Na DOTTO NKAJA–Mahakama, Geita
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Geita, Mhe. Kevin Mhina, tarehe 17 Oktoba, 2025 alizindua Jengo la Mahakama ya
Mwanzo Ng’anzo iliyopo Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita.
Akiwa katika zoezi hilo, Mhe. Mhin alitoa wito kwa
watumishi aliowapangia katika Mahakama hiyo kuhakikisha wanakuwa kimbilio la
wananchi wanaotafuta haki ili waweze kupata haki zao bila usumbufu wowote.
“Wananchi wana imani na Mahakama kama chombo cha
kupata haki zao, hivyo ni muhimu kwa watumishi kutekeleza majukumu yenu kwa
uadilifu na weledi ili kuendeleza imani hiyo,” alisema.
Aidha, Jaji Mfawidhi aliwasisitiza juu ya mambo
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ushirikiano na Taasisi za kiserikali na zisizo
za kiserikali pasipo kuathiri dhamira ya Mahakama ya Tanzania.
Aliongeza kuwa maadili ya watumishi yawe kioo kwa
wananchi kwani Mahakama ni sehemu tukufu na wajikite zaidi katika kusuruhisha
kesi za madai ili kuondoa kabisa migogoro katika Kata ya Ng’anzo.
Mhe. Mhina pia aliwahimiza watumishia hao kulitunza
jengo hilo la kisasa ambalo linanyezo zote za kitehama zenye kiwango cha juu Pamoja
miundombinu iliyosimikwa ndani yake.
Wakati wa ufunguzi huo, Mkuu wa Wilaya aliwakilishwa
na Katibu Tawala wa Wilaya, Bw. Ally Mketo, ambaye aliipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa kuwasogezea huduma za kimahakama karibu wa wananchi. Aliwaomba
wananchi wa Ng’anzo kuitumia Mahakama hiyo ili kutatua migogoro yao.
Zoezi la ufunguzi wa Mahakama hiyo lilishuhudiwa na wananchi
wa Kata na Kijiji cha Ng’anzo na Viongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita,
wakiongozwa na Naibu Msajili, Mhe. Fredrick Lukuna na Mtendaji wa Mahakama Bi.
Masalu Kisasila.
Wengine ni Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Geita, Mhe. Cleofas Waane, Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya zilizopo
katika Kanda ya Geita, wadau kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Geita na
watumishi wote wa Mahakama hiyo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina akifungua Jiwe la Msingi la Jengo la Mahakama ya Mwanzo Ng’anzo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina akipanda mti wa kumbukumbu katika Mahakama ya Mwanzo Ng’anzo.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Fredrick Lukuna [kulia] akipanda mti wa kumbukumbu katika Mahakama ya Mwanzo Ng’anzo.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Bi. Masalu Kisasila akipanda mti katika uwanja wa Mahakama ya Mwanzo Ng’anzo.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina [katikati waliokaa] akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu, watumishi wa Mahakama na Wadau kwenye siku ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Ng’anzo iliyopo Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ng’anzo siku ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Ng’anzo.
Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni