Ijumaa, 5 Desemba 2025

JAJI MKUU, MHE. GEORGE MASAJU AWAASA MAWAKILI WAPYA KUDUMISHA UADILIFU, UTAWALA WA SHERIA

  • Awaelekeza Mawakili 774 waliopokelewa na kukubaliwa kuhakikisha haki inatendeka kwa wananchi kwa kuzingatia Katiba, Sheria na maadili ya kitaaluma 
  • Awasisitiza kuwa mstari wa mbele kulinda haki, kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu
  • Awataka kudumisha utawala wa sheria na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani

Na MARY GWERA & HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju amewaasa Mawakili wapya kuwiwa kuona haki ikitendeka, huku wao wakiwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanatenda haki kwa wananchi, kuzingatia uadilifu na wakijikita katika sehemu kuu mbili za uadilifu ambazo ni kuzingatia Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria zinazoongoza utumishi na maadili ya mawakili, sambamba na mila na desturi za Tanzania, kudumisha Utawala wa Sheria na kutokuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.

Mhe. Masaju ametoa wito huo leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye Sherehe za Kuwapokea na Kuwakubali Mawakili wapya 774 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

“Sasa mimi nichukue nafasi hii kuwaasa kwamba mtataka na kuendelea kuwa watu wenye akili nzuri, kama Mawakili, moja mtapaswa kuwa ‘sensitive to justice’ muwiwe kuona haki inatendeka  na ninyi wenyewe mtende haki, la pili mnapaswa kuwa waadilifu, uadilifu uko kwa maana mbili, moja kuzingatia Katiba na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zikiwemo na zile Sheria zinazoongoza utumishi wenu wa uwakili  na ni sheria ya mawakili na sheria ya maadili zinazotungwa na hiyo sheria lakini kuzingatia maadili na mila za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Masaju amewataka Mawakili hao kuwa na uwezo wa kumudu kutekeleza majukumu yao ya kazi ipasavyo, huku wakijiendeleza kielimu jambo ambalo litaongeza utendaji wao na maarifa zaidi katika utendaji.  “Tatu mtapaswa kuwa watu mnaomudu majukumu yenu kwa jinsi ipasavyo, viongozi hawa wamewaasa ni namna gani mnaweza kumudu majukumu yenu na kujiendeleza kimasomo sio mnaridhika tu na kukaa katika viwango mlivyonavyo, mtapaswa kusoma na hata yanayotokea nje ya mipaka ya Taifa hili, mjue nini kinakufanya wewe kuwa Wakili.”

Akiendelea kuzungumza kuhusu uwezo wa kumudu kutekeleza majukumu, Mhe. Masaju ameeleza kuwa kitu kinachomtambulisha Mwanasheria ni uwezo wa kutafsiri sheria na kutoa tafsiri hizo kwa watu wengine wanaofahamu na wale wasioifahamu Sheria, kwa Mahakama au wateja.

“Kitu kingine unachokuja kukigundua katika nini kinachokufanya kuwa Mwanasheria ni uwezo wako wa kutafsiri sheria hizo lakini na kuzitoa hizi tafsiri ulizozitoa kwa watu wengine wasiojua sheria au wanaojua sheria, iwe ni mahakamani iwe ni kwa mteja wako, na ndio maana kuna somo linaitwa communication skills, na pale utaona kwamba hata alama ya kushagaa ina maana kubwa, muundo mbovu katika sentensi unaathiri maana iliyokusudiwa, kwa hiyo sio lazima usome ‘International Law’, ndio ujifunze mambo mengine yanayotokea duniani, suala la umahiri ni la muhimu sana,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amewataka pia Mawakili hao kuendelea kuzingatia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kujenga mahusiano mazuri ili kutetea maslahi ya taifa, pamoja na kushirikiana katika majadiliano ya mikataba kwa kuzingatia utayari wa Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Kwa majukumu haya ambayo mnayo, na nimeona moyo wa utayari wa Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendelea kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na ikizingatiwa pia kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndio Mwanasheria namba moja, hivyo endeleeni kuzingatia fursa hizi mnazopewa na Serikali kujenga mahusiano mazuri na Serikali katika kutetea maslahi ya  Taifa hili ikiwa  ni pamoja na kwenye majadiliano ya mikataba, kama alivyokuwa anasema Rais Magufuli, sisi huku serikalini hatuwezi kujifanya tuna akili kuliko wote, kuna mashughuli ya mikataba tuna kazi nyingi za kufanya,” ameeleza Jaji Mkuu.

Aidha, Mhe. Masaju amewaeleza Mawakili hao kuwa, wanapaswa kufanya kazi bila kupuuza maslahi ya wanyonge, kuwanyanyasa au kuchukua rushwa ili kupoteza haki zao halikadhalika kutambua umuhimu wa uzalendo kwa taifa na kwamba mtu atakaye mpuuza, kumnyanyasa au kuchukua rushwa ili kuipindisha haki ya mtu mnyonge basi mtu huyo ataadhibiwa na Mungu.

“Mtu atakayempuuza mnyonge na kumnyanyasa akachukua rushwa ili kuhatarisha haki na maslahi ya mteja wake mnyonge huyo Mungu atamuadhibu, hawezi kufanikiwa, na Wakili miongoni mwenu ambaye hatambui  umuhimu wa uzalendo kwa Taifa hili ni kama hayupo, kwa sababu fursa yako ya kufanya 'legal practice' ni katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio kwingineko, na fursa hizo ziko za kutosha, miongoni mwenu pia huwa wanateuliwa Majaji na miongoni mwenu huwa wanateuliwa watu wengine kushika nyazfa mbalimbali katika utumishi wa umma," amesema.

“Mungu ni Mwanasheria na yeye ni wa utawala wa sheria na utawala wake unaongozwa na Katiba, na Katiba ile ina Ibara mbili kumpenda Mungu na kumfanya kuwa wa kwanza katika maisha yako yote, lakini na kumpenda jirani yako kama nafsi yako, lakini hiyo katiba yenye Ibara mbili ina zile Amri kumi, kwa hiyo ukisoma kile kitabu cha Kutoka sura ya 20 utapata zile Amri kumi, na Kutoka sura ya 21 mpaka  23 pale kuna zile sheria ndogo zinazotafsiri zile amri nyingine.na ukizifuata hizo na kuziishi utafanikiwa katika maisha yako, Mhe. Mwabukusi amesisitiza sana kuhusu hii ya kuwajali maskini na wanyonge muwe na huruma hapo mtakuwa mnatekeleza ile amri kumpenda jirani yako kama nafsi yako, katika ibara ya pili katika ile Katiba ya Mungu ambayo ni upendo,” amesisitiza Jaji Mkuu.

Katika upande mwingine, Mhe. Masaju ametoa ushauri kwa Shule ya Sheria ya Tanzania kuanzisha programu mbalimbali za vitendo ambazo zitatumika kuwapima Wanasheria kuliko zile za nadharia, ili kutoa fursa kwa vijana wanaohitimu kutoa huduma ya kisheria kwa jamii.

“Na kwa kuzingatia umuhimu wa ujuzi wa vitendo katika taaluma ya sheria, napenda kutoa ushauri kwa Shule ya Sheria ya Tanzania kuanzisha programu mbalimbali za mafunzo ya vitendo kwenye nadharia unakamata watu wengi lakini sio kwenye vitendo, sisi Serikalini tunachukua hatua tunataka kila mhitimu wa Shahada ya Sheria apate uwezo wa kusoma hicho chuo kusudi ije imsaidie na yeye ama kujiajiri au kuajiriwa,” ameeleza Mhe. Masaju. 

Ameongeza kuwa, suala la wanafunzi wanaosoma katika Shule ya Sheria ya Tanzania kupata mikopo linafanyiwa kazi na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ili kutoa fursa kwa vijana kusoma Shule ya Sheria ya Tanzania. 

“Nilivyokuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali niliweka kwenye muswada kwamba Wanasheria wanaoenda kusoma Diploma ya Sheria pale Shule ya Sheria ya Tanzania  nao waweze kupata mkopo, hawa watu watafanyaje, wao wanaenda kusoma Vyuo Vikuu kwa mikopo na ili waweze kufanya kazi wanapaswa wawe  wamesoma Shule ya Sheria ya Tanzania, mikopo hawana sasa wataendaje kusoma, kwa hiyo tumeshachukua hatua ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria hili tatizo litapatiwa utatuzi siku hizi za karibuni, Serikali lazima itoe mkopo kwa kila mwanafunzi ili aweze kupata nafasi ya kusoma Shule ya Sheria ya Tanzania,” Mhe. Masaju ameeleza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewataka Mawakili Wapya wa Kujitegemea kutawanyika katika maeneo mbalimbali nchini ili kufikisha huduma zao za utetezi wa haki kwa wananchi wengi zaidi.

“Kwa sasa kama mnavyofahamu kwenye Mahakama za Mwanzo, makosa yote yanadhaminika maana yake ni kwamba kama milango ya dhamana itafunguka kuna uwezekano mkubwa sana Mahakama ya Mwanzo kuongezewa majukumu ambapo sasa ninyi mtakuwa mnaenda kufanya kazi huko kwa sababu soko lipo, hii habari ya kwenda kukaa Dar es Salaam, Dodoma na Miji mingine Mhe. Mwabukusi amewatajia maeneo mengine ambapo fursa zipo nyingi, kwahiyo niwaombe sana jiandaeni,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema mnamo tarehe 05 Aprili, 2025, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuja kuzindua Jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania aliridhia Sera ya Mahakama ya kuwa na Mahakama ya Mwanzo kila Kata maana yake zitajenga Mahakama za Mwanzo. 

Jaji Mkuu amewaeleza Mawakili hao kutawanyika kwani kwa sasa Mawakili wa Kujitegemea na Mawakili wa Serikali wanaruhusiwa kwenda kwenye Mahakama za Mwanzo kama Hakimu ni Hakimu Mkazi yaani Hakimu ambaye ana Shahada ya Sheria. Mhe. Masaju amesisitiza, “ninawahakikishia kuwa nafasi ya kipaumbele cha kwanza katika msingi mkuu wa Dira ni Utawala Bora na Haki na hivi vitu huwa vinaenda pamoja. Tunataka Wanasheria wanaohitimu wapate soko wasiwe na sababu ya kuilalamikia Serikali.”

Mhe. Masaju amesema kuwa, hadi kufikia mwaka 2026 kuna Sheria ya Dhamana (The Bail Act) itatungwa ambayo inaweka taratibu za kina na sababu za kutoa dhamana au kuzinyima. Ameeleza kwamba, kabla mwaka 2026 haujaisha sheria hiyo itakuwa tayari na ikitokea ni hivyo na umewekwa utaratibu kwa makosa machache ambayo hayana dhamana itatakiwa kesi iwe imeanza kusikilizwa ndani ya kipindi cha miezi sita la sivyo watu watapata dhamana.

Kadhalika, Mhe. Masaju amekemea tabia ya baadhi ya Mawakili kuwalazimisha wateja wao kufungua kesi zisizo na msingi sanjari na tabia ya kuegesha mashauri mahakamani.

Aidha, Jaji Mkuu amewaasa Mawakili hao kuzingatia Kanuni/vitendea kazi muhimu nane katika utumishi wao ambavyo ni pamoja na Uadilifu (Integrity), Uwezo wa kutekeleza majukumu (Competency)Kuwiwa kuona haki inatendeka (Sensitivity to justice)Uwajibikaji (Accountability).

Vingine ni Ubunifu (Creativity), Uchukuaji hatua kwa mapema (Proactivity), Uzalendo wa Kitaifa (National Patriotism) na Uhalisia/ukweli usioegemea upande wowote (Objectivity).

Katika kumalizia Mhe. Masaju amewatakia baraka Mawakili wapya na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki katika shuhuli zao za kila siku za kutetea haki na kuwa wakifanya hivyo watakuwa watu wenye mafanikio makubwa.

“Ombi langu kwa Mwenyezi Mungu ni hili, kwamba Mwenyezi Mungu aendelee kuwabariki katika maisha yenu katika utumishi wenu na shughuli zenu za kutetea haki, haki, na mkifanya hivyo mtafanikiwa sana,” amesema.

Kwa mujibu wa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, kukubaliwa na Kupokelewa kwa Mawakili wa Kujitegemea wapya 774 kunafanya idadi ya Mawakili walioandikishwa nchini kufikia 14,220.

Kati ya Mawakili hao wapya  439 ni Wanaume na 335 ni Wanawake.

Sehemu ya Mawakili wapya wa Kujitegemea wakitoa heshima mbele ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) mara baada ya Kuwapokea na Kuwakubali Mawakili wapya 774 kwenye Sherehe iliyofanyika leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.



Picha za makundi mbalimbali ya Mawakili wapya wa Kujitegemea wakiwa katika sherehe za Kuwapokea na Kuwakubali Mawakili wapya 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Mawakili wapya wa Kujitegemea mara baada ya 
Kuwapokea na Kuwakubali Mawakili wapya wa Kujitegemea 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno akitoa hotuba wakati wa Sherehe ya Kuwapokea na Kuwakubali Mawakili wa Kujitegemea 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.


Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akitoa hotuba wakati wa Sherehe ya Kuwapokea na Kuwakubali Mawakili wa Kujitegemea 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

Sehemu ya Viongozi walioshiriki kwenye Sherehe ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili Wapya wa Kujitegemea leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma. 


Mawakili wa Kujitegemea wapya wakisaini Kiapo cha Uadilifu kwa Mawakili wapya wakati wa
 Sherehe ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili Wapya wa Kujitegemea leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma. 

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja kwenye 
Sherehe ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili Wapya wa Kujitegemea leo tarehe 05 Desemba, 2025 katika ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma. 

Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania waliohudhuria katika sherehe hizo.



Meza kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na makundi kadhaa ya Mawakili wapya wa Kujitegemea mara baada ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili Wapya wa Kujitegemea 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 katika ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma. 

(Picha na MARY GWERA, Mahakama)

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni