Jumanne, 17 Juni 2025

JAJI MAHAKAMA KUU GEITA AFANYA UKAGUZI WA MAHAKAMA

Na DOTTO NKAJA-MAHAKAMA, GEITA

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Venance Mwakapeje jana tarehe 16 Juni, 2025 alifanya ziara ya ukaguzi wa Mahakama kwa Robo ya Nne ya Mwaka 2024/25 kwa katika Mahakama za Wilaya ya Mbogwe na Bukombe na Mahakama za Mwanzo Masumbwe na Ushirombo.

Katika ziara hiyo aliyoifanya kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, Jaji Mwakapeje aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna, Mtendaji wa Mahakama Kanda hiyo, Bi. Masalu Kisasila na Maofisa wengine.

Akizungumza na watumishi mara baada ya kumaliza kusikiliza taarifa mbalimbali zilizowasilishwa, kuhusu Mahakama hizo, Mhe. Mwakapeje aliwataka kuzingatia maadili na uadilifu katika utoaji haki ili kuimarisha uhusiano na Watu waliopo nje ya Mahakama.

Jaji Mwakapeje aliwahimiza Watumishi kutumia rasilimali zilizopo kuzalisha zaidi na kuimarisha misingi ya utoaji haki na kuendelea kuyaenzi na kuyaishi maazimio ya Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA.

Mhe. Mwakapeje alisema, “Binafsi sipendi kuona Mtumishi yeyote katika Kanda yetu anakuwa kikwazo katika kukuza uwezo wa matumizi ya TEHAMA. Rai yangu ni kuiona Geita inazidi kuwa nuru ya kimataifa katika matumizi ya Mahakama Mtandao.”

Naye Mtendaji wa Mahakama Kanda hiyo aliwakumbusha Watumishi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu pamoja na miongozo mbalimbali inayoendelea kutolea na Viongozi.

Aidha, alikemea vitendo vya utovu wa nidhamu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuwataka Watumishi wawe na upendo, heshima, hekima na ushirikiano kwani kila mtumshi ni muhimu katika kukuza Taasisi.

Pia aliwataka kutambua kwamba kila Mtumishi ana mchango muhimu katika mafanikio ya Kituo chake alipo na Taasisi kwa ujumla.

“Mtumishi wa Umma hana kwao nyumbani kwake ni pale alipo. Hii ina maana kwamba Mtumishi wa Umma anatumia muda mwingi kuwa kazini, hivyo Watumishi wenzake alionao kazini ndiyo kama ndugu zake. Kwa hiyo, Watumishi tushirikiane na tuchukuliane kama ndugu,” alisema.


Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Masumbwe iliyopo Wilayani Mbogwe wakiupokea msafara wa Jaji Griffin Venance Mwakapeje.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Masumbwe, Mhe. Mashaka Msologone akiwasilisha taarifa fupi ya hali ya mashauri ile ya utawala na rasilimaliwatu kwa Jaji Mwakapeje.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna akitoa ufafanuzi juu ya changamoto za utumiaji wa mifumo ya Mahakama.

Watumishi wa Mahakama Wilaya ya Bukombe wakiwa katika kikao kifupi na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Mwakapeje baada ya ukaguzi kukamilika.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Griffin Venance Mwakapeje akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe.

 Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni