Na Mwandishi Wetu, SINGIDA
Chama
cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF) wameandaa na kuendesha kikao kazi cha siku mbili kwa
wanachama wa Chama hicho tawi la Mahakama ya Rufani.
Akizungumza
leo tarehe 15 Julai, 2025 mkoani Singida na Wajumbe wa kikao kazi hicho kwa
niaba ya Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija amesisitiza
ushirikiano imara kati ya NSSF na wadau hasa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) umekuwa kichocheo kikubwa cha mafanikio ya Mfuko huo na wanachama wa TMJA.
“Ushirikiano huu unatoa nafasi ya kujadili changamoto kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kubuni njia bora za kuimarisha huduma kwa wanachama,” amesema Mhe. Mwarija.
Mhe. Mwarija amepongeza waandaaji wa kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA) kwa kushirikiana na NSSF, na kusema kuwa, kufanyika kwa kikao hicho ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2020/2021–2024/2025), hususani nguzo ya tatu inayolenga ushirikishwaji wa wadau katika utoaji wa haki.
Ameongeza kuwa, changamoto kama za mirathi zinahitaji
kushughulikiwa kwa pamoja kwa kuweka mifumo ya pamoja inayotambua wategemezi na
kuharakisha utoaji wa haki.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania, Mhe. Elimo Massawe ameishukuru NSSF kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa TMJA uliowezesha kufanyika kwa kikao kazi hicho.
Mhe. Massawe amesisitiza kuwa, Chama hicho kitaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha weledi na ufanisi wa wanachama wake unakua kila uchao.
Kadhalika, amewajuza wajumbe wa mkutano huo kuwa, mkutano wa Baraza Tendaji uliofanyika jana tarehe 13 Julai, 2025 mkoani Singida umeazimia pamoja na mambo mengine kuwa, Jina la Chama limebabilishwa kutoka Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) kuwa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA).
Mhe. Massawe ameeleza kwamba, sababu kubwa ya kubadili jina hilo ni kupisha matumizi ya ufupisho wa awali kwa JMAT kwa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania ambao wakati wanasajili Taasisi yao hii walisajili na ufupisho huo wakati TMJA iliposajili haikusajili na ufupisho huo.
Azimio la pili ni kuundwa kwa tawi jipya la Divisheni litakalojumuisha Divisheni za Mahakama Kuu, Kituo cha Usuluhishi na Kituo Jumuishi cha mashauri ya Ndoa na familia Temeke. Hatua hiyo ni kutokana na sababu kuwa kabla ya Mahakama kuhamia Dodoma Divisheni zote na Kituo cha usuluhishi vilikuwa ni sehemu ya tawi la Masjala Kuu.
Mhe. Massawe amesema kuwa, kutokana na masjala kuu
kuhamia Dodoma iliazimiwa na mkutano mkuu kuwa liundwe tawi jipya la Divisheni
na kuboresha muundo wa Tawi la Masjala kuu na Tawi la Mahakama ya Rufani.
"Kwa muundo mpya sasa imeazimiwa kuwa Tawi la Mahakama ya Rufani litawajumuisha Majaji wa Mahakama ya Rufani, Msajili Mkuu, Msajili na Naibu Wasajili wa Mahakama ya Rufani pamoja na Wasaidizi wa Sheria wa Mahakama ya Rufani," amesema Mhe. Massawe.
Ameongeza kwamba, Naibu Wasajili na Mahakimu walioko kwenye Kurugenzi mfano ya Usimamizi wa Mashauri, Idara ya Ukaguzi na Maadili, Maktaba, Wizara ya Katiba na Sheria, Kitengo cha Maboresho cha Mahakama, na kadhalika watakuwa wanachama wa tawi la Masjala Kuu.
Amewapongeza wanachama wote waliojiunga na mfuko wa FARAJA JMAT FUND na kuwahimiza wale ambao bado
hawajajiunga wajiunge kwani dhumuni kubwa ni kuwa na TMJA moja yenye umoja.
Amebainisha kuwa, mkutano mkuu ujao utakuwa wa wanachama
wote badala ya uwakilishi na unatarajiwa kufanyika ifikapo tarehe 13 hadi 15
Januari, 2026.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba ameeleza kuwa tangu mwaka 2018 Serikali ilipofanya uboreshaji mkubwa wa sheria, NSSF imekuwa chombo pekee kinachotoa huduma za hifadhi ya jamii kwa sekta binafsi na waliojiajiri.
"Mwaka 2024, kupitia mabadiliko ya Sheria ya NSSF (Sura ya 50), wanachama sasa
wanaweza kuchangiwa na zaidi ya mwajiri mmoja, vipindi vya uchangiaji vya zaidi
ya miaka 60 vinazingatiwa, adhabu ya kuchelewesha michango imepunguzwa kutoka
asilimia tano hadi 2.5, na waliojiajiri sasa wanaweza kujiunga kupitia mpango wa
lazima (mandatory)," amesema Bw. Mshomba.
Bw.
Mshomba ameeleza kuwa, thamani ya Mfuko imeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka
Shilingi trilioni 4.8 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 9.6 hadi
kufikia Juni 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 98. Aidha, michango ya
wanachama imeongezeka kutoka trilioni 1 hadi trilioni 2.16 huku mapato ya
uwekezaji yakipanda kutoka Shilingi bilioni 527.1 hadi bilioni 543.5.
Mafanikio mengine yaliyoelezwa ni pamoja na ongezeko la thamani ya vitega uchumi vya Mfuko kufikia trilioni 8.2 kutoka trilioni 7.4. Vilevile, mafao ya wanachama yaliyolipwa yamefikia Shilingi bilioni 947.2 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 884.8 mwaka uliotangulia, ongezeko la asilimia 7.
Ameongeza kuwa, NSSF pia inalenga kulipa mafao ndani ya saa 24 pindi mwanachama
anapostaafu, hatua inayowezekana kupitia uboreshaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo kwa sasa
huduma za Mfuko zinatekelezwa kwa asilimia 90 kwa njia ya kidijitali.
Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025, NSSF imefikisha wanachama wachangiaji 1,816,026 kutoka 1,358,882 mwaka uliotangulia, ongezeko la asilimia 19. Ongezeko hili limetokana na mabadiliko ya sheria ambayo sasa yanamruhusu kila Mtanzania analiye katika shughuli za kujiajiri kujiunga na hifadhi ya jamii, hivyo kuimarisha uhakika wa kipato kwa Watanzania wote kwa kuwa na akiba ya uhakika na kuwa mnufaika wa hifadhi ya jamii muda utakapofika.
Bw. Mshomba
amesema pamoja na mambo mengine, mazingira mazuri ya kisera yaliyoanzishwa na
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamechangia
mafanikio ya Mfuko.
Pamoja
na mafanikio hayo, changamoto bado zipo. Bw. Mshomba alibainisha kuwa, baadhi ya
waajiri hawawasilishi michango kwa wakati au huwasilisha kwa kiwango kidogo
tofauti na kiasi halisi wanachowalipa wafanyakazi wao. Hata hivyo, elimu
inaendelea kutolewa kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu umuhimu wa hifadhi ya
jamii, kuwasilisha michango sahihi na kwa wakati.
Naye, Mwenyekiti
wa TMJA Tawi la Mahakama ya Rufani, Mhe. Shaabani Ally Lila ambaye pia ni Jaji
wa Mahakama ya Rufani, aliishukuru NSSF kwa kuandaa kikao kazi hicho ambacho
kimelenga kushirikisha wadau muhimu katika kuhakikisha haki za wanachama
zinalindwa. Ameongeza kuwa, kikao kazi hicho ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano
na kuhakikisha mafao ya wastaafu yanalipwa kwa wakati na haki.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mahakama ya Rufani, Mhe. Bupe Abonike Kibona amesema kuwa, kikao kazi hicho kimewapa maarifa ya kina kuhusu taratibu za NSSF, jambo litakalosaidia kushughulikia mashauri ya hifadhi ya jamii kwa haraka na kwa usahihi zaidi. Aliongeza kuwa mpango wa Hifadhi Scheme wa NSSF ni hatua chanya inayowawezesha Watanzania wote kujiunga na kunufaika na mafao mbalimbali ya hifadhi ya jamii.
Kikao
kazi kati ya TMJA na NSSF kinachofanyika mkoani Singida, kimehudhuriwa na
Majaji wa Mahakama ya Rufani, Wasajili, Mahakimu, pamoja na watendaji wa NSSF,
kikiongozwa na kaulimbiu isemayo “Utoaji Haki kwa Wakati kwa Ustawi wa Hifadhi
ya Jamii.”
Picha za mbalimbali za makundi wakati wa kikao hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni