Jumatatu, 14 Julai 2025

JAJI MFAWIDHI MOROGORO AFURAHISHWA NA KASI UTENDAJI KAZI WA WADAU HAKI JINAI

Na ASHA JUMA-Mahakama, Morogoro

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim, ameonesha kuridhishwa na kasi ya usikilizaji wa mashauri ya jinai pamoja na ushirikiano mzuri kutoka kwa Wadau wa mnyororo wa haki jinai mkoani Morogoro.

Mhe. Ebrahim alitoa pongezi hizo wakati wa kikao maalum cha kusukuma mashauri ya jinai (Case Flow Management) kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Mikutano kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro.

Kikao hicho kililenga kutathmini mwenendo wa usikilizaji wa mashauri ya jinai na kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza mlundikano.

Akiongoza kikao hicho, Jaji Mfawidhi alieleza kuwa mafanikio yaliyofikiwa kwa sasa yanatokana na jitihada za pamoja za Wadau na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano-TEHAMA- katika uendeshaji wa mashauri.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ebrahim alisisitiza umuhimu wa kutumia nyenzo mbalimbali katika utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya kimahakama.

Alieleza kuwa ni muhimu wananchi waelimishwe kuhusu matumizi ya TEHAMA, faida za adhabu mbadala na mchakato wa kukata rufaa. Mhe. Ebrahim alibainisha kuwa utoaji wa elimu hiyo usisubiri matukio maalum kama Siku ya Sheria au sherehe nyingine, bali ufanyike kwa njia endelevu. 

“Tunapaswa kutoa elimu kwa jamii kwa kutumia nyenzo mbalimbali bila kusubiri siku maalum kama Siku ya Sheria na sherehe nyingine,” alisema Jaji Mfawidhi.

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Susan Kihawa, alieleza hali ya Magereza mkoani humo baada ya kuyatembelea. Alibainisha kuwa kati ya Magereza nane, hakuna lililo na msongamano, huku Magereza ya Kihonda, Kingolwira (la wanawake) na Mtego wa Simba yakiweka mkakati wa kununua vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kujiunga na mfumo wa Mahakama Mtandao (Virtual Court).

Hata hivyo baadhi ya changamoto tulizokutana nazo zinashughulikiwa ikiwemo ucheleweshaji wa taarifa za wafungwa wanaohama Magereza kutoka Mikoa mingine,” alisema Mhe. Kihawa.

Wadau mbalimbali wa haki jinai walihudhuria kikao hicho wakiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), TANAPA, Uhamiaji, TAKUKURU, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro, Maofisa Ustawi wa Jamii, Maofisa Uangalizi wa Jamii na watoa huduma za msaada wa kisheria.

Katika kikao hicho, wadau waliazimia mambo muhimu kama kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya, kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wafungwa wanaohamia kutoka maeneo mengine na kuandaa mkakati wa elimu kwa jamii kuhusu ukatili wa kijinsia na usalama wa watoto.

Wadau hao pia walipongeza matumizi ya TEHAMA katika kazi zao, wakieleza kuwa yameongeza kasi, kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki, hususan kwa mashahidi wanaosafiri kutoka mbali.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Rose Ebrahim akiongoza kikao maalum cha kusukuma mashauri ya jinai (Case Flow Management).

 

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Susan Kihawa, akieleza ripoti yake katika kikao hicho.

 Baadhi Wadau wa haki jinai waliohudhuria kikao hicho.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni