Ijumaa, 5 Desemba 2025

MAKUMBUSHO YA MAHAKAMA TANZANIA YANUKIA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Watumishi 12 wa Mahakama ya Tanzania, wakiongozwa na Mkurugenzi kutoka Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu, Bw. Malimo Manyambura, walifanya ziara maalum kwenye Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam kwa lengo ka kujifunza mambo mbalimbali, ikiwemo mbinu bora za uanzishaji, usimamizi na uendeshaji wa makumbusho.

Ziara hiyo ya siku mbili ambayo ilifanyika kuanzia tarehe 2 Desemba, 2025 imewawezesha watumishi hao wa Mahakama kupata uelewa wa namna ya kuanzisha makumbusho, jinsi ya kukusanya taarifa na uendeshaji kwa ujumla.

Wakiwa katika Makubusho hayo ya Taifa, ujumbe huo wa Mahakama ulipokea mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalam waliobobea kwenye masuala ya uhifandhi, walioongozwa na Mkurugenzi wa Makumbusho na Malikale, Bi. Adelaide Sallema.

Mada zilizowasilishwa wakati wa ziara hizo zilihusu makumbusho ni kitu gani, majukumu na kazi zake kwa ujumla na muundo wa uongozi wa makumbusho.

Watumishi wa Mahakama pia walipishwa kwenye mada inayohusu Sheria, Sera na Miongozo ya uanzishwaji na usimamizi wa makumbusho; Dhana ya uhuifadhi katika makumbusho na Kanuni na taratibu za utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kama rasilimali muhimu katika Taasisi.

Mada nyingine zilihusu usimamizi na uendeshaji wa makumbusho na ushiriki wa umma na katika makumbusho. Miongoni mwa wataalam wengine waliowasilisha mada wakati wa ziara hiyo walikuwa Mkuu wa Idara ya Utafiti, Uteuzi wa Maonesho na Uhifadhi Wilbard Lema na Ofisa Utalii Antonia Mkama.

Baada ya kupata mada hizo, watumishi wa Mahakama walipitishwa kwenye maeneo mbalimbali katika Makumbusho ya Taifa kujionea hazina ya makumbusho yaliyopo tangu uhuru, yakiwemo magari ya kifahari yaliyokuwa yanatumiwa na Baba wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Watumishi wa Mahakama pia walitembelea Kijiji cha Makumbusho kilichopo Kijitonyama na kujionea makazi ya asili ya Watanzania wa makabila kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mahakama ya Tanzania imepitia vipindi mbalimbali vya kihistoria tangu kuanzishwa kwake. Historia hii inajumuisha mabadiliko ya kimfumo, uongozi, changamoto zilizojitokeza na mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha utoaji wa haki na utawala wa sheria. Hifadhi ya historia hii ni muhimu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo na ni nyenzo muhimu ya elimu, kumbukumbu na utambulisho wa kitaifa.

Kwa msingi huo, Mahakama ya Tanzania inampango wa kuanzisha Makumbusho ya Mahakama ya Tanzania itakayohifadhi na kuonyesha vifaa na taarifa za kihistoria (Objects and Documentary Materials) ikiwa ni pamoja na nyaraka, vielelezo, picha na vifaa vilivyotumika katika nyakati mbalimbali za kihistoria kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo na kuimarisha uelewa wa umma kuhusu mchango wa Mahakama katika maendeleo ya taifa na utawala wa sheria.

Watumishi wa Mahakama waliofanya ziara hiyo walitoka katika Idara na Vitengo mbalimbali, ikiwemo Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu (DRM), Idara ya Usimamizi wa Mashauri (DCM), Idara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (DICT), Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu (DARHM), Idara ya Usimamizi na Uendelezaji wa Milki (DEDM) na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano (HIECU).


Watumishi 12 wa Mahakama ya Tanzania wakiwa na wenyeji wao wakati wa ziara kwenye Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.


Mkurugenzi kutoka Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu, Bw. Malimo Manyambura [kushoto] akipokea zawadi kutoka Mkurugenzi wa Makumbusho na Malikale, Bi. Adelaide Sallema wakati wa ziara hiyo.

Mkurugenzi kutoka Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu, Bw. Malimo Manyambura akizungumza wakati wa ziara hiyo. Picha mbili chini ni Mkurugenzi wa Makumbusho na Malikale, Bi. Adelaide Sallema.
 


Watumishi wa Mahakama ya Tanzania [juu na chini] wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa ziara hiyo.



Ofisa Utalii Antonia Mkama akifafanua jambo.

Ofisa Utalii Lisa Shirima akitoa maelezo kwa watumishi wa Mahakama wakati wa ziara hiyo. Picha chini akitoa maelezo kuhusu magari ya kifahari yaliyotumiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.


Muhifadhi Elimu Mwandamizi kutoka Kijiji cha Makumbusho, Bi. Wilhelmina Joseph akitoa maelezo kwa watumishi wa Mahakama walipotembelea kijiji hicho.

Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakifanya 'demo' ya kusikiliza shauri kwenye Mahakama ya Wakinga baada ya mtuhumiwa [aliyekaa katikati] kukamatwa ugoni. Watumishi hao walikuwa kwenye Kijiji cha Makumbusho.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni