Na MARY GWERA, Mahakama-Mwanza
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ametoa ushauri kwa
waajiri wote nchini kuhakikisha wanaweka mazingira salama kwa wafanyakazi wao ili
kuepusha hatari za kiafya mahali pa kazi.
Akizungumza
leo tarehe 16 Julai, 2025 jijini Mwanza wakati akifungua Mafunzo kwa Majaji, Watendaji
na Wadau wa Mahakama yaliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi
(OSHA), Mhe. Dkt. Siyani amesema, usalama na afya
kazini si suala la hiari bali ni haki ya msingi kwa kila mfanyakazi.
“Ili
kusema kwamba mfanyakazi
ana mazingira
salama, ni lazima mazingira hayo yawe na mguso chanya kwa mwili, akili na hisia
zake. Mazingira ya
kazi yanayogusa sehemu
hizi humfanya mfanyakazi aweze kutoa huduma bora, kuwa na morali ya juu na kuchangia kwa ufanisi zaidi
maendeleo ya taasisi na taifa kwa ujumla,” amesema Jaji
Kiongozi.
Amesema kuwa,
mazingira salama ya kazi
si tu yanamlinda mfanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa, bali pia yanachangia
katika kuongeza tija, ubunifu na mshikamano miongoni mwa watumishi hivyo ni
muhimu pia kuhakikisha wafanyakazi wanaelewa kwa mapana mantiki
na umuhimu wa afya na usalama kazini.
Akizungumzia kuhusu Sekta ya Haki, Mhe. Dkt. Siyani ameongeza kwamba, Dhana ya Haki Kazi haiwezi kutenganishwa na dhana ya usalama na afya mahala pa kazi (Occupational Safety and Health).
“Hizi ni dhana mbili zinazoshikamana na hakuwezi kuwa na dhana moja bila nyingine. Dhana ya Haki Kazi ni pana, na inajumuisha ujira wa haki, usawa kazini, ushiriki wa wafanyakazi katika uamuzi, fursa za maendeleo, pamoja na mazingira salama na yenye afya. Mazingira salama ya kazi yanampa mtumishi hali ya utulivu, ujasiri wa kufanya kazi kwa bidii na uwezo wa kutoa huduma zenye viwango vya juu,” amesisitiza Jaji Kiongozi.
Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi amesema, mazingira hatarishi huzaa hofu, huzuni, magonjwa, ajali, changamoto za afya ya akili na hata vifo, mambo ambayo huvunja misingi ya haki kazi.
“Kama nilivyotangulia kusema, suala la usalama na afya mahala pa kazi sio hiari, bali ni wajibu wa waajiri. Hivyo basi, waajiri, ikiwemo serikali wanapaswa kuhakikisha uwepo wa mazingira salama ya kazi na kuelimisha wafanyakazi juu ya namna wanavyoweza kushiriki ili kufaidika na kudumisha mazingira hayo,” ameeleza Mhe. Dkt. Siyani.
Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa, katika dunia inayoendelea kubadilika kwa kasi, ni vema kuendana na maendeleo yanayoletwa na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (Fourth Industrial Revolution) yanayoendeshwa na teknolojia kama Intaneti ya Vitu, Akili Unde, Ukusanyaji wa taarifa na vitu kujiendesha vyenyewe (Automation).
“Ninaamini kuwa, uelewa wa teknolojia hizi si anasa, bali ni hitaji la msingi
kwa taasisi yoyote inayotaka kusalia hai na yenye ushindani katika enzi hizi za kidigitali,” amesema
Mhe. Dkt. Siyani.
Ameongeza kwa kusema kuwa, “pamoja na mambo mengine, kwa siku mbili hizi mtapata wasaa wa kujifunza namna ya kulinda faragha ya taarifa za kazi, matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kurahisisha kazi na kuwa na uelewa juu ya athari za kijamii na kisaikolojia zinazotokana na matumizi ya mifumo ya kidijitali mahala pa kazi. Hili ni jambo la muhimu sana katika zama hizi.”
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina amesema, nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unaoishia mwaka huu 2025, katika utekelezaji wake inalenga pamoja na mambo mengine ushirikishwaji wa wadau.
“Katika kutekeleza hayo, Mahakama Kuu
Divisheni ya Kazi imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa haki kazi. Wakati huu, tumeshirikiana na OSHA katika
kuhakikisha watumishi wa Mahakama na wadau wetu wengine wanapata elimu juu ya
haki kazi na usalama mahali pa kazi,” amesema Mhe. Dkt. Mlyambina.
Jaji Mfawidhi huyo amesema, wamefanya
hivyo kwa kutambua kuwa bila usalama mahali pa kazi hakuna maendeleo endelevu
kwa watumishi kutokana na vihatarishi mbalimbali mahali pa kazi vinavyoweza
kuhatarisha maisha ya wafanyakazi na kupunguza au kudhoofisha nguvu kazi ya
taifa na kufanya taifa lisifikie maendeleo endelevu.
“Nipende kuwashukuru kwa kipekee OSHA kwa
kuonyesha utayari kufanya kazi na sisi katika kusimamia haki kazi ikiwemo
usalama mahali pa kazi, mafunzo hayo ni ya tatu kufanya, tulianza mafunzo ya
kwanza kwa watumishi wenye ulemavu kutoka ndani na nje ya mahakama mwezi Desemba,
2024 Jijini Dodoma,” amesema Mhe. Dkt. Mlyambina.
Ameongeza kuwa, mafunzo ya pili
yalifanyika Jijini Dodoma mwezi Aprili mwaka huu na yalihusisha watumishi
kutoka Kanda za Dodoma, Kigoma Tabora na Singida. Mafunzo hayo yalihudhuriwa na
jumla ya watumishi 70 walinufaika na mafunzo hayo.
Aidha, Jaji Mfawidhi amesema kwamba,
mafunzo ya awamu hii yanayofanyika jijini Mwanza yamegawanywa katika makundi
mawili yaani kundi la viongozi washiriki 110 na kundi la watumishi wasaidizi wa
viongozi washiriki 90.
Baada ya hafla ya uzinduzi wa mafunzo
hayo kumefanyika tukio la utiaji saini kwa Hati ya Ushirikiano (Memorandum of
Understanding) kati ya Mahakama ya Tanzania na OSHA yenye lengo la kufanya
mafunzo kwa pamoja kwa nchi nzima kwa kipindi cha miaka miwili.
Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha
uelewa wa Sheria ya Afya na Usalama Kazini na kanuni zake, kuongeza uwezo wa kushughulikia
migogoro ya kazi, kuendeleza utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Kazi na kutilia
mkazo sheria zinazosimamia ustawi wa wafanyakazi.
Amesema, Hati hiyo ya mashirikiano
imegawanya mafunzo hayo kwa kanda mbalimbali. Mafunzo hayo pia yatajumuisha
mafunzo ya watumishi wenye ulemavu mara moja kwa mwaka.
Mhe. Dkt. Mlyambina ameongeza kuwa,
utekelezaji wa makubaliano hayo utatimizwa na wadau wengine wa Haki Kazi kama
Kamishna wa kazi, Wakili Mkuu wa Serikali, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali,
Shirika la Kazi Duniani (ILO), CMA, LESCO, TUCTA, ATE na mifuko ya hifadhi ya
jamii katika majukumu mbalimbali yaliyoainishwa kwenye makubaliano hayo.
Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wakala
wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Joshua Matiko amesema, OSHA kwa
kushirikiana na Mahakama imeona ni vyema kuwa na mashirikiano rasmi katika maeneo
manne ambayo ni pamoja na kuimarisha uelewa wa Sheria ya Afya na Usalama mahali
pa kazi, kuongeza uwezo wa kushughulikia migogoro ya kazi, kuboresha
utekelezaji wa sheria za kazi na kanuni zake na mengine.
Washiriki wa mafunzo hayo ni pamoja na Majaji, Naibu Wasajili, Wasaidizi wa Sheria wa Majaji, Watendaji wa Mahakama kutoka Mwanza, Shinyanga, Geita, Bukoba na Musoma, Kamishna wa Kazi, Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Wakili Mkuu wa Serikali, Madereva na Walinzi wa Viongozi hao.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo kwa Majaji, Watendaji na Wadau wa Mahakama leo tarehe 16 Julai, 2025 kwenye Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.
Majaji, Watendaji na Wadau wa Mahakama wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo iliyokuwa ikitolewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani (hayupo katika picha).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo kwa Majaji, Watendaji na Wadau wa Mahakama yanayofanyika katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Joshua Matiko katika picha ya pamoja baada ya kusaini hati za makubaliano ya ushirikiano kati ya Taasisi hizo.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akipokea tuzo kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Joshua Matiko ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika eneo la Haki Kazi.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Joshua Matiko ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika eneo la Haki Kazi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Joshua Matiko ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika eneo la Haki Kazi.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (kushoto) akipokea tuzo kutoka kwa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bw. Joshua Matiko ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika eneo la Haki Kazi.
Meza kuu ikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani wakiwa katika picha za pamoja na sehemu ya washiriki wa Mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni