Ijumaa, 5 Desemba 2025

UWAKILI NI WITO WA HAKI: MWABUKUSI

  • Serikali yasisitiza ushirikiano kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wananchi

Na HALIMA MNETE, Mahakama-Dodoma

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno wamewahimiza Mawakili wapya 774 kuutumikia wito wao kwa uadilifu, uzalendo na ushirikiano katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.

Akizungumza leo tarehe 05 Desemba, 2025, kwenye Sherehe za Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili hao wapya, Wakili Mwabukusi amesema kuwa kazi ya uwakili siyo ajira ya kawaida bali ni wito wa kuhudumia haki na jamii kwa mujibu wa Katiba na misingi ya utawala bora.

Akizungumza katika Sherehe hito, Rais wa TLS amesema kuwa kuwakilisha wateja ni kuhudumia haki, kulinda misingi ya katiba na kuendeleza utawala wa sheria unaozingatia usawa na haki za binadamu.

“Wakili ni mtu ambaye kiwango chake cha uzalendo kwa Taifa, ujasiri katika kusimamia na kulinda Katiba na sheria, pamoja na utawala bora na haki za binadamu, kinapaswa kuwa cha juu kuliko kitu kingine chochote,” amesema Wakili Mwabukusi.

Ameongeza kuwa, Mawakili ni nguzo muhimu katika jamii na wanapaswa kuishi kwa maadili, uadilifu na ukweli, huku akisisitiza kuwa uaminifu kwa wateja, mahakama na jamii ni mtaji mkubwa unaojengwa kwa muda mrefu lakini unaweza kupotea kwa kosa moja.

Wakili Mwabukusi pia amewakumbusha mawakili wapya umuhimu wa elimu endelevu, kujitolea kwa ajili ya wanyonge, kuheshimu mahakama na kushirikiana kwa karibu na mihimili ya dola kwa maslahi ya taifa. Aidha amesisitiza kuwa Chama cha Wanasheria Tanganyika si mpinzani wa Serikali bali ni mshirika katika kusimamia utawala wa sheria, haki za binadamu na utawala bora.

Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewapongeza mawakili wote waliokubaliwa pamoja na Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania) kwa kazi kubwa ya kuwaandaa wanataaluma hao.

Amesema mafanikio ya Mawakili wapya ni matokeo ya jitihada za muda mrefu za walimu, wazazi, walezi, Serikali na wadau mbalimbali waliochangia katika safari yao ya kitaaluma.

Bw. Maneno ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya Sheria, akieleza kuwa ongezeko la mawakili nchini litaongeza kasi ya upatikanaji wa haki kwa wananchi na kusaidia kupunguza changamoto za kisheria.

Ameeleza kuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kushirikiana bega kwa bega na mawakili pamoja na wadau wa haki jinai na madai katika kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.

“Mawakili ni kiungo muhimu kati ya wananchi na mahakama. Mna nafasi kubwa sana ya kuhakikisha haki inapatikana kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, usawa na haki za binadamu,” amesema.

Kauli za Viongozi hao zimekuja wakati ambapo Taifa linaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya mawakili, hali inayotajwa kuwa chachu ya kuimarisha utawala wa sheria, amani na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno akizungumza wakati wa Sherehe ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili wa Kujitegemea wapya 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akitoa hotuba yake wakati wa Sherehe ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili wa Kujitegemea wapya 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.






Baadhi ya makundi ya Mawakili wa Kujitegemea wapya wakifuatilia hotuba zilizokuwa zikitolewa wakati wa Sherehe ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili wa Kujitegemea wapya 774 leo tarehe 05 Desemba, 2025 kwenye ukumbi wa Mabeyo jijini Dodoma.

(Picha na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni