Jumatano, 2 Julai 2025

JAJI MFAWIDHI KANDA YA MTWARA AFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MAHAKAMA MKOA WA MTWARA

Na HUBERT MAANGA, Mahakama-Mtwara

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Elias Kakolaki amefanya ziara ya ukaguzi wa Mahakama  za Mkoa wa Mtwara wenye lengo la kukagua utendaji kazi katika mahakama za ngazi ya chini kuhakikisha huduma ya utoaji haki inaenda vizuri.

 Katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 23, 24 na 30 Juni, 2025,  Jaji Kakolaki aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Seraphine Nsana, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Bw. Yusuph Msawanga, Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Stella Shindika na Afisa TEHAMA, Bw. Hubert D. Maanga.

 Miongoni mwa Mahakama zilizokaguliwa ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, Mahakama ya Wilaya Tandahimba, Newala, Nanyumbu,Masasi, Mahakama ya Mwanzo Mahuta, Kitangali, Chikundi na Nanyumbu.

Katika ziara yake, Mhe. Kakolaki alikutana na watumishi ambapo alipokea taarifa za utendaji kazi, kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutoa maelekezo mbalimbali. Aidha, kila Mahakama ya Wilaya, alizungumza na Mahakimu ambapo aliwasisitizia utendaji wenye uadilifu.

Aidha, Jaji Mfawidhi huyo aliwapongeza watumishi kwa utendaji kazi mzuri hasa kumaliza mashauri kwa wakati, kutokuwa na mlundikano wa mashauri, unadhifu na ubunifu wa kuhifadhi nakala laini za hukumu na mwenendo wa shauri kwa Mahakama za Mwanzo.

 "Kwa mwenendo huu, huduma ya Mahakama itazidi kuonekana bora na kuzidi kuvutia wateja kwa maana, mteja atakapopata haki yake na kuridhika na huduma yetu, atawashawishi hata wengine kuiamini Mahakama katika utoaji haki," alisema Mhe. Kakolaki.

Kadhalika, aliwapongeza Mahakimu kwa elimu inayotolewa redioni na sehemu nyingine kuhusu matumizi ya mifumo na manufaa yake, huku akiwasihi Mahakimu hao kuendelea kuwapa elimu wananchi, kuwaelewesha kuhusu matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji mashauri na jinsi gani inavyosaidia kuondoa gharama, kupunguza muda kuwezesha wateja kuendelea na shughuli nyingine.

Katika kutekeleza maagizo ya Jaji Mkuu, Jaji Mfawidhi huyo aliwataka Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuendelea kuchapa mashauri yote kwenye mfumo ili kurahisisha upatikanaji wa nakala laini za mienendo hiyo.

 

Akizungumzia hali ya Majengo ya Mahakama na vyombo vya usafiri, Mhe. Kakolaki alielekeza majengo yatunzwe kwa kutumia fedha za ndani zinazopatikana na magari na pikipiki navyo vifanyiwe matengenezo mara kwa mara ili viendelee kutumika.

“Aidha, Mahakama za wilaya zihakikishe maeneo yote ya Mahakama ambayo hayana hati miliki, yanapatiwa hati ili kurahisisha kuombea miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama,” alisisitiza.

Katika ziara yake Jaji Kakolaki alikagua miradi miwili ya ujenzi ya Mahakama ya Mwanzo Kitangari na Chikundi inayoendelea katika Mkoa wa Mtwara na kuridhika na kasi sambamba na usimamizi wa ujenzi wa miradi hiyo.

Jaji Mfawidhi huyo alitembelea pia Magereza ya Lilungu, Newala na Masasi ambapo alipokea taarifa na kusikiliza changamoto za wafungwa na mahabusu na kuwashauri kujifunza na  kukuza vipaji vya elimu ya ujasiriamali kwa manufaa yao watakaporudi uraiani.

Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Masasi wakimpokea Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki alipowasili katika Mahakama hiyo kwa lengo la ukaguzi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (wa pili kushoto) akiteta machache na watumishi wa Mahakama ya Wilaya Nanyumbu alipotembelea Mahakama hiyo hivi karibuni.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Tandahimba, Mhe. Joseph Waruku (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya Mahakama ya Wilaya hiyo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki akipanda mti katika viwanja vya Mahakama  ya Mwanzo Mahuta wilayani Tandahimba wakati alipotembelea Mahakama hiyo hivi karibuni.

Ukaguzi wa ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Kitangari iliyopo Wilaya ya Newala.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara,  Mhe. Edwin Kakolaki (kulia) akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Wilaya na Mkoa Mtwara.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wadau walipotembelea Gereza la Lilungu.


Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Masasi wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (wa pili kulia).

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mtwara Mhe. Edwin Kakolaki (wa tano kushoto). 

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni