· Jaji Mfawidhi Dkt. Mlyambina aainisha faida lukuki za Juzuu
Na MARY GWERA, Mahakama-Dar es Salaam
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju jana tarehe 25 Agosti, 2025 alizindua juzuu mbili za maamuzi ya Mahakama Kuu kuhusu migogoro ya kazi nchini lengo mojawapo likiwa ni kusaidia kutoa mwongozo wa moja kwa moja kwa vyombo vya chini kama vile Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) pamoja na Mahakama ya Kazi yenyewe.
Juzuu ya kwanza ni ya kipindi cha 2010 hadi
2022, na ya pili ikihusu miaka ya 2023 hadi 2024 ambazo zimekusanya kwa pamoja
maamuzi muhimu yaliyotolewa na Mahakama Kuu katika muktadha wa kuendesha na
kuamua mashauri ya kikazi.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tisa ya Kamati ya Utatu (Tripartite Users Committee) jijini Dar es Salaam, Mwenyeji wa shughuli hiyo ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina amesema uchapishaji wa Juzuu hizo umefadhiliwa na Wadau wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF na kuchapishwa na Elite Publishers’.
“Maamuzi ya Mahakama Kuu bado yana uzito mkubwa wa
kisheria kwa sababu yana sifa ya kuripotiwa (reportable decisions), uwepo wa
juzuu hizi ni msaada mkubwa kwa Majaji, Wasuluhishi na Waamuzi katika kutoa
maamuzi yaliyojengeka katika misingi ya kanuni, tafsiri, na maamuzi
yaliyokwishatolewa,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.
Alisema kuwa, Juzuu hizo zitawaongoza wanasheria,
watetezi wa haki kazi, wanafunzi, watafiti na wanazuoni wa sheria kuelewa
mwenendo wa tafsiri za kisheria katika migogoro ya ajira.
“Mahakama ya Kazi ni Kitengo maalum (Specialized
Division), hivyo, ina wajibu wa kukuza sheria (jurisprudence) na hasa kwa
kuzingatia kwamba sheria zetu za kazi bado ni changa na zinakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukuaji wa teknolojia na akili unde,”
ameeleza Mhe. Dkt. Mlyambina.
Aliongeza kwamba, japokuwa Divisheni ya Kazi
inasikiliza migogoro ya kazi pekee, kupitia Tangazo la Serikali Namba 209 la
2010 Mahakama Kuu Kanda zote isipokuwa Kanda ya Dar es Salaam na Divisheni nazo
zinasikiliza migogoro ya Kazi. Hivyo juzuu hizo zikitumika kama rejea na kusaidia
kupunguza maamuzi kinzani.
“Juzuu hizi zikitumika kama rejea zitasaidia kuona
takwimu za maamuzi yote yaliyoamriwa kwa kuchochea ukuaji wa Uchumi sanjari na
matakwa ya kifungu cha 3 (a) Cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini
kinachoelekeza kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia ufanisi wa kiuchumi,
uzalishaji na haki ya kijamii,” alisisitiza Jaji Mfawidhi huyo.
Mbali na faida hizo, Jaji Mlyambina aliongeza kuwa,
juzuu hizo zitatumika kama kumbukumbu ya maamuzi ya Mahakama ya Kazi kwa ajili
ya rejea ya sasa na hata nyakati za baadae endapo kutakuwa na mabadiliko ya
sheria za kazi na kwamba zitasaidia katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali za
sheria za kazi ndani na nje ya nchi.
Kadhalika, alisema kuwa, juzuu zinasaidia kuonesha
namna nchi inavyotekeleza mikataba ya kimataifa, inasaidia pia kuonesha hali
halisi ya sheria za kazi na zinavyotafsiriwa nchini, hivyo kuhamasisha
uwekezaji nchini kwa maendeleo endelevu kufikia Dira ya Taifa 2050.
“Juzuu hizi zitasaidia kuonesha mapungufu mbalimbali yaliyopo katika sheria zetu za kazi na hivyo kuchochea mabadiliko, hata kama ikitokea maamuzi ya Mahakama Kuu yamebatilishwa na Mahakama ya Rufani, inatokea nyakati ambapo si uamuzi wote unakuwa umebatilishwa, hivyo kipengele au vipengele ambavyo vinakuwa havijaguswa huendelea kuwa mwongozo sahihi.” Alieleza Mhe. Dkt. Mlyambina.
Kwa mujibu wa Mhe. Dkt. Mlyambina Juzuu hizo zinapatikana katika mfumo wa nakala ngumu na kwa njia ya mtandao/kielektroniki kupitia 'QR Code'.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju (kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa moja ya Juzuu mbili wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Tisa ya Kamati ya Utatu (Tripartite Users Committee) iliyofanyika jana tarehe 25 Agosti, 2025 katika Ukumbi wa PSSSF jijini Dar es Salaam. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni