- Ahimiza uaminifu, uadilifu kazini, nidhamu ya kazi
- Asema kupata uhakimu siyo mwisho wa kujifunza
Na FAUSTINE KAPAMA-MAHAKAMA,
Dodoma
Msajili wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. George Herbert, amewataka Mahakimu Wakazi wapya 89
kuzingatia mambo tisa muhimu wanapoanza kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia
wananchi na Taifa kwa ujumla.
Mahakimu hao waliapishwa
na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, hivi karibuni na
baadaye kushiriki kwenye mafunzo ya siku tisa yaliyoanza kutolewa tarehe 7
Octoba, 2025 na kuhitimishwa tarehe 17 Octoba, 2025.
Mafunzo hayo yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania
jijini Dodoma, yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Akizungumza wakati
anahitimisha mafunzo hayo jana tarehe 17 Octoba, 2025, Mhe. Herbert aliwataka
Mahakimu hao kuzingatia umuhimu wa kazi yao, uadilifu na uaminifu, nidhamu ya
kazi na kuwa na uhusiano mwema kazini.
Mambo mengine waliyohimizwa
Mahakimu hao kuyazingatia ni kuendelea kujifunza kila siku, huduma wanazotoa, utunzaji
wa rasilimali, kuzingatia maadili na mwenendo mzuri na uwajibikaji.
Umuhimu wa kazi yako
Mhe. Herbert amewaeleza
Mahakimu hao kuwa kazi wanayoenda kuifanya ni kazi nyeti na wamepewa dhamana
kubwa. Hivyo, wanatakiwa kufanya kazi kwa moyo wa kujitoa, huku wakitambua kwamba
wana hudumia watu, Mhimili wa Mahakama na Taifa kwa ujumla.
Uadilifu na uaminifu
Msajili wa Mahakama ya
Rufani amesema kuwa kila mmoja wa Mahakimu hao aamini kwamba jina lake na
taaluma yake vitajengwa kwa uaminifu na uadilifu. Amewataka kujiepusha na vitendo
vya rushwa, upendeleo au matumizi mabaya ya mamlaka. Amewaeleza kuwa wanatakiwa
kujua kwamba uadilifu ndiyo nguzo ya mafanikio kwa Hakimu yoyote.
Nidhamu ya kazi
Mhe. Herbery amewaeleza
Maheshimiwa hao kuwa kama Mahakimu wanategemewa kuwa na nidhamu ya kazi,
kuheshimu ratiba za mashauri, kutengeneza malengo na kutekeleza maagizo na
misingi ya utendaji kazi. Ameeleza kuwa nidhamu ndiyo itakayowatofautisha wao
na watu wengine.
Uhusiano mwema kazini
Msajili wa Mahakama ya
Rufani amewahimiza Mahakimu hao kuheshimu wote wanaofanya kazi kuanzia mkubwa
mpaka yule wanayemuona ni mdogo. ‘Mkiheshimina kutakuwa na ushirikiano na
mahusiano mazuri kazini na mambo hayo yataleta matokeo chanya sehemu ya kazi,’
amesema.
Tuendelee kujifunza kila
siku
Mhe. Herbert amesema kuwa
kupata uhakimu siyo mwisho wa kujifunza, hivyo
amewahimiza kutambua kwamba kila siku wanapokuwepo kazini, fursa ya kuongeza
maarifa na uzoefu zipo na wanatakiwa wasiziache zikawapita.
Aidha, Kiongozi huo
mwandamizi wa Mahakama amewaeleza Mahakimu hao kuwa wanapokutana na lolote wasiache
kuuliza, wawe wasikivu na tayari kujifunza kwa wengine, hata wale ambao wanadhani
ni wadogo kwao, kwamba siyo Mahakimu.
Huduma tunazotoa
Msajili wa Mahakama ya
Rufani amewaeleza Mahakimu hao kujua kwamba wanayemhudumia ni mwananchi na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wahakikishe wanatoa huduma bora ya haki
mapema ipasavyo kwa kila mwananchi.
Utunzaji rasilimali
Mhe. Herbert ameeleza pia
kuwa katika ofisi zao kuna rasilimali mbalimbali, hivyo ni vizuri wakavitumia
vifaa hivyo vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa. Amesema kuwa hatua hiyo itawasaidia
kulinda na kuvitunza vifaa hivyo.
Tuzingatie maadili na
mwenendo mzuri
Msajili wa Mahakama ya
Rufani amewakumbusha Mahakimu hao kuwa maadili yao siyo pale wanapokuwa
mahakamani tu, bali hata nje ya ofisi zao.
Hivyo wanatakiwa kujua kwamba
Hakimu ni mtu ambaye anayeheshimika na anafuatiliwa kwa sababu anaonekana kuwa
mfano na taswira kwa wote waliopo katika jamii husika.
Uwajibikaji
‘Kila kazi unayopewa ni
jukumu la kutekeleza kwa ufanisi na hivyo unapaswa kuwajibika ipasavyo,’ Mhe.
Herbert amewambia Mahakimu hao.
Katika hili, amewakumbusha
kwamba kuna Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050. Mhe. Herbert amewaasa kila
mmoja wao aisome Dira ile, aielewe na aone inamtakaje yeye kama Hakimu kuwa
mwajibikaji.
Katika hafla ya
kuhitimisha mafunzo hayo, washiriki wote walipatiwa vyeti pamoja na vitendea
kazi, ikiwemo kompyuta mpakato, yaani laptops, huku wengine wakikabidhiwa
zawadi mbalimbali kwa ushiriki bora walioutoa wakati wa mafunzo hayo.
Viongozi wengine
walioshiriki kwenye hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo ni Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu
wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick na Mkurugenzi wa Mafunzo wa Chuo
cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Patricia Kisinda.
Wengine ni Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Emmanuel Mrangu na Naibu Mkurugenzi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngunguru.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo akipokea kompyuta mpakato kama kitendea kazi ktuka Meza Kuu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni