- Mfumo wa digitali kuongeza ufanisi na uwazi katika shughuli za Mahakama
- Mahakimu wapya watakiwa kutumia Tehama kama nyenzo ya utoaji
haki kwa haraka
Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dodoma
Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George
Hillary Herbert, amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) yameleta mapinduzi makubwa katika utendaji kazi wa Mahakama nchini,
hatua iliyoongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa muhimili huo.
Akizungumza wakati wa kufunga Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu
Wakazi Wapya 89 yaliyofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 7 hadi 17 Oktoba
2025, Mhe. Herbert alisema Mahakama imepiga hatua kubwa kupitia utekelezaji wa
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2020/2021 – 2024/2025) kwa kuimarisha mifumo ya
TEHAMA inayowezesha utoaji haki kwa haraka na kwa uwazi.
Mhe. Herbert, ambaye ni Msajili wa Mahakama ya Rufani
Tanzania, alisema kuwa matumizi ya TEHAMA yameifanya Mahakama ya Tanzania
kutambulika kimataifa kutokana na ubunifu na ufanisi wake katika mifumo ya
kidijitali, ikiwemo uendeshaji wa mashauri kwa njia ya kielektroniki.
Pamoja na hayo, alisema, “Matumizi ya kiwango cha juu ya
TEHAMA katika Mahakama ya Tanzania yameongeza sana ufanisi wa utendaji kazi wa Mhimili
huu na hivyo imani ya wananchi kwa Mahakama imeongezeka sana. Ili kuendeleza na
kuimarisha ufanisi huu, ni rai yangu kwenu kwamba kila mmoja wenu ajitayarishe
kuendesha shughuli zake za kila siku kama Hakimu kwa kutumia TEHAMA kama nyenzo
muhimu ya kuwezesha utoaji haki kwa wote mapema ipasavyo.”
Aidha, aliwataka Mahakimu Wakazi wapya kuhakikisha wanatumia
kikamilifu teknolojia hiyo katika kazi zao za kila siku, kama njia ya
kuimarisha utoaji haki kwa wote na kuongeza uaminifu wa wananchi kwa Mahakama
ya Tanzania.
Mafunzo hayo Elekezi yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania
kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), ili kuwaandaa
Mahakimu Wakazi Wapya kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kutumia
TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.
Akizungumzia kuhusu uhuru wa Mahakama, Mhe. Herbert alisema ni
msingi muhimu wa kikatiba unaolenga kuwa na Mahakama huru isiyoingiliwa na
mihimili mingine.
Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) inasema kuwa katika
kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika
kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.
‘Uhuru huo haujawekwa kwa Mahakama kama Mhimili pekee, bali
unaenda hadi kwa Hakimu au Jaji mmoja mmoja wakati anatekeleza majukumu ya
utoaji haki. Uhuru huu ni muhimu sana, lakini siyo kibali cha kufanya uamuzi
bila kufuata Katiba ya nchi, Sheria, kanuni na taratibu zilizopo…
‘Badala yake uhuru huu unawapa nafasi ya kutenda haki bila
kuingiliwa au bila ushawishi kutoka nje, mambo ambayo kwa namna moja au
nyingine huathiri utendekaji wa haki,’ alisema.
Mhe. Herbert alibainisha pia kuwa uhuru huo haumaanishi
kujitenga kabisa na watendaji au Viongozi wengine wa kiserikali, watumishi
wenzao au wadau wa Mahakama, la hasha!!
Alisema wao kama Mahakimu na Viongozi wa umma wanao wajibu
wa kushirikiana na Viongozi wengine, watumishi wenzeo na wadau wa Mahakama
katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na katika masuala yote
yatakayoboresha huduma za utoaji haki, bila kusahau kuzingatia miiko na mipaka
ya kazi yenu.
Mhe. Herbert aliwaambia Mahakimu hao kuwa ushirikiano huo
utafanya utekelezaji wa majukumu yao uwe mwepesi lakini pia utazidi kuimarisha
imani ya wananchi kwa Mahakama na kwa mfumo mzima wa sheria hapa nchini.
Aidha, Msajili wa Mahakama ya Rufani aliwakumbusha kuwa na
bidii ya kujielimisha zaidi na kuhuisha maarifa yao ya kitaaluma mara kwa mara
kwa kufuatilia mabadiliko ya sheria, maamuzi yanayotolewa na Mahakama za juu na
kwa kusoma vitabu na maandiko mbalimbali yanayohusu sheria na maarifa ya jumla.
Alieleza kuwa tabia hiyo itawawezesha kuendana na mabadiliko
yote yanayotokea katika sheria, lakini pia katika jamii wanayoishi kwani sheria
na Mahakama vipo kwa ajili ya kuongoza maisha ya wanajamii.
‘Mahakama isiyozingatia mabadiliko ya kisheria na kijamii
haitaheshimika wala kuaminika na jamii husika kwa kuwa itakuwa imepitwa na
wakati,’ alisema.
Alimnukuu Jaji wa Uingereza, Lord Denning ambaye alisema, “A
judge must not alter the law, he must apply it, but in doing so, he must remain
up to date with the society he serves.”
Kwa hiyo, Mhe. Herbert aliwasisitiza Mahakimu hao kuwa ni
muhimu kuendelea kujifunza ili kujiongezea ujuzi na hivyo kuepuka makosa
yanayoepukika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni