Ijumaa, 29 Agosti 2025

SHUGHULIKIENI IPASAVYO MASHAURI YA UCHAGUZI KUREJESHA IMANI YA UMMA KWA MAHAKAMA; JAJI KIONGOZI

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani ametoa rai kwa Majaji wa Mahakama Kuu nchini kuwa, namna watakavyotimiza wajibu wao ipasavyo katika utatuzi wa migogoro ya mashauri yanayotokana na uchaguzi inaweza kuwa fursa mojawapo ya kurejesha imani ya umma kwa Mahakama.

Akitoa neno fupi la utangulizi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi yanayotolewa kwa Majaji wa Mahakama Kuu jana tarehe 28 Agosti, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Siyani alisema kuwa, katika jamii kuna baadhi ya watu hawana imani na taasisi mbalimbali za Umma ikiwemo Mahakama, ambapo malalamiko mengi yanahusishwa na huduma zinazotolewa.

“Sote tunafahamu tarehe 29 Oktoba, 2025 kutakuwa na uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hivyo tunapojiandaa kupokea na kusikiliza mashauri ya uchaguzi ni lazima kujua kuwa mashauri ya uchaguzi ni moja kati ya maeneo oevu kwa malalamiko, kwahiyo hatuna budi kutimiza wajibu wetu katika namna itakayohakikisha haki inapatikana lakini tunajenga imani ya Mahakama kwa umma, hili nadhani ni jambo la msingi sana," alisema Jaji Kiongozi.

Alisisitiza kwamba, Mahakama ndio Chombo pekee chenye kauli ya mwisho kwenye utoaji haki kwa mujibu wa Ibara ya 107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa msingi huo Mahakama inayo wajibu wa kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi kwenye migogoro inayotokana na uchaguzi.

“Katika kutimiza wajibu huo, yapo masharti ya kikatiba yanayopaswa kuzingatiwa na Mahakama ikiwemo kutenda haki bila kujali hali ya kijamii, nafasi ya mtu kiuchumi kwa pande zote,ni kuhakikisha kuwa, usikilizwaji na uamuzi wa mashauri ya uchaguzi unakuwa ni wa haki, haraka kadri inavyopaswa na pia kutochelewesha haki bila sababu ya msingi na zaidi kutofungwa na masharti ya kiufundi ambayo yanaweza kukwamisha utoaji haki,” alisema Mhe. Dkt. Siyani.

Akizungumzia kuhusu mafunzo hayo muhimu, Jaji Kiongozi alisema kuwa, “mimi naamini mafunzo haya yamepangwa kwa wakati muafaka, ambapo sote kama ambavyo tunavyofahamu Taifa letu linaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.”

Alisema kwamba, uchaguzi ni mchakato unaohusisha ushindani baina ya watu kutoka kwenye vyama tofauti tofauti vya kisiasa, migororo inayotokana na ushindani huo imekuwa ikisababisha mashauri hayo kuwa na mvuto wa aina yake kwa umma, ni kwa msingi huo matarajio ya wananchi kwa Mahakama huwa ni makubwa.

Aliongeza kuwa, mafunzo hayo yamelenga kubadilishana uzoefu juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Naibu Wasajili na Mahakimu Wafawidhi wa ngazi zote na hivyo kujengeana uwezo wa jinsi ya kushughulikia mashauri ya aina hiyo.

Mhe. Dkt. Siyani alisema kuwa, mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa Majaji ambao waliteuliwa baada ya chaguzi zilizopita kujua changamoto zinazojitokeza katika uendeshaji wa mashauri yanayotokana na chaguzi hizo, kufahamu kwa kina sheria za sasa za uchaguzi na usimamizi wa mashauri hayo.

“Ni matumaini yangu kuwa, mafunzo haya yatawawezesha kuwa na viwango vya juu vya weledi, uwajibikaji na maadili zaidi katika kutimiza majukumu yenu, niwasihi Majaji kuwa tayari kupokea na kubadilishana uzoefu kwenye mada zitakazojadiliwa ili matokeo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa,” alisema Mhe. Dkt. Siyani.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani akitoa neno wakati wa hafla ya ufunguzi wa Mafunzo ya Namna Bora ya Uendeshaji wa Mashauri ya Uchaguzi kwa Majaji wa Mahakama Kuu jana tarehe 28 Agosti, 2025 kwenye ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.



Sehemu ya Majaji Wafawidhi pamoja na Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni