Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Biashara wa
Kampuni ya Masuala ya Mifumo kutoka Italia, Bw. Franco Martino leo tarehe 14
Julai, 2025 amemtembelea Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante
Ole Gabriel na kufanya naye mazungumzo mafupi yenye lengo la kuendeleza
ushirikiano kwenye maeneo yanayohusu mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
[TEHAMA].
Bw. Franco amekutana na Prof.
Ole Gabriel katika ofisi ndogo iliyopo kwenye jengo la Mahakama ya Rufani
jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri,
Mhe. Desdery Kamugusha, Mkurugenzi wa TEHAMA, Bw. Enoc Kaleghe na Wataalam
wengine kutoka Mahakama ya Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa.
Mkurugenzi huyo kutoka
Kampuni ya Almawave amekutana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ili kuendelea
kukubaliana kuhusu namna gani ya kuweza kuendeleza mahusiano ya kibiashara kuhusu
Mfumo wa Tafsiri na Unukuzi [Translation and Transcription Software-TTS].
Mfumo wa TTS unasaidia
kupunguza jukumu kubwa la Majaji na Mahakimu kuandika mienendo ya mashauri au
hata kutayarisha nakala za hukumu kwa mkono.
Ikumbukwe kuwa Mei 2022,
Mahakama ya Tanzania iliingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kuuziwa
mifumo ya tafsiri na unukuzi.
Hivyo Bw. Franco
amekutana na Prof. Ole Gabriel ili kupitia kwa pamoja muhtasari wa mambo gani
mahsusi na muhimu kwa ajili ya kuendelea kuboresha.
Kadhalika, Mkurgenzi huyo
amekuja kuiomba Mahakama ya Tanzania kuona jinsi gani inaweza kuendelea
kuhabarisha Taasisi nyingine ambazo zinaweza kuhitaji kutumia mifumo kama hiyo
ili waweze kuitumia.
Kwa upande wake, Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania amemhakikishia Mkurugenzi huyo ushirikiano wa
kutosha na kuomba mafunzo endelevu kwa Wataalam wa ndani na pia watumiaji wa
mfumo wa TTS, hususan Majaji, Naibu Wasajili na Mahakimu ili matumizi ya mfumo
huo yaende sambamba na mabadiliko yanayofanyika mahakamani.
‘Tungetamani siku za
mbele watalaam wetu wa ndani hususan wale wa TEHAMA chini ya Mkurugenzi wao,
Bw. Enoc Kaleghe waweze kuelewa na kutambua jinsi gani ya kusimamia na kubuni uboreshaji
katika mifumo hii,’ amesema.
Prof. Ole Gabriel
amemshukuru kwa kipekee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.
Samia Suluhu Hassan ambaye kwa hakika ameridhia na amekuwa akitoa fedha za
kutosha kwa ajili ya kuboresha mifumo ya TEHAMA.
Ameeleza kuwa mifumo ya TEHAMA
ikiboreshwa hushajiisha kasi na ubora wa utoaji wa haki kwa wakati na kwa
gharama nafuu.
Kadhalika, Mtendaji Mkuu
amemshuku Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju kwa
usimamizi wake anaoendeleza matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli za kimahakama.
Ametoa wito kwa
Watanzania kuwa tayari kuendana na mabadiliko yanayoendelea ndani ya Mahakama ya
Tanzania kwa ajili ya matumizi ya TEHAMA kwani zama za kutuma karatasi na
mifumo ya zamani, imepitwa na wakati na Mahakama inazidi kwenda na teknolojia
ya kisasa.
Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya Masuala ya Mifumo kutoka Italia, Bw. Franco Martino [kushoto] akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel walipokutana leo tarehe 14 Julai, 2025 jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni