Alhamisi, 17 Julai 2025

MAHAKAMA MBEYA YAPUNGUZA KERO MASHAURI YA MIRATHI

Na Daniel Sichula – Mahakama, Mbeya

Katika taarifa za ukaguzi zilizotolewa kwenye Mahakama zilizokaguliwa asilimia kubwa ilioneshwa namna mashauri ya mirathi yalivyoshughulikiwa kwa Mahakama zote za wilaya hasa Mahakama ya Rungwe, Kyela na Mahakama ya Mkoa wa Songwe vile vile na Mahakama zake za Mwanzo

Akifanya kaguzi hizo kwa nyakati tofauti Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akiwa ameambatana na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu, Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Mbeya Mhe. Zawadi Laizer pamoja kaimu Mtendaji wa Mahakama Kuu Mbeya Bw. Alintula Ngalile

Jopo hilo la ukaguzi hivi karibuni ilipokea taarifa za ukaguzi Mahakama ya Wilaya ya Rungwe na Kyela na Mahakama zake za Mwanzo zikiwemo Mahakama ya Mwanzo Kiwila, Ikama, Tukuyu Mjini, Katumba, Ipinda, Kyela Mjini na Busale.

Aidha, taarifa hizo zilionesha kufanya vizuri zaidi kwenye kushughulikia mashauri ya Mirathi ambayo kwa mwaka huu kikanda ndiyo ilikua kipaumbele na kulingana na mikakati iliyowekwa ikiwemo kutangaza kwenye vyombo habari na makanisani na kwenye ofisi za kata ilisaidia kuwafikia wadau wengi.

“Inatakiwa Mahakama kufuatilia mirathi na kuhakikisha inalipwa kwa wakati na kupata mrejesho baada ya mchakato mzima wa ulipaji kukamilika,” alisema Mhe. Tiganga akiwa Wilayani Rungwe na Kyela

Aidha, Mhe. Tiganga alipokea taarifa za hali ya majengo na changamoto zake kwani kuna majengo ya baadhi ya Mahakama si yakulizisha mengi ni chakavu na baadhi kutokua na hadhi.

“Ni muhimu kusimamia viwanja vya Mahakama na kuvitambua mipaka yake kwani vikiachwa bila uangalizi ni rahisi kuvamiwa na watu, tuainishe mipaka yake na tuvitafutie hati.” Alisisitiza Mhe. Tiganga

“Nawapongeza Mahakimu kwa kumaliza kesi na kahakikisha magereza halijai mahabusu” alisema Mhe. Tiganga akiwa katika gereza la wilaya Kyela, vile vile alipata wasaa wakutembelea jengo jipya la Magereza kwa wafungwa wanawake.

Wakati huohuo, Mhe. Tiganga alipongeza Mahakimu kwa kuzingatia matumizi ya TEHEMA na uendeshaji wa mashauri kwa njia ya mtandao na kuwasisitiza Mahakimu kuendelea kutumia mifumo ya kimtandao ya Mahakama kuendeshea kesi.

Akiwa wilayani Rungwe Mhe. Tiganga na timu yake walipokelewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Jackson Banobi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Kyela Mhe. Andrew Njau.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Said Kalunde akiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Judith Lyimo walipokea taarifa ya ukaguzi ya Mahakama Mkoa wa Songwe, Mahakama za Wilaya na Mwanzo.

“Hongereni kwa kushughulikia mashauri ya mirathi vizuri naona namba ya ulipaji na ufungaji wa mashauri haya unaenda vizuri, cha kufanya ili tupige hatua zaidi inatakiwa kupunguza milolongo ya kudai mirathi ili tuendelea kushughulikia kwa wakati,” alisema Mhe. Kalunde akiwa na watumishi wa Mahakama mkoa Songwe.

Aidha, Mhe. Kalunde aliwasisitiza Mahakimu walio na mashauri machache kuongeza ubora wa kazi katika usikilizaji wa mashauri na uandishi wa maamuzi hasa kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.

Akiwa Mkoa wa Songwe Mhe. Kalunde alipokelewa na Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Songwe Mhe. Francis Kishenyi pamoja na Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa Songwe Sostenes Mayoka.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akipokelewa na Maafisa magereza katika Gereza la Wilaya ya Kyela Mbeya aliwasili kwa ajili ya ukaguzi, kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Said Kalunde wa pili kulia akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Mahakama Mkoa wa Songwe, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Judith Lyimo na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Songwe Mhe. Francis Kishenyi.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akipokelewa na kusalimia na Maafisa magereza katika Gereza la Wilaya ya Kyela Mbeya aliwasili kwa ajili ya ukaguzi, kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu.

Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Said Kalunde akikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Mahakama Mkoa wa Songwe, kulia ni Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Songwe Mhe. Francis Kishenyi

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga akisaini Kitabu cha wageni katika ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya Rungwe.

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu akiwa anapitia taarifa ya ukaguzi
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Joachim Tiganga (mwenye tai nyekundu) akiwa kwenye picha pamoja na viongozi wa Mahakama na maafisa magereza mara baada ya ukaguzi wa gereza hilo la wilayani Kyela.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni