Jumanne, 21 Oktoba 2025

MAHAKAMA, OFISI YA MKUU WA MKOA TABORA WAKABIDHI KOMPYUTA GEREZA KUU UYUI KURAHISISHA UENDESHAJI MASHAURI

  • Jaji Mfawidhi aishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora kwa kutoa vifaa hivyo
  • Asema vitasaidia kurahisisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo

Na AMANI MTINANGI, Mahakama -Tabora

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Simon Chacha wamekabidhi jumla ya Kompyuta Mpakato nane (8) kwa Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kusaidia usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (Virtual Court).

Zoezi la makabidhiano ya vifaa hivyo vilivyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa lilifanyika jana tarehe 20 Oktoba, 2025 na vilikabidhiwa kwa Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Tabora, ACP Mussa Mkisi katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Gereza Kuu Uyui mkoani Tabora.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mhe. Dkt. Mambi alisema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za kushirikiana na wadau wa Mahakama ya Tanzania kuhakikisha kuwa haki inatolewa kwa haraka, uwazi na ufanisi zaidi kupitia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Tunataka kuhakikisha kwamba hata wale walio katika Magereza wanapata haki mapema ipasavyo kupitia mifumo ya kisasa ya mtandao, hii ni sehemu ya mageuzi ya kimfumo yanayolenga kuondoa ucheleweshaji wa mashauri na kupunguza gharama zisizo za lazima,” alisema Jaji Mfawidhi huyo.

Aidha, Mhe. Dkt. Mambi alisema kuwa, Kompyuta hizo zitasaidia Majaji na Mahakimu wengi kuendesha mashauri kwa njia ya mtandao kwa wakati mmoja na vilevile Mahabusu na Washtakiwa watapata fursa ya mashauri yao kusikilizwa kwa haraka na kwa wakati mmoja bila kusubiriana.

"Magereza zote za Mkoa wa Tabora zitakuwa na Kompyuta mpakato na TV za kutosha, hii itasaidia kuipunguzia gharama Serikali kusafirisha Mahabusu na Wafungwa kwenda mahakamani ukizingatia jiografia ya Tabora ambao ni Mkoa mkubwa kuliko yote Tanzania," alieleza Jaji Mfawidhi.

Aidha, Mhe. Dkt. Mambi alisema upatikanaji wa vifaa hivyo, vitaimarisha usalama kwa Askari ambao wanalazimika kusafirisha wafungwa kutoka Magereza ambazo ziko mbali hadi Mahakamani. Kwa upande wa Mahakama itaongeza idadi ya mashauri yanayoondeshwa kwa njia ya mtandao ambapo kati ya mwezi Septemba, 2024 mwaka hadi mwaka huu Mahakama Kanda ya Tabora imeendesha jumla ya mashauri 421 kwa njia ya mtandao.

Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Jaji Mkuu kuhusu utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 ambayo imeweka msisitizo juu ya matumizi ya TEHAMA na Akili Unde katika kurahisisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.

Mhe. Dkt. Mambi ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu ya Mkoa kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA katika kurahisisha upatikanaji wa haki. Aidha ameishukuru pia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuleta TV Sreen' katika Gereza la Uyui Tabora 

Vilevile, Jaji Mfawidhi huyo ameushukuru Uongozi wa Mahakama kwa kuleta Makasha kwenye Magereza yenye vyumba vya kuendeshea mashauri kwa njia ya mtandao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Simon Chacha, aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano na ubunifu huo, akiahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha mazingira ya utoaji haki na ustawi wa Wafungwa, Mahabusu na Sekta ya Sheria kwa ujumla wake.

“Serikali ya Mkoa wa Tabora itaendelea kushirikiana na Mahakama, Jeshi la Magereza na wadau wengine kuboresha huduma kwa wafungwa na mahabusu hasa kwa kutumia mifumo ya TEHAMATulipokuwa ndani tuliambiwa kuhusu changamoto ya malazi nasi kama sehemu ya mchango wetu, tumeamua kutoa magodoro 168 ili kuboresha mazingira ya malazi katika Gereza hili,” alisema Mhe. Chacha.

Naye Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Tabora, ACP Mussa Mkisi akizungumza kwa niaba ya Jeshi la Magereza, alishukuru kwa msaada huo na kusema kuwa utarahisisha mawasiliano na usikilizaji wa mashauri bila kulazimika kuwasafirisha Mahabusu mara kwa mara.

“Hii itasaidia kupunguza gharama, kuongeza usalama wa Mahabusu na Wafungwa na kuharakisha mwenendo wa mashauri. Tunashukuru sana kwa uongozi wa Mahakama na Mkoa kwa kuona changamoto zetu na kuzitatua,” alisema ACP Mkisi.

Katika tukio lingine lililofanyika siku hiyo hiyo, Timu ya Uongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wa Mahakama ikiongozwa na Mhe. Simon Chacha ilitembelea Kontena maalum lenye vifaa vya kisasa vinavyotumika katika usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao ili kujionea namna mfumo huo unavyofanya kazi.

Aidha walimshukuru Jaji Mfawidhi kwa jitihada kubwa anazozifanya za kuwaunganisha wadau ili kuhakikisha kuwa wanashirikiana katika kuboresha huduma za utoaji wa huduma ya haki kwa wananchi.

“Ni jambo la kujivunia kuona teknolojia kama hii ikitumika hapa Tabora. Hii ni hatua kubwa katika mageuzi ya Sekta ya Sheria nchini,” aliongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora.


 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Adam Juma Mambi akikabidhi kompyuta mpakato kwa ACP Mussa Mkisi kwa ajili ya matumizi. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Simon Chacha pamoja na Maafisa wengine wa Magereza wakishuhudia zoezi hilo.

Jaji Mfawidhi wa Mahahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe.Dkt. Adam Mambi (wa pili kushoto) akimpokea na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Simon Chacha (kushoto) kabla kuanza hafla ya makabidhiano ya Kompyuta Mpakato katika Gereza Kuu la Uyui.

Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Tabora, ACP Mussa Mkisi akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Jeshi la Magereza.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Chacha (wa kwanza kushoto) akikagua Kontena/kasha maalumu lenye vifaa vya kusikilizia mashauri kwa njia ya mtandao. Wengine katika picha wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi anayefuata ni Mkuu wa Wilaya Tabora, Mhe. Upendo Wella na Viongozi wa Mahakama na Magereza.


Muonekano ndani ya Kasha/Kontena lililopo katika Gereza Kuu la Uyui ambapo Mkuu wa Mkoa wa Tabora alitembelea na kujionea jinsi Mahakama mtandao inavyofanya kazi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Adam Mambi (wa tatu kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora (wa nne kushoto), Mhe. Simon Chacha na sehemu ya Viongozi wa Magereza Tabora na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni