• Watumia fursa hiyo kuwaasa watumishi kuepuka huba, upendeleo na kutotumika kisiasa kipindi cha Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025
• Wakumbushwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma
• Utunzaji wa miundombinu ya majengo nao wahimizwa
Na PAUL PASCAL, Mahakama-Moshi
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi imefanya ukaguzi katika Mahakama za Wilaya Mwanga na Same ikiwa ni lengo likiwa ni kukagua shughuli zote za utoaji haki na uendeshwaji wa Mahakama hizo katika kipindi hicho.
Ukaguzi huo ulifanyika tarehe 17 Juni, 2025 na ulioongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Adriani Kilimi aliyeambatana na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje pamoja na Mtendaji wa Mahakama-Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala.
Viongozi hao walifanya ukaguzi pamoja na kukumbushana mambo kadhaa na watumishi wa Mahakama za Same na Mwanga kupitia vikao vya pamoja vilivyofanyika wakati wa kaguzi hizo.
Akizungumza katika vikao na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Same na Mwanga kwa nyakati tofauti, Mhe. Kilimi aliwakumbusha watumishi kufanya kazi kwa weledi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao haswa kipindi hiki ambapo Taifa linaelekea katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025.
“Kwanza kabisa niwapongeze watumishi wote wa Mahakama hizi kwa kutimiza majukumu yenu ya msingi hali inayowezesha kuondokana na mashauri ya mlundikano katika vituo vyenu, vilevile niwatake watumishi wote kutambua haki zenu na kuheshimu haki za wananchi wote ni dhahiri kila mmoja wetu afahamu ya kuwa mwaka huu Taifa letu linakwenda katika uchaguzi mkuu ni wajibu wetu kuhakikisha tunafanya kazi zetu kwa weledi ili kulinda haki ya kila mwananchi,” alisema Jaji Kilimi.
Aliwataka kwa namna yoyote ile kutorubuniwa au kutumika vibaya kwa maslahi ya mtu binafsi, kuepuka upendeleo na fitna bali wajikite kufuata taratibu za utoaji haki kwa kuwa ndilo jukumu la msingi la Mahakama.
“Tujiepushe na mambo yasiyo ya kimaadili ili tuisaidie Serikali yetu kuwa na mazingira ya amani na utulivu katika wakati huu tunaoelekea kwenye uchaguzi mkuu,” alisisitiza Mhe. Kilimi.
Naye, Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje aliwasihi watumishi wa Mahakama za Wilaya hizo kutambua na kuiishi Dira ya Mahakama ya Tanzania wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
“Nami nianze kwa kuwapongeza watumishi wote wa kada zote, naamini utendaji huu mzuri tuliouona katika vituo vyenu kuanzia Mahakama za Mwanzo Makanya, Same Mjini, Lembeni na Mwanga Mjini yote ni kufuatia ushirikiano uliopo baina yetu sote tukiendelea kwa kasi hii tunakwenda kuitimiza Dira yetu ya Mahakama ipasavyo ya Upatikanaji wa Haki kwa wote na kwa wakati,” alisema Mhe. Mwaiseje.
Aidha, Naibu Msajili huyo aliwaomba watumishi hao kuwa, waadilifu katika kipindi cha uchaguzi mkuu kwani ni kipindi ambacho baadhi ya watu wenye nia ovu wanaweza kukitumia makusudi kuchafua taswira ya Mahakama kwa wananchi na kusisitiza kwa kusema, “tutambue mipaka yetu, tuheshimu wateja wetu tuwahudumie bila upendeleo wala chuki hapo tutakuwa tumetimiza wajibu wetu ipasavyo.”
Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala aliwahimiza watumishi wa Mahakama za wilaya Mwanga na Same kutambua umuhimu wa kutunza rasilimali zote za Mahakama pamoja na kuwa na maadili ya utumishi wa umma.
“Kama ambavyo wamekwisha sema mengi mazuri watangulizi wangu niwaombe kila mmoja wetu kuona thamani ya uboreshaji uliofanywa na Mahakama ya Tanzania katika Wilaya hizi. Tumebahatika kupata majengo mapya matatu ndani ya miaka hii miwili ni jambo la kheri kwa kuwa yanakwenda kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu katika mazingira Rafiki,” amesema Bi. Itala.
Aliwaomba kila mtu kwa nafasi yake kutunza majengo hayo pamoja na vitendea kazi vyote kwa kuwa kupitia hivyo, vinawawezesha kutimiza majukumu ya msingi ya Mhimili wa Mahakama. Huku akiongeza kuwa, ana imani kupitia mafunzo waliyofanya katika Kanda hiyo tarehe 30 Mei mwaka huu kila mtumishi anajua vitendo vyote visivyoruhusiwa katika utumishi wa umma na hivyo kuwataka kuyaishi maadili ya utumishi wa umma.
Ukaguzi huo ni wa robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambao ni wa kawaida na hufanyika kwa mujibu wa miongozo ya ukaguzi kwa Mahakama ya Tanzania. Ulianza kwa kukagua Mahakama za Mwanzo Same Mjini na Makanya kwa Wilaya ya Same na Mahakama za Mwanzo Lembeni na Mwanga Mjini kwa upande wa Wilaya ya Mwanga na utaendelea kwa Wilaya nyingine nne zinazounda Mahakama Kuu Kanda ya Moshi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Adriani Kilimi akisaini kitabu cha wageni tarehe 17 Juni, 2025 alipowasili Mahakama ya Wilaya Same kwa ajili ya Ukaguzi wa Mahakama hiyo.
Muonekano wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Same ambalo limejengwa kupitia maboresho yanayoendelea ya Mahakama ya Tanzania.
Naibu msajili Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Sekela Mwaiseje akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Mwanga (hawapo katika picha) wakati wa kikao cha watumishi na viongozi wa Kanda hiyo waliofika kufanya ukaguzi.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Bi. Maria Itala akizungumza na watumishi (hawapo katika picha) kuhusu umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya Mahakama.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Adriani Kilimi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Wilaya ya Same.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Adriani Kilimi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Mwanga.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni