Na YUSUFU AHMADI-IJA, Lushoto
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule, hivi karibuni aliongoza
waombolezaji kwenye maziko ya aliyekuwa mama mzazi wa Jaji wa Mahakama Kuu
Divisheni ya Ardhi, Mhe. Nehemia Ernest Mandia, Bi Alice Mandia, aliyefariki Dunia
Agosti 20, 2025 katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.
Bi. Mandia, ambaye alijaliwa
kuishi hapa duniani kwa miaka 90, akiwa alizaliwa Septemba 17, 1935, alizikwa Agosti
25, 2025 majira ya jioni pembeni mwa makaburi ya mumewe, Jaji Mstaafu wa
Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Ernest Mandia na mwanaye Julius Mandia.
Katika salamu zake zilizosomwa
kwa niaba yake na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Gerson Mdemu, Jaji Mkuu wa Mahakama
ya Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju, aliwapa pole wafiwa na kubainisha kuwa
uongozi wa Mahakama upo pamoja nao katika kipindi hiki cha majonzi.
Naye Mhe. Mteule alitoa
salamu za Mahakama Kuu ya Tanzania na kuwasihi wafiwa kuwa na subira katika
kipindi hiki kigumu cha kumpoteza mpendwa wao.
Kwa upande wake, Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kilishiriki kikamilifu katika maziko hayo
ambapo Mkurugenzi wa Mafunzo ya Kimahakama, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda alimwakilisha
Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.
Mhe. Dkt. Kisinda alisema
kuwa uongozi wa Chuo umepokea kwa majonzi makubwa kufuatia kifo hicho na
kuahidi kuendelea kushirikiana na wafiwa katika kipindi chote cha maombolezo.
Askofu wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt.
Msafiri Joseph Mbilu aliongoza ibada hiyo ya maziko na kuwahimiza waombolezaji
kutenda mema na kutowafanyia Watoto ukatili.
Viongozi wengine
wakiwemo Makatibu Wakuu wa Wizara, Viongozi wa Mkoa wa Tanga na Wilaya ya
Lushoto pamoja na wananchi kwa ujumla walihudhuria maziko hayo yaliyofanyika katika
Kata ya Magamba.
Wasifu wa marehemu unaonesha kuwa Bi Alice alijaliwa kupata watoto 10 na wajukuu kadhaa. Aidha, wasifu huo unaonesha kuwa enzi za uhai wake, Mama Mandia alifanya kazi za uuguzi na alistaafu utumishi wa umma mwaka 1985.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe. Zephania Sumaye akitoa salamu za rambirambi kwenye maziko hayo.
Mkurugenzi wa Mafunzo
ya Kimahakama wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Patricia
Kisinda akiwasilisha salamu kwa niaba ya Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni