Jumatatu, 20 Oktoba 2025

TEHAMA YAONGEZA UFANISI UTOAJI HAKI MAHAKAMANI

  • Mfumo wa digitali kuongeza ufanisi na uwazi katika shughuli za Mahakama
  • Mahakimu wapya watakiwa kutumia Tehama kama nyenzo ya utoaji haki kwa haraka

Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dodoma

Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Hillary Herbert, amesema matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameleta mapinduzi makubwa katika utendaji kazi wa Mahakama nchini, hatua iliyoongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa muhimili huo.

Akizungumza wakati wa kufunga Mafunzo Elekezi kwa Mahakimu Wakazi Wapya 89 yaliyofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 7 hadi 17 Oktoba 2025, Mhe. Herbert alisema Mahakama imepiga hatua kubwa kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2020/2021 – 2024/2025) kwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA inayowezesha utoaji haki kwa haraka na kwa uwazi.

Mhe. Herbert, ambaye ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema kuwa matumizi ya TEHAMA yameifanya Mahakama ya Tanzania kutambulika kimataifa kutokana na ubunifu na ufanisi wake katika mifumo ya kidijitali, ikiwemo uendeshaji wa mashauri kwa njia ya kielektroniki.

Pamoja na hayo, alisema, “Matumizi ya kiwango cha juu ya TEHAMA katika Mahakama ya Tanzania yameongeza sana ufanisi wa utendaji kazi wa Mhimili huu na hivyo imani ya wananchi kwa Mahakama imeongezeka sana. Ili kuendeleza na kuimarisha ufanisi huu, ni rai yangu kwenu kwamba kila mmoja wenu ajitayarishe kuendesha shughuli zake za kila siku kama Hakimu kwa kutumia TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kuwezesha utoaji haki kwa wote mapema ipasavyo.”

Aidha, aliwataka Mahakimu Wakazi wapya kuhakikisha wanatumia kikamilifu teknolojia hiyo katika kazi zao za kila siku, kama njia ya kuimarisha utoaji haki kwa wote na kuongeza uaminifu wa wananchi kwa Mahakama ya Tanzania.

Mafunzo hayo Elekezi yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), ili kuwaandaa Mahakimu Wakazi Wapya kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kutumia TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.

Akizungumzia kuhusu uhuru wa Mahakama, Mhe. Herbert alisema ni msingi muhimu wa kikatiba unaolenga kuwa na Mahakama huru isiyoingiliwa na mihimili mingine.

Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) inasema kuwa katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.

‘Uhuru huo haujawekwa kwa Mahakama kama Mhimili pekee, bali unaenda hadi kwa Hakimu au Jaji mmoja mmoja wakati anatekeleza majukumu ya utoaji haki. Uhuru huu ni muhimu sana, lakini siyo kibali cha kufanya uamuzi bila kufuata Katiba ya nchi, Sheria, kanuni na taratibu zilizopo…

‘Badala yake uhuru huu unawapa nafasi ya kutenda haki bila kuingiliwa au bila ushawishi kutoka nje, mambo ambayo kwa namna moja au nyingine huathiri utendekaji wa haki,’ alisema.

Mhe. Herbert alibainisha pia kuwa uhuru huo haumaanishi kujitenga kabisa na watendaji au Viongozi wengine wa kiserikali, watumishi wenzao au wadau wa Mahakama, la hasha!!

Alisema wao kama Mahakimu na Viongozi wa umma wanao wajibu wa kushirikiana na Viongozi wengine, watumishi wenzeo na wadau wa Mahakama katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na katika masuala yote yatakayoboresha huduma za utoaji haki, bila kusahau kuzingatia miiko na mipaka ya kazi yenu.

Mhe. Herbert aliwaambia Mahakimu hao kuwa ushirikiano huo utafanya utekelezaji wa majukumu yao uwe mwepesi lakini pia utazidi kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama na kwa mfumo mzima wa sheria hapa nchini.

Aidha, Msajili wa Mahakama ya Rufani aliwakumbusha kuwa na bidii ya kujielimisha zaidi na kuhuisha maarifa yao ya kitaaluma mara kwa mara kwa kufuatilia mabadiliko ya sheria, maamuzi yanayotolewa na Mahakama za juu na kwa kusoma vitabu na maandiko mbalimbali yanayohusu sheria na maarifa ya jumla.

Alieleza kuwa tabia hiyo itawawezesha kuendana na mabadiliko yote yanayotokea katika sheria, lakini pia katika jamii wanayoishi kwani sheria na Mahakama vipo kwa ajili ya kuongoza maisha ya wanajamii.

‘Mahakama isiyozingatia mabadiliko ya kisheria na kijamii haitaheshimika wala kuaminika na jamii husika kwa kuwa itakuwa imepitwa na wakati,’ alisema.

Alimnukuu Jaji wa Uingereza, Lord Denning ambaye alisema, “A judge must not alter the law, he must apply it, but in doing so, he must remain up to date with the society he serves.”

Kwa hiyo, Mhe. Herbert aliwasisitiza Mahakimu hao kuwa ni muhimu kuendelea kujifunza ili kujiongezea ujuzi na hivyo kuepuka makosa yanayoepukika.


Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert.

Meza Kuu inayoongozwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert [katikati]. Picha chini ni Viongozi wengine wa Mahakama wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri.

 Washiriki wa mafunzo wakifuatilia hotuba ya kuhitimishwa mafunzo hayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni