Alhamisi, 17 Julai 2025

DIVISHENI YA KAZI YAAHIDI KUIMARISHA USIMAMIZI UTEKELEZAJI SHERIA YA USALAMA MAHALI PA KAZI

Na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi inakusudia kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni ili kuendelea kuboresha mazingira bora ya kazi na kuleta ustawi kwa wafanyakazi.

Hayo yamebainishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina leo tarehe 17 Julai, 2025 katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza wakati akifunga Mafunzo ya Siku mbili kwa Majaji, Watendaji na Wadau wa Mahakama yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

“Siku ya jana tuliweza kushuhudia, wakuu wa Taasisi hizi mbili Mahakama ya Tanzania na OSHA wakiweka saini katika makubaliano ili OSHA kuweza kuendelea kutoa mafunzo ya aina hii kwa muda wa miaka miwili. Hili ni tukio moja muhimu na la kihistoria, hivyo Divisheni ya Kazi itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi na usalama wa wafanyakazi,” amesema Mhe. Dkt. Mlyambina.

Jaji Mfawidhi huyo ameishukuru OSHA kwa kuendelea kushirikiana na Mahakama hususani Divisheni ya Kazi na kuahidi kuwa, makubaliano hayo yatatekelezwa kupitia mafunzo endelevu kwa Majaji, Mahakimu, Watendaji wengine wa Mahakama na wadau mbalimbali wa Haki Kazi.

“Lengo la kuendelea kutoa mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa juu ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na kanuni zake na hivyo kuwawezesha kusimamia haki kupitia jukumu lao la msingi la kutafsiri sheria katika mashauri yanayohusiana na usalama na afya mahali pa kazi,” ameeleza Jaji Mfawidhi huyo.

Kuhusu mafunzo hayo yaliyohitimishwa leo, Mhe. Mlyambina amesema yalikuwa na malengo makuu manne nayo ni pamoja na kujenga uelewa wa masuala ya usalama na afya kwa washiriki hususani kuwawezesha kutambua vihatarishi vya magonjwa na ajali katika shughuli za kila siku.

Amesema lengo lingine ni kujenga uelewa juu ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake na viwango vya kimataifa vya usalama na afya kazini (OSHA) na jinsi ya kuvitumia katika mazingira ya kazi ya sasa, hasa kwa kuzingatia mabadiliko ya kidijitali na Akili Unde (AI) miongoni mwa washiriki ili waweze kuitumia ipasavyo katika kushughulikia mashauri yanayohusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

“Lengo lingine ni kuandaa washiriki kuwa na ujuzi wa kisasa unaoendana na mabadiliko ya dunia ya kazi, ili waweze kuchangia katika mazingira ya kazi yenye amani, usalama, na tija — kwa manufaa ya pande zote na kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla kufikia malengo ya Dira ya Taifa ambayo inasainiwa leo tarehe 17 Julai, 2025,” amesema Mhe. Dkt. Mlyambina.

Kadhalika, Jaji Mfawidhi huyo ameongeza kwamba, mafunzo hayo yalilenga pia kuwawezesha madereva, walinzi wa viongozi na wadau wa usafirishaji kuelewa na kutumia teknolojia za kisasa kwa kufuata sheria, kuboresha usalama barabarani, kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali, na kukuza ujuzi wa kidijitali kwa ajili ya huduma bora na salama za usafirishaji.

Aidha, Mhe. Dkt. Mlyambina amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuhusu mada zilizotolewa na kuwasihi kuzingatia na kutekeleza kwa vitendo yote waliyofunzwa.

Miongoni mwa mada zilizotolewa wakati wa mafunzo hayo yaliyofunguliwa tarehe 16 Julai, 2025 na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ni pamoja na  Itifaki, Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Vihatarishi vya Afya na Usalama Mahali pa Kazi na kadhalika.

“Kwa kupitia mada hizo ni wazi kuwa tumepata shule ya kutosha na kama alivyoshauri Jaji Kiongozi ni matumaini yangu kuwa elimu hiyo itasaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu,” amesema Jaji Mfawidhi huyo.

Mhe. Dkt. Mlyambina amewashukuru washiriki wote wa mafunzo hayo kwa ushirikiano, usikivu na michango ya mawazo mbalimbali waliyoyatoa akiongeza kwa kusema, “ni matumaini yangu kuwa yale tuliyojifunza na kushirikiana hapa yatakuwa chachu ya maendeleo kwa kila mmoja wetu na kwa jamii kwa ujumla. Nawatakia kila kheri katika kutekeleza majukumu yenu ya kila siku na tuendelee kushirikiana kama wana Haki Kazi kwa ajili ya ustawi wa pamoja.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akifunga Mafunzo ya Siku mbili kwa Majaji, Watendaji na Wadau wa Mahakama yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) leo tarehe 17 Julai, 2025 katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.

Sehemu ya Majaji, Watendaji na Wadau wengine wa Mahakama ambao ni washiriki wa Mafunzo hayo wakifuatilia hotuba iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (hayupo katika picha).


Sehemu ya washiriki wa Mafunzo wakipokea Vyeti vya ushiriki wa mafunzo kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina. Wanaoshuhudia zoezi hilo wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, wa kwanza kushoto ni Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa, wa pili kulia ni Mwakilishi wa Mtendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na wa kwanza kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, Bi. Getrude Sima.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)


 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni