- Abainisha wakati akimkabidhi Ofisi Jaji Kahyoza
Na EMMANUEL OGUDA, Mahakama-Shinyanga
Katika kuhakikisha wananchi wa Kanda ya Shinyanga wanapata haki kwa wakati, Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imepunguza kwa kasi idadi ya mashauri yanayosikilizwa na kumalizika ndani ya Kanda hiyo.
Akizungumza jana tarehe 16 Juni, 2025 wakati akikabidhi ofisi ya Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga, aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Frank Mahimbali alibainisha kuwa, wakati anapokea Kanda hiyo mwezi Juni, 2023 idadi ya mashauri katika Kanda hiyo ilikuwa 1,948 idadi hiyo imepungua hadi kufikia mashauri 768.
“Kwa kushirikiana na Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu wasajili, Mahakimu na watumishi wote wa Mahakama kwa muda wa miaka miwili idadi hiyo imepungua hadi kufikia mashauri 768 ambayo ninajivunia kukabidhi Kanda hii ikiwa na idadi ndogo ya mashauri huku Mahakama Kuu pekee ikiwa na mashauri 248 kutoka mashauri 655 mwezi Juni, 2023,” alisema Mhe. Mahimbali.
Mhe. Mahimbali alieleza kuwa, mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa aliopewa na Majaji wa Kanda hiyo, Naibu Wasajili, Mahakimu, Watendaji na watumishi wote wa Mahakama Kanda ya Shinyanga.
“Kanda hii imeweza kusikiliza na kumaliza mashauri kwa wakati huku idadi ya mashauri ya mlundikano yakiwa tisa pekee ambayo pia mikakati imewekwa kuhakikisha mwezi Juni, 2025 mashauri hayo yanasikilizwa na kumalizika kabisa,” alisisitiza.
Aliongeza kwa kuwashukuru watumishi na wadau wa Kanda hiyo kwa kuwezesha shughuli ya usikilizwaji wa mashauri ndani ya Kanda hiyo kutekelezwa kikamilifu na kwamba anaondoka Shinyanga akiwa na furaha baada kuleta matokeo yanayoonekana.
Naye, Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Khyoza baada ya kukabidhiwa Kituo hicho ameahidi kuendeleza alipoishia Jaji Mahimbali huku akibainisha mikakati yake katika kuhakikisha nguzo tatu za Mpango Mkakati wa Mahakama zinatekelezwa kikamilifu.
Mhe. Kahyoza alisema kuwa, kupitia mapokezi mazuri aliyoyapata kwa Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga ana imani kuwa atapata ushirikiano kutoka kwa watumishi hao na kuhakikisha kuwa mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake yanaendelezwa na pengine zaidi ya hapo kwani asingependa wakati anakabidhi kituo hicho kiwe na idadi kubwa zaidi ya mashauri tofauti na aliyokabidhiwa.
‘’Dira ya Mahakama ya Tanzania ni kutoa haki kwa wakati, nitahakikisha ninaisimamia dira hiyo na niombe kila mmoja katika eneo lake ahakikishe anajipima iwapo imani ya wananchi kwa Mahakama imeimarishwa, nimepokea idadi ndogo ya mashauri nisingependa wakati nakabidhi kituo hiki kiwe na idadi kubwa tofauti na nilivyopokea nategemea kukabidhi na idadi sawa na niliyopokea ama pungufu ya niliyoipokea leo’’ alisema Jaji Kahyoza.
Kwa upande wa muda wa usikilizwaji na umalizaji wa mashauri, Jaji Kahyoza alibainisha kwamba, kwa kushirikiana na Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga wataendelea kushauriana ili kupunguza zaidi muda wa umri wa shauri mahakamani hadi kufikia miezi sita tangu shauri linapofunguliwa hadi kumalizika ikiwa ni mikakati ndani ya Kanda kukabiliana na mlundikano wa mashauri mahakamani.
Aidha, Jaji Kahyoza alibainisha kwamba, ataendelea kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ndani ya Kanda hiyo.
Akitoa salama za shukrani kwa niaba ya Watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Asha Mwetindwa alimpongeza Jaji Mahimbali kwa kuimarisha mshikamano wa watumishi wa Kanda hiyo kwa kuwa na vikundi vya kusaidiana wakati wa maafa, kuimarisha Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) ndani ya Kanda hiyo na vilevile kuweka msukumo kwa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA).
‘’Nikupongeze Mhe. Mahimbali kwa uongozi imara na thabiti wenye kuleta matokeo yanayoonekana, kila mmoja ana tabia yake lakini ulifanikiwa kutuleta pamoja watumishi wa Mahakama Kanda ya Shinyanga na sisi tunakutakia kila la kheri katika kituo kipya, aidha, tunakukaribisha Kanda ya Shinyanga, Mhe. Kahyoza tumejiandaa vema kushirikiana na wewe kuhakikisha tunafanya kazi kuendeleza alipoishia Jaji Mahimbali,’’ alisema Mhe. Mwetindwa.
Kadhalika, Mhe. Kahyoza alitembelea miradi ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo Kahama Mjini pamoja na Shinyanga Mjini ambapo alijionea miradi hiyo ambayo itakabidhiwa.
Mhe. Mahimbali amehamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha kuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo.
Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza akisalimiana na watumishi wa Kanda hiyo aliporipoti katika Mahakama hiyo jana tarehe 16 Juni, 2025.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. John Kahyoza akizungumza na watumishi wa Mahakama hiyo mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi ya Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa Kanda hiyo mara baada ya kukabidhi rasmi Kanda hiyo kwa Mhe. Kahyoza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni