Jumatatu, 20 Oktoba 2025

WADAU WA HAKI JINAI WAJIPONGEZA BAADA YA TATHMINI

Na EUNICE LUGIANA, Mahakama-Kibaha

Wadau wa Haki Jinai Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani wamejipongeza baada ya kutathmini na kubaini kuwepo kwa upungufu wa mahabusu na Watoto katika Gereza la Mahabusu Mkuza Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.

Pongezi hizo zilitolewa na wadau hao tarehe 17 Oktoba 2025 katika Kikao cha Kusukuma Mashauri cha Mahakama ya Wilaya Kibaha kilichofanyika kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama hiyo.

Akitoa pongezi hizo Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Matilda Zakaria alisema wiki moja iliyopita Wadau wa Haki Jinai walitembelea Gereza la Mahabusu Mkuza ambapo walikuta Mahabusu wakiwa wachache na hakuna Watoto au Mahabusu wala wafungwa waliodhaniwa kuwa ni Watoto, hivyo kutoa viashiria kwamba Mahakama pamoja na wadau wote wa Haki Jinai wamefanya kazi yao vizuri na kwa umakini.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai aliwataka baadhi ya Mawakili wa Kujitegemea kuweka shajara zao vizuri ili kuepuka kuahirisha mashauri kutokana na shajara zao kujaa mashauri ya Mahakama nyingine.

Aliwaomba pia Polisi wanapoandaa hati za mashtaka kuzingatia makosa ili wasipeleke mashauri Mahakama za Mwanzo ambazo  mamlaka yake ni Mahakama ya Wilaya.

Aliwataka Polisi waweke usawa katika kupeleka mashauri ya jinai Mahakama za Mwanzo kwakuwa Mahakama hizo ziko mbili mjini hivyo wasipeleke Mahakama moja tu.

Sambamba na kikao hicho, kulikuwa pia na Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Madai ambapo hakukuwa na mashauri ya mlundikano lakini yapo yanayokaribia kufikia mlundikano hivyo, Mawakili wametakiwa kupunguza mapingamizi ya kiufundi ili kuepuka mlundikano wa mashauri.

Wakati huo huo Afisa Adhabu Mbadala, Bw. Deogratius Njuu aliwapongeza Mahakimu wa Mkoa wa Pwani maana umekuwa Mkoa wa tatu Tanzania kwa kutumia adhabu mbadala ambayo inaokoa pesa nyingi kwa Serikali. Ikiwa ni pamoja na kupunguza pesa za chakula wawapo gerezani na mahitaji muhimu lakini pia kifungo cha nje kinasaidia taasisi za Serikali kuajiri vibarua kufanya usafi katika Ofisi za Umma na katika maeneo ya wazi na ya jumuiya kama stendi na masokoni.

Kikao hicho cha robo ya tatu ya mwaka kilihudhuriwa na Wadau wa Haki Jinai pamoja na Wadau wa Haki Madai.


Wajumbe wa Kikao cha Kusukluma Mashauri cha Mahakama ya Wilaya Kibaha  wakiwa katika kikao hicho kilichofanyika tarehe 17 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha ambaye ni Mwenyekiti  wa Kikao cha Kusukuma Mashauri ya Jinai, Mhe. Emmael Lukumai (kushoto) akiwa kwenye Kikao cha Kusukuma Mashauri kilichofanyika tarehe 17 Oktoba, 2025 kwenye ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha. Kulia ni Katibu wa kikao hicho Wakili wa Serikali, Bi. Caroline Kigembe.
 
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao cha Kusumuma Mashauri ya Madai, Mhe. Emmael Lukumai (kushoto) akiwa na Katibu wa kikao hicho, Wakili wa Kujitegemea, Wakili Amos Sura ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Pwani.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni