu kuona thamani ya uboreshaji uliofanywa na Mahakama ya Tanzania katika Wilaya hizi.ni jukumu letu kulinda rasilimali zote za Mahakama, tujitahidi kuishi maisha ya kizalendo ikiwa ni sambamba na kuheshimu maadili ya mtumishi wa umma sitegemei kusikia malalamiko juu ya vitendo visivyo vya kimaadili katika vituo vyetu,” alisema Bi. Itala.

Ukaguzi huo ni wa robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambao unakwenda kukamilisha ukaguzi wa jumla ya Mahakama za wilaya sita zinazounda Kanda ya Moshi. Ukaguzi huu ni wa kawaida na hufanyika kwa mujibu wa miongozo ya ukaguzi kwa Mahakama ya Tanzania.

Ukaguzi huo ulilenga kukagua shughuli zote za utoaji haki na uendeshwaji wa Mahakama hizo katika kipindi hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt Lillian Mongella akikagua maeneo mbalimbali katika eneo la Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Siha ili kujionea shughuli zinazoendelea katika mradi huo.

Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi Mahakama ya Wilaya Siha, Mhandisi Mike Laswai (kushoto) akitoa maelezo kuhusu mradi huo kwa Jaji  Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Lillian Mongella wakati wa ukaguzi uliofanyika kwenye mradi huo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Lillian Mongella (katikati) akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika katika eneo la Mradi wa Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Siha kwa ajili ya ukaguzi wa Mradi huo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Lillian Mongella (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa mahakama ya Mwanzo Ngarenairobi Wilayani Siha wakati wa ukaguzi huo uliofanyika tarehe 24 Juni, 2025.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Lillian Mongella (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Bomang'ombe wilayani Hai wakati wa ukaguzi huo.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)









 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni