Alhamisi, 5 Februari 2026

HUDUMA YA MAHAKAMA INAYOTEMBEA KIGAMBONI YAANZISHWA

Na MWANDISHI WETU-Mahakama, Dar es Salaam

Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia (IJC) Temeke kimeanza rasmi kutoa huduma ya Mahakama Inayotembe katika Wilaya ya Kigamboni, Mtaa wa Mjimwema zilipo Ofisi za Mtendaji Kata.

Kuanzishwa kwa huduma hiyo ya kimahakama kulitanguliwa na kipindi cha kumepambazuka kilichoendeshwa katika Mahakama hiyo, kikilenga kufikisha ujembe kwa wakazi wa Wilaya ya Kigamboni kuhusu kuanzishwa kwa shughuli za usikilizwaji wa mashauri ya mirathi, ndoa na talaka katika Mahakama Inayotembea ndani ya Wialaya hiyo.

Kipindi hicho kiliongozwa na Mtangazaji Abdalah Kulwa wa Radio One na Mzungumzaji akiwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo ndani ya IJC Temeke, Mhe. Upendo Kapama.

Mhe. Kapama alifafanua kwamba Mahakama Inayotembea itatoa huduma za mashauri ya mirathi, ndoa na talaka yanayosikilizwa na Mahakama ya Mwanzo, na mpango huo unalenga kusogeza huduma kwa wananchi.

Aliendelea kusema kwamba sasa Wilaya ya Kigamboni, Mtaa wa Mjimwema patakuwa na Kituo kitakachotoa huduma kila siku ya Jumatano ili kuwaepushia wananchi adha ya kusafiri, muda na gharama za kutoka Kigamboni hadi Temeke.

Mhe. Kapama alieleza jinsi Mahakama Inayotembea inavyowasaidia Wananchi katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa kupata elimu na huduma bora kwa haraka mtaani kwako. Huduma hii inatolewa katika Wilaya ya Kinondoni, Bunju A Ofisi za Mtendaji Kata, Wilaya ya Ubungo Kibamba zilipo Ofisi za Mkuu wa Wilaya na Wilaya ya Ilala Chanika Ofisi za Mtendaji Kata na sasa ni Kigamboni.

Alisisitiza huduma hii inaongeza ufunguaji wa mashauri katika maeneo hayo kwa sababubu wananchi wengi wanapata elimu kubwa ya masuala ya familia, mirathi na ndoa na wanarahisishiwa kwa kufuatwa walipo.

Pia Mhe. Kapama aliendelea kuonyesha jinsi gani Mahakama hiyo inavyowarahisishia wagonjwa kutoa ushahidi kwa kutokusafiri umbali mrefu, hivyo kupunguza gharama na muda.

Mhe. Kapama alisema matarajio ya kusogeza huduma hiyo Mjimwema Kigamboni ni kuondoa dhana ya watu kuishi kimazoea pindi wanapopoteza wapendwa wao na kufuata sheria kwa kufungua mirathi mapema ili kuondoa migogoro katika familia inayoweza kutokea, hivyo kwa kusogezewa Mahakama Inayotembea kutaondoa changamoto hizo.

Aidha, Mhe. Kapama aliwahimiza wakazi wa Kigamboni kujitokeza kwa wingi ili kupata elimu na kufungua mashauri kwa wale wenye uhitaji na mashauri yao yatasikilizwa hapo hapo ndani ya Mahakama Inayotembea kwa haraka, kwani mashauri huchukua siku 30 hadi kusomwa hukumu.



Mahakama Inayototembea ikiwa Wilaya ya Kigamboni, Mtaa wa Mjimwema. Picha chini, wadau wakiwa ndani ya Mahakama Inayotembea.


 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo ndani ya IJC TemekeMhe. Upendo Kapama akiwa ndani ya Mahakama Inayotembea.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni