Na DHILLON UISSO, Mahakama- Dar es Salaam
Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Temeke na Mahakama za Mwanzo katika Wilaya hiyo wamepatiwa mafunzo yaliyolenga kuwajengea uwezo na kukumbushana masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwa mteja, kuondoa msongo wa mawazo, mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa Mashauri (e-CMS) na elimu kuhusu Mifuko ya Jamii na Uwekezaji.
Mafunzo hayo ambayo yalifanyika wiki iliyopita kwenye Ukumbi wa Mahakama uliopo kwenye Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke na kuhudhuriwa na Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo pamoja na watumishi wa Mahakama hizo.
Akifungua mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo, Mhe. David Ngunyale aliwataka Mahakimu pamoja na watumishi wote wa Mahakama ya Wilaya Temeke na Mahakama zake za Mwanzo kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia Maadili na weledi.
Mhe. Ngunyale alisema dhana ya utoaji haki kwa wakati inakuwa halisi watumishi wanapofanya kazi yao kwa maadili na wa weledi.
Aidha, Jaji Ngunyele alitoa mada kuhusu afya ya akili, akifundisha viashiria vya mtu mwenye shida ya afya ya akili alitaja kuwa ni pamoja na kukosa furaha , kujitenga, kuwa na hasira, usahaulifu, kupoteza ari ya kufanya kazi na kadhalika.
Alielezea pia kuhusu mbinu za kurudi kwenye mstari
ikiwemo kujichanganya na watu ‘socialization’,
kula milo kamili (balanced diet), kupata muda wa kupumzika kuwa na ratiba za
kubadilisha mazingira hasa wakati wa likizo na kutoa kipaumbele kwa familia.
Kadhalika, Mhe. Ngunyale aliwataka watumishi hao
kujikita katika mbinu hizo ili kutoharibu majukumu yako ya utoaji haki.
Naye Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bw. Tumaini Malima aliwasilisha mada kuhusu matumizi sahihi ya Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ambapo alisisitiza kuwa hakuna njia nyingine ya kukwepa matumizi ya TEHAMA isipokuwa kufungamana nayo ili kuboresha utendaji kazi kwa mtu mmoja mmoja na Taasisi nzima kwa ujumla.
Mada alizowasilisha ni pamoja na matumzi sahihi ya barua pepe (email), changamoto na utatuzi wa kushughulika na mashauri ya Mahakama ya Mwanzo kwa kutumia Programu Tumishi pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri na jinsi ya kuandaa taarifa mbalimbali kupitia mifumo.
Kadhalika Wataalamu kutoka Mfuko wa Uwekezaji (UTT) na Mifuko ya Hifadhiy a Jamii (PSSSF) walipata wasaa wa kuwapitisha watumishi hao kwenye mifumo ya Mifuko hiyo ili kujua namna bora ya uwekezaji na kuangalia michango ya mwanachama kupitia mifumo ili kujua kila mwezi michango kama inawasilishwa ipasavyo.
Mafunzo hayo yalifungwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. Vicky Mwaikambo na kuwasisitiza watumishi
kubadilika na kufanya kazi kwa weledi ili kuleta matokeo chanya katika utoaji
haki mapema ipasavyo.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mafunzo, Mhe. David Ngunyale akitoa mada wiki iliyopita wakati wa Mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Temeke.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni