Ijumaa, 17 Oktoba 2025

TANZIA; NAIBU MSAJILI MAHAKAMA KUU DIVISHENI YA BIASHARA, MHE DKT. ANGELA TEYE AFARIKI DUNIA

Mhe. Dkt. Angela Benedict Teye enzi za uhai wake.

                                               TANZIA

Mahakama ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha Mtumishi wake, aliyekuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara. 

Kwa mujibu wa Mtendaji wa Mahakama, Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Bw. Anatory Kagaruki Marehemu Dkt. Angela Teye alifikwa na umauti tarehe 16 Oktoba, 2025 katika Hospitali ya John Muir 'Medical Center' iliyopo Walnut Creek mjini California nchini Marekani alipokuwa akipatiwa matibabu.

Bw. Kagaruki amesema taratibu na mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa na familia.

Marehemu Dkt. Teye aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania kwa Cheo cha  Hakimu Mkazi tarehe 29 Juni, 2007 na kupangiwa Kituo cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga.

Mwaka 2012, marehemu Dkt. Teye aliteuliwa kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na alipangiwa kituo katika Divisheni ya Biashara Masjala ndogo Arusha.

Baada ya hapo alitumikia wadhifa huo katika Vituo vya Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mahakama Kuu Kituo cha Usuluhishi, Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri (DCM) na mnamo Mei 2025, alihamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara alipotumikia hadi umauti ulipomkuta.

Mahakama ya Tanzania inaungana na ndugu, jamaa na marafiki katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza msiba huo mzito wa kuondokewa na Mpendwa wetu.

BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE.

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni