Jumatano, 16 Julai 2025

MAREHEMU FRANCIS KABWE AZIKWA MAMBA MIAMBA SAME-KILIMANJARO

  • Viongozi, watumishi mbalimbali wa Mahakama na mamia ya watu wajitokeza kwenye mazishi yake
  • Simanzi yatanda

 Na SETH KAZIMOTO, Mahakama-Arusha

Mamia ya watu wamejitokea kumzika aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Francis Kabwe aliyepumzishwa katika nyumba yake ya milele tarehe 13 Julai, 2025.

Marehemu Kabwe alizikwa Kijijini kwao Mamba Miamba wilayani Same Mkoani Kilimanjaro. katika mazishi hayo, mamia ya watu wakiwemo Viongozi mbalimbali wa Mahakama na wananchi wameshiriki kikamilifu kumhifadhi Mhe. Kabwe katika mazishi yaliyotawaliwa na simanzi kubwa kwa ndugu na jamaa waliohudhuria.

Akizungumza na waombolezaji, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alisema kuwa, Mhe. Kabwe atakumbukwa daima kwa utendaji wake wa kazi uliotukuka na kwamba Mahakama ilifanya kila jitihada kuhakikisha anapona, lakini mapenzi ya Mungu yametimia.

Akitoa salamu za Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali alisema kuwa, marehemu Kabwe alikuwa Kiongozi wa pekee kwani alikuwa mnyenyekevu, mwenye busara na moyo wa huduma, alizingatia misingi ya haki, alikuwa mshauri na Mwalimu pia.

“Kwa hakika, tunakusanyika hapa kwa huzuni kubwa na tafakari ya kina tukimuenzi mtu aliyetoa maisha yake katika kuitumikia haki, kuhifadhi utu na kuimarisha mifumo ya sheria hapa Tanzania,” alisema Mhe. Mahimbali.

Akisoma wasifu wa marehemu, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. George Hubert alisema kuwa, marehemu Francis Kabwe alizaliwa tarehe 20 Novemba, 1976 Iringa na kusoma katika Shule ya Msingi Kitangiri, Shule za Sekondari Bulima na Ikizu mkoani Mwanza.

Pia, alisoma shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Tumaini mkoani Iringa na baadae akasoma katika Chuo cha Diplomasia ambapo alipata Shahada ya juu ya Menejimenti ya Mahusiano ya nje.

Marehemu Kabwe aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania mwaka 2003 na kufanya kazi kwa nyadhifa mbalimbali katika Mikoa ya Kilimanjaro, Singida, Mara, Manyara, Dar es Salaam, Mwanza na Arusha. Marehemu Kabwe alifariki dunia tarehe 08 Julai, 2025 katika Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro, marehemu ameacha Mke na Watoto wawili.

Mazishi ya Mhe. Kabwe yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama wakiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali, Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Hubert, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Arusha, Mhe. Amir Msumi na Mtendaji wa Mahakama Kuu Arusha, Bw. Festo Chonya.

Wasajili wa Mahakama ya Tanzania wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa marehemu Francis Kabwe kuelekea eneo la mazishi tarehe 13 Julai, 2025 kijijini Mamba Miamba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akitoa salamu za Mahakama wakati wa mazishi ya aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe.  Francis kabwe aliyezikwa tarehe 13 Julai, 2025 katika Kijiji cha Mamba Miamba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro. Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Bw. Festo Chonya.

Viongozi wa Mahakama wakitoa salamu zao za mwisho kwa mwili wa marehemu Francis Jacob Kabwe. Aliye mbele ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Gabriel, katikati ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na nyuma ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa wakiwa katika Kijiji cha Mamba Miamba wilayani Same Mkoani Kilimanjaro tarehe 13 Julai, 2025.

Msajili Mkuu wa Mahakama, Mhe. Eva Kiaki Nkya (kushoto) akizungumza jambo wakati wa mazishi ya marehemu Francis Kabwe. Katikati ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel na kulia ni Msajili wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. George Hubert.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali (kulia) akiwa na Majaji kutoka Kanda ya Moshi kwa pamoja wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Francis Kabwe wakati wa mazishi yake yaliyofanyika tarehe 13 Julai, 2025 katika Kijiji cha Mamba Miamba wilayani Same mkoani Kilimanjaro.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) na 
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (kulia) wakiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu Francis kabwe aliyezikwa tarehe 13 Julai, 2025 katika Kijiji cha Mamba Miamba wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza)



 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni