Jumatatu, 30 Juni 2025

KAMPUNI YA URUSI, MWAJIRIWA KUTOKA UKRAINE WAKAA MEZA MOJA

  • Wakubali kusuluhishwa kwenye mgogoro wa kikazi kuhusu mapunjo ya mshahara

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, imefanikisha kusuluhisha mgogoro wa kazi kati ya Mwajiri, Kampuni la Maendeleo Technologies inayoongozwa na Raia wa Urusi na Mwajiriwa, Bw. Sergiy Lyeshchynskyy, ambaye ni Raia wa Ukraine, uliokuwa unahusu mapunjo ya mishahara.

Usuluhishi huo uliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, kwenye shauri la kazi lililowakutanisha Kampuni hiyo na Kamishna wa Kazi Tanzania, aliyemwakilisha Mwajiriwa huyo.

Kufuatia usuluhishi huo, kampuni hiyo imekubali kulipa kwa awamu mbili Dola za Kimarekani 40,000, ambayo ni zaidi ya Shilingi za Kitanzania milioni 100 kwa Mwajiriwa huyo, ambaye alikuwa Fundi Mitambo katika kampuni hiyo inayojihusisha na kukodi mitambo ya uchimbaji madini.

‘Mwajiri atamlipa Mwajiriwa Dola za Kimarekani 20,000 siku au kabla ya tarehe 30 Juni, 2025 na kiwango kitakachobaki cha Dola za Kimarekani 20,000 zitalipwa siku au kabla ya tarehe 31 Julai 31, 2025 na kufanya jumla ya Dola za Kimarekani 40,000 ya madai yote,’ inaeleza sehemu ya amri iliyotolewa hivi karibuni.

Katika makubaliano hayo, Mwajiri pia amekubali kulipa gharama za shauri ambazo ni sawa na asilimia tano ya Dola za Kimarekani 40,000 (Dola za Kimarekani 2,000) moja kwa moja kwa Wakili wa Mwajiriwa.

Kadhalika, Mwajiri amekubali kutoa tiketi ya ndege kwa mwajiriwa ya kurudi nchini kwake siku au kabla ya tarehe 31 Julai, 2025.

‘Kama Mwajiri atashindwa kutekeleza malipo hayo kama walivyokubaliana, Mwajiriwa atakuwa na haki ya kuomba amri ya utekelezaji wa makubaliano hayo dhidi yake,’ inaeleza sehemu ya amri hiyo.

Kukamilika kwa mgogoro huu kunatoa somo kuwa usuluhishi una faida nyingi, ikiwemo kama ukisimamiwa vizuri unawapatia nafasi  waajiri na waajiriwa kujielekeza zaidi katika shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi endelevu kwa maslahi yao na kwa Taifa, kuliko kupoteza muda mwingi pamoja na rasilimali fedha katika kufuatilia migogoro kwenye hatua ya uamuzi na marejeo.

Usuluhishi pia ni njia inayoweza kumaliza shauri kwa wakati na kwa urafiki na unaepusha upatikanaji wa tuzo isiyotekelezeka, mfano: Wakati kesi inaisha mdaiwa wa hukumu ana kuwa hana kitu cha kumlipa, mmiliki wa tuzo, kwa sababu ya muda mrefu ulitumika kusikiliza shauri lake na pengine anakuwa amefirisika.

Aidha, usuluhishi unaondoa uadui baina ya pande mbili zenye mgogoro na ukifanywa vizuri unaponya.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.


Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni