Na AIDAN ROBERT, Mahakama-Kigoma
Kanda ya Kigoma inaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya mifumo ya Mahakama kwa wananchi ili kuwajengea utamaduni wa kufuatilia mashauri yao kwa njia ya simu janja.
Akitoa elimu jana tarehe 18 Juni, 2025 kuhusu matumizi ya simu janja kwa wananchi waliofika Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kupata huduma, Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Bw. Ramadhan Kufakunoga alisema, ni rahisi kwa mwananchi kufuatilia mashauri yaliyopo mahakamani kupitia simu janja.
“Ni muhimu kufanya hivyo ili kufahamu jinsi Mahakama zinavyofanya kazi kutumia mifumo yake,” alisema Bw. Kufakunoga huku wananchi hao wakionesha kuhamasika na kujifunza kufuatilia mashauri yao kwa njia ya simu janja.
Aliwaeleza kuwa, maboresho makubwa ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na mingine imekuja kurahisisha na kupunguza gharama za wananchi katika kuifikia Mahakama.
“Kupitia njia hiyo unaweza kufahamu tarehe au kutaka nyaraka kama hukumu, amri, na uamuzi unaotolewa na mahakama, ambazo kwa sasa zinapatikana katika mfumo huo kwa urahisi kabisa,” alisema Bw. Kufakunoga.
Aidha, aliongeza kuwa, katika jengo la Mahakama Kuu ipo Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani ambayo inashughulikia rufaa zote kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, hivyo wasioridhishwa na hukumu za Mahakama Kuu nao wanahudumiwa katika masjala hiyo bila kuchelewa kwakuwa nayo masjala hiyo nayo ipo katika mfumo huo, ambapo rufaa zinasajiliwa pia.
“Tumieni simu zenu kwa ajili ya kuokoa muda na gharama za kusafiri kutoka mbali kuja mahakamani kufuata tarehe au hukumu mahakamani kwani hizo zinapatika katika mifumo yetu kupitia simu janja zetu, katika kurasa za tovuti za www.judiciary.go.tz na (https://tanzlii.org/judgments) pamoja na (www.judiciaryportal.go.tz),” alisisitiza.
Jumla ya wananchi 30 waliofika katika jengo la Mahakama hiyo walipata elimu ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza nguzo namba tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania ya kuoingeza imani ya wananchi kwa Mahakama.
Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Bw. Ramadhan Kufakunoga akifafanua jambo kwa wananchi wakati akitoa elimu ya matumizi ya simu janja kupakuwa taarifa za mashauri katika mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Sehemu ya wananchi wakifuatilia kwa makini elimu iliyokuwa ikitolewa na Msaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Bw. Ramadhan Kufakunoga (hayupo katika picha).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni