Ijumaa, 17 Oktoba 2025

MAFUNZO ELEKEZI KWA MAHAKIMU WAPYA YAHITIMISHWA

  • Msajili Mahakama ya Rufani awataka kuzingatia maadili, viapo vyao
  • Awakumbusha kazi ya uhakimu ni nyeti, haiwezi kufanywa na mtu yoyote

Na FAUSTINE KAPAMA na HALIMA MNETE-MAHAKAMA, Dodoma

Mafunzo elekezi ya siku tisa yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania, kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto [IJA], kwa Mahakimu Wakazi wapya 89 yamehitimishwa leo tarehe 17 Octoba, 2025.

Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert amehitimisha mafunzo hayo yaliyokuwa yanafanyika kwenye moja ya Kumbi za Mikutano zilizopo katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mhe. Herbert amewaeleza Mahakimu hao walioapishwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, hivi karibuni kuwa anaamini mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa tarehe 7 Octoba, 2025 yamekuwa ya mafanikio makubwa kwao.

‘Nimatumaini yangu kwamba katika siku tisa za mafunzo mmeweza kupata uelewa mkubwa wa viwango vya kitaaluma na kimaadili kwa nafasi mnayoenda kufanyia kazi. Napenda kuwakumbusha na kuwasisitiza kuzingatia yale yote mliyofundishwa, iwe kwa upande wa weledi wa kitaaluma au kwa upande wa unyoofu wa kimaadili,’ amesema.

Msajili wa Mahakama ya Rufani amewaeleza washiriki hao kuwa pande hizo mbili zina umuhimu kwa Hakimu kwani zinategemeana. Amesema kuwa Mahakama bora inajengwa na Maofisa wa Mahakama wenye weledi wa kutosha na maadili ya kiwango cha juu.

Mhe. Herbert amesema kuwa matendo ya kila mmoja wao yanaweza kuinua au kuharibu taswira ya Mahakama nzima kwa jamii ambao ndiyo wanailenga katika kuihudumia. Amewasihi kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na kuishi kwa viapo vyao.

Amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo kuwa kazi ya uhakimu ni nyeti, muhimu na ya kipekee na kwamba haipo sawa na kazi nyingine yoyote. Huku akinukuu kutoka kwenye maandiko matakatifu, Msajili wa Mahakama ya Rufani amewaeleza Mahakimu hao kuwa kazi ya uhakimu inatoka kwa Mwenyezi Mungu.

‘Hivyo nyinyi Mahakimu mmekasimiwa mamlaka haya na Mwenyezi Mungu ili mtende kazi yake ya kutoa uamuzi mkiwa hapa duniani, huku mkijua uamuzi wenu utapimwa na Mwenyezi Mungu. Kazi hii ya uhakimu muichukulie kwa uzito mkubwa, umakini na uadilifu wa hali ya juu,’ amesema.

Mhe. Herbert alimnukuu pia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliwahi kusema kwamba kazi ya uhakimu au ujaji siyo kazi ambayo inaweza kufanywa na mtu yoyote, ni kazi ambayo inahitaji umakini, uadilifu na kuwa na fikra tofauti na watu wengine.

Ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kwa kutoa kibali cha kufanyika na kwa yeye mwenyewe kufungua mafunzo hayo.

Kadhalika, Mhe. Herbert ametoa shukrani kwa IJA, chini ya Uongozi wa Mkuu wa Chuo Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, kwa kuandaa na kuratibu mafunzo hayo kuanzia yalipoanza hadi kufikia tamati.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mafunzo wa IJA, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda amewashukuru Mahakimu hao kwa kushiriki kikamilifu kwenye mafunzo hayo ya wiki mbili.

‘Sisi kama IJA kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania tunajisikia fahari kuwa mafunzo haya yameleta ufahamu na maarifa ya kutosha kwa washiriki na imekuwa wakati mzuri kwao kukaa Dodoma na kufurahia mazingira yake,’ alisema.

Mhe. Dkt. Kisinda aliwapongeza wawezeshaji wa mafunzo hayo ambapo jumla ya mada 27 ziliwasilishwa. Amewaeleza washiriki kuwa watakubaliana na yeye kwamba maarifa waliyopata ni matokeo ya ujuzi na uzoefu wa kina ambao wawezeshaji wameupata wakati wa utumishi wao mahakamani.


Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo elekezi yaliyokuwa yanatolewa kwa Mahakimu Wakazi wapya 89 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda akizunguza kwenye hafla hiyo.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo [juu na chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri. 


Sehemu nyingine ya washiriki wa mafunzo hayo [juu na chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri. 


Sehemu nyingine ya tatu ya washiriki wa mafunzo hayo [juu na picha mbili chini] ikifuatilia kilichokuwa kinajiri. 




 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni