Jumamosi, 18 Oktoba 2025

WATUMISHI WA MASJALA KUU WAFANYA ZIARA YA UTALII NGORONGORO

Na. Innocent Kansha – Mahakama, Ngorongoro

Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wamefanya ziara ya kutembelea Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali vya mbuga hiyo ikiwa ni mkakati wa kutanganza utalii wa nadani na kujifunza utunzaji wa mazingira na ekolojia ya mazingira, zira hiyo ya kitalii ilifanyika tarehe 17 na 18 Oktoba, 2025 katika bode hilo maarufu Dunia lenye wanyama Pori mbalimbali ikiwemo wale wanyama watano maarufu Duniani.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati wa maandalizi wa ziara hiyo wakati wa kuhitimisha ziara mratibu wa ziara hiyo Afisa Utumishi kutoka Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma Bi. Edith Kajuna amesema lengo la ziara hiyo ni kuitangaza Tanzania kwa Dunia kwamba kuna vivutio vizuri sana vya mbuga za wanyama na vivutio vingine kama Mlima Kilimanjaro ambao upo miongoni mwa maajabu saba ya Dunia.

“Si lazima tuwategemee wageni kutoka nje ndiyo waje kuvitangaza vivutio vyetu ni sisi wenye kuweza kuona kwamba tunamaeneo, tunavivutio vya kila aina na tuna maeneo ya utalii ambao tunaweza kuvitangaza sisi na kuufanya wenyewe hivyo kuvutia watu wengi kwa maana watalii wa ndani,” alisema Bi. Kajuna.

Akifafanua malengo ya ziara hiyo ya utalii wa ndani alisema ilikuwa kutoa elimu kwa jamii hasa kuhusu masuala ya kisheria na kuutangazia umma kwamba sasa Makao Makuu ya Mahakama yapo Dodoma, kwa kutoa machapisho mbalimbali ya kimahakama yanayo onesha kuwa sasa mahitaji yote ya kisheria yanapatikana Makao Makuu ya Mahakama Dodoma.

“Watumishi wote kama wanavyofahamu mdhamina wa ziara hii ya utalii katika bonde la Ngorongoro ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani na Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Bw. Leonard Magacha waliowezesha kwa namna moja au nyingine kufanikisha safari hii hivyo timu zima ya watumishi inatoa kongole za dhati,” aliongeza Bi Kajuna.

Aidha, Bi. Kajuna ameongeza kuwa, kupitia ziara hiyo wamejifunza mambo mengi sana walitarajia kuwaona wanyama watano wale maarufu Dunia lakini kupitia ziara hiyo walifanikiwa kuwaona wanyama nne ambao ni Simba, Faru, Twiga na Tembo na wengine wakiwemo kiboko, nyati, nyumbu, pundamilia, sungura, swala, kasongo, fisi,  na ndege mbalimbali kama bata, mbuni, cowbird na uoto wa asili wa kuvutia sana. Vitu hivyo vyote vinavutia sana kuweza kumvutia kila mtalii kuweza kuja kujionea vitu gana ambavyo vinapatikana ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.

“Tunatoa rai kwa Taasisi, Idara, Mashirika na watumishi wa umma na binafsi kuweza kujionea mambo mbalimbali ambayo yanapatikana kwenye Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro,” amesisitiza Bi. Kajuna.

Akitoa wito kwa wananchi Bi. Kajuna amesema wananchi wanapaswa kujitoa na kupenda nchi yao na kupenda kufanya utalii lakini pia kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake. Aidha alihimiza utunzaji wa mazingira kwasababu utunzaji wa mazingira unasaidia uoto wa asili kuendelea kuwepo na historia ya wanayama pamoja na mimea mingine yote kuendelea kuwepo.

“Tunapoharibu mazingira tunafanya uoto wote wa asili unapotea wanyama wote wanatoweka, kwa hiyo tuendelee kupambana kwa ajili ya kuiweka Tanzania iendelee kuwa ya kijana, iendelee kuvutia na kila mtu anayeingia kwenye hifadhi zetu aweze kutamani kurudi tena,” amesema Bi. Kajuna.

Kwa upande wake mratibu wa ziara hiyo ambaye ni Afisa Usafrishaji kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu Dodoma Bw. Richard Dotto William amesema kuwa, ziara ilikuwa na malengo mbalimbali ikiwemo kujifunza masuala ya utalii na kuunga juhudi za kukuza utalii wa ndani.

Vilevile ziara ililenga kuboresha afya ya akili na kupumzisha akili hasa kutokana na majukumu ya kila siku ya kiutumishi na kujifunza namna Taasisi zingine zinazofanya kazi na Mahakama ya Tanzania zinafanya kazi kwa ufanisi katika majukumu yao ya kulijenga taifa la Tanzania.

Akatoa rai kwa Taasisi nyingine ziweze kuona umuhimu wa kufanya utalii hasa utalii wa ndani pamoja na kutunza mazingira ili kufanya utalii uwe endelevu na kudumisha hifadhi pamoja na misitu ya Tanzania kwa ujumla.

“Nawashauri viongozi na Taasisi zingine ziwe na utaratibu huu walau wa mara moja kwa mwaka katika kuwapa watumishi wao ama kutoa nafasi kwa watumishi ambao watakuwa tayari kwa ajili ya kutemebelea vivutio na maeneo mbalimbali ya kitalii ili kujifunza, kufanya mambo yanayohusiana na utalii na utunzaji wa mazingira ili nchi ya Tanzania iimarike katika sekta ya utalii,” amesema Bw. William.

Naye Mwakilishi kutoka Kampuni ya Utalii ya Dodoma Safari Tour Bw. Billali Ally amesema, anamshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kutembelea hifadhi ya Bonde la Ngorongoro na kujifunza mambo mbalimbali kama inavyosomeka kwenye vitabu Ngorongoro ni sehemu yenye umashuhuri mkubwa sana Duniani.

“Lengo letu kubwa ilikuwa kuja kupata uzoefu wa maisha mengine ya wanyama jinsi wanavyoishi na kujifunza vitu mbalimbali vya ekolojia ya maisha ya wanyama na kufurahisha akili zetu kwa mwaka mzima tunakuwa na shughuli mbalimbali za kufanya kazi na vitu vingine, kunawakati inabidi tupumzishe akili ni miongoni mwa malengo yaliyosababisha tuje kutembelea hapa hifadhi ya Ngorongoro,” amesema Ally.

Aidha, ameongeza kuwa kusafiri na watumishi wa Muhimili wa Mahakama ni jambo moja lililowapa uzoefu mkubwa kampuni ya Dodoma Safari Tour ya kuunganisha umoja na Taasisi ya Mahakama katika kutekeleza majukumu yao ya kuendesha shughuli za kiutalii kwa kutambulisha hifadhi za Taifa na kuunganisha wadau wengi wa utalii ili kukuza utalii wa ndani nchini Tanzania.  

Moja ya Big Five akiwa amepumzika mara baada ya hekaheka zake za mawindo katika Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro 

Kundi la wanyama jamii ya nyumbu wakiwa malishoni katika Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro 
Kundi la wanyama jamii ya Pundamilia wakiwa malishoni katika Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro 
Sehemu ya ya msafara wa magari waliyotumia Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma kwa ajili safari ya kutembelea Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali vya mbuga hiyo
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja wakijiandaa kwa safari ya ziara ya kutembelea Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali vya mbuga hiyo.


Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja wakijiandaa kwa safari ya ziara ya kutembelea Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali vya mbuga hiyo

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wakiwa kwenye picha ya pamoja wakijiandaa kwa safari ya ziara ya kutembelea Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali vya mbuga hiyo


Sehemu ya ya msafara wa magari waliyotumia Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma kwa ajili safari ya kutembelea Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali vya mbuga hiyo
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wakiwa kwenye Lango Kuu la kuingia ndani ya Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma Bw. Leonard Magacha akisaini Kitabu cha wangeni cha Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro.





Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma wakiwa katika eneo la Boma la Wamasai walipotembelea Mbuga ya Hifadhi ya Ngorongoro kujionea vivutio mbalimbali.
 

     

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni