- Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mahakama awaita wananchi kupata huduma na elimu
- Huduma ya usikilizaji mashauri kwenye Mahakama Inayotembea nayo yatolewa moja kwa moja viwanjani hapo
Na MARY GWERA,
Mahakama-Dar es Salaam
Mahakama ya Tanzania
imeweka kambi katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2025 yanayoendelea
kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es
Salaam kwa lengo la kutoa huduma na elimu kwenye masuala mbalimbali ya Mahakama
na sheria kwa ujumla.
Kwa mwaka huu, Viongozi
na watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau mbalimbali ambao ni watalaam na
wabobezi katika masuala ya kisheria wanaendelea kutoa huduma na elimu ya sheria
kwa muda wote wa Maonesho ambayo yameanza tarehe 28 Juni, 2025.
Katika kipindi chote cha
Maonesho, Mahakama inatoa huduma mbalimbali zikiwemo za kusikiliza Mashauri
kwenye Mahakama Inayotembea ‘Mobile Court Services’, kutoa Msaada wa Kisheria
‘TLS’, elimu kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Mahakamani
na safari ya Mahakama kuelekea Mahakama Mtandao ‘e-Judiciary’.
Akizungumza katika
mahojiano maalum leo 30 Juni, 2025 katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini
Dar es Salaam, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam
na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya ushiriki wa Mahakama katika Maonesho
ya hayo, Mhe. Hussein Mushi ametoa rai kwa wananchi kutumia nafasi adhimu
inayotolewa na Mahakama kwa kuwaleta pamoja watumishi wake na wadau katika
kutoa elimu ya sheria bure na kuelimisha taratibu mbalimbali za kupata haki Mahakamani.
“Nawaomba wananchi
kutumia fursa hii ya maonesho kuja kutoa maoni, malalamiko pamoja na kupata
msaada wa kisheria kutoka kwa Mawakili kutoka Chama cha Mawakili wa Kujitegemea
Tanganyika (TLS), Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria pia kujua
taratibu mbalimbali za Kimahakama,” amesema Mhe. Mushi.
Aidha, ametoa wito kwa
wananchi wote wa Dar es Salaam na Mikoa ya karibu kufika katika banda la
Mahakama.
Huduma nyingine
zinazotolewa katika banda la Mahakama ni elimu kuhusu huduma na taratibu
mbalimbali za ufunguaji wa mashauri, yakiwemo mashauri ya mirathi, elimu kuhusu
Mahakama ya Watoto, kuelezea manufaa au faida za Mfumo ulioboreshwa wa
Kusajili, Kuratibu na Kusimamia Uendeshaji wa Mashauri (Advanced Case
Management System).
Nyingine ni kutoa elimu
kwa wananchi kutambua umuhimu wa kutumia Kituo cha Huduma kwa Mteja ‘Call
Centre’ ya Mahakama ya Tanzania kutoa malalamiko na maoni yao.
Kueleza huduma
zinazotolewa na ngazi mbalimbali za Mahakama ikiwemo Divisheni za Mahakama Kuu
na Kituo cha Usuluhishi.
Katika kipindi chote cha Maonesho hayo, Mahakama ya Tanzania ipo pamoja na baadhi ya Wadau wake ambao ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama Cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambao wote wanatoa elimu kuhusu maeneo yao.
Banda la Mahakama ya Tanzania linapatikana ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere almaarufu Viwanja vya Sabasaba na linapatikana mkabala na banda la JKT.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ushiriki wa Mahakama ya Tanzania kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2025, Mhe. Hussein Mushi akizungumza kuhusu ushiriki wa Mhimili huo kwenye Maonesho ya (Sabasaba).
Mmoja kati ya wananchi waliofika katika banda la Mahakama akisubiri kupata huduma kwenye Mahakama Inayotembea iliyopo ndani ya Viwanja vya Mwalimu Nyerere (Sabasaba) vilivyopo barabara ya Kilwa-Temeke jijini Dar es Salaam.
Wananchi wakipata msaada wa kisheria kutoka kwa Mawakili wa Kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni