Jumatano, 25 Februari 2026

JAJI MKUU AWATAKA MAJAJI, MAHAKIMU KUWAJIBIKA IPASAVYO

Na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma

Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, amewataka Majaji na Mahakimu nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwa kujituma bila kusubiri maelekezo kutoka kwa Viongozi.

Mhe. Masaju ametoa maagizo hayo leo tarehe 25 Februari, 2026 wakati akifungua Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kinachofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.

“Mimi siku zote naimba wimbo juu ya kujituma (Proactivity) na hili sio sharti langu kama nimelibuni, ni sharti la Katiba lipo kwenye Ibara ya 25 ya Katiba na kujituma huku kunatokana na kuwajibika,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Masaju amesema Ibara ya 25 ya Katiba inazungumza juu ya uwajibikaji wa watumishi wote wa Serikali na kila mtu, katika hotuba yangu nilipoongea na Wasajili tarehe 22 Desemba, 2025 nilizungumza kwamba hatuwezi kuishi kwa maelekezo, sisi ni binadamu tuna akili kuliko Wanyama, tunatambua wajibu wetu na tunapaswa kujua kwamba ili kama binadamu tuweze kuendelea kimwili, kiroho na kiakili tunapaswa tufanye nini,” amesema Mhe. Masaju.

Sambamba na hilo, Jaji Mkuu amewataka Maafisa Mahakama hao kujituma wanapotimiza majukumu yao kwa kuwa pia ni takwa la kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Masaju ameongeza kwa kuwataka Majaji hao kuwajibika kama Viongozi kwa kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwa kuwa Mahakama inapaswa kukimbiliwa na wananchi.

Kadhalika, Jaji Mkuu ametoa rai kwa Majaji Wafawidhi kusimamia nidhamu za Mahakimu na Watumishi wengine wa Mahakama sambamba na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

 

“Endeleeni kusimamia kikamilifu nidhamu za watumishi wote walioko chini yenu na hasa Mahakimu. Kama nilivyosema kwenye Mkutano wa TMJA kuwa tutarekebisha Sheria ya Usimamizi wa Mahakama ( Judiciary Administration Act, Cap. 237) ili Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya zisimamiwe na Maafisa wa Mahakama wenyewe,” amesisitiza Mhe. Masaju.

 

Jaji Mkuu amesema suala la nidhamu na maadili linahitaji ujasiri, uadilifu mkubwa na dhamira ya ndani ili kulisimamia na kusema kuwa, “tusiposimamia eneo hili kwa umakini,  mabadiliko yanayopendekezwa yanaweza kutafsiriwa kuwa yalilenga kufichiana madhaifu yetu na si vinginevyo.”

 

Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju amewapongeza Majaji na Mahakimu kwa kuendelea kutekeleza jukumu la utoaji haki kikamilifu.

 

“Mwaka 2024, Mahakama ilipokea jumla ya mashauri 242,309, huku mashauri 244,808 yakiamuliwa katika mwaka huo, mwaka 2025, Mahakama ilipokea jumla ya mashauri 243,848, sawa na ongezeko la takribani asilimia 0.6 ya mashauri yaliyopokelewa ikilinganishwa na mwaka 2024. Katika mwaka huo, Mahakama iliamua jumla ya mashauri 254,793,” amesema Jaji Mkuu.

 

Amesema takwimu hizo zinaonesha mambo makuu matatu yenye umuhimu mkubwa, ambayo mosi ni licha ya kuongezeka kwa idadi ya mashauri yanayopokelewa, jitihada zimefanyika ili kukabiliana na ongezeko hilo, pili ni kwa miaka yote miwili (2024 na 2025), Mahakama imefanikiwa kuamua mashauri mengi zaidi kuliko yaliyopokelewa katika mwaka husika.

 

Mhe. Masaju amesema ongezeko kubwa la mashauri yaliyoamuliwa mwaka 2025 (254,793) linaonesha kasi iliyoimarishwa ya utoaji haki, nidhamu katika usimamizi wa mashauri, pamoja na kujituma kwa watumishi wa Mahakama katika kutekeleza wajibu wao.

 

“Sambamba na hilo, nawapongeza pia kwa jitihada mlizochukua kusikiliza na kuyatolea uamuzi mashauri ya kiuchumi katika zoezi lililoanza mwezi Oktoba 2025 na kumalizika Desemba, 2025 kwa mafanikio makubwa,” amesema Jaji Mkuu.

 

Mhe. Masaju amebainisha kwamba, kwa kipindi kifupi cha mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025, jumla ya mashauri 2,973 yenye thamani ya Tshs. 13,190,729,076,332 yalisikilizwa na kumalizika.

 

“Baadhi ya fedha hizo zimeingia kwenye matumizi, biashara na uwekezaji, hivyo kuchangia katika ukuaji wa Uchumi,” amesema Jaji Mkuu.

 

“Tuendelee na mikakati hii kuhakikisha kuwa Mahakama inatoa mchango wake katika kukuza uchumi kupitia jukumu lake la utoaji haki. Kufanya hivyo pia ni kutekeleza kwa vitendo Nguzo ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo ni Uchumi Imara, Jumuishi na Shindani,” amesisitiza Mhe. Masaju.

 

Kwa upande mwingine, Mhe. Masaju ametoa maelekezo kwa Majaji Wafawidhi kuyapa kipaumbele mashauri ya Mirathi ambapo amesema, “tarehe 22 Desemba, 2025 nilipofanya kikao na Wasajili na Naibu Wasajili niliwasisitiza kuweka kipaumbele kwenye usikilizaji wa mashauri ya mirathi.”

 

Jaji Mkuu amesema kwa upande wa Mahakama ya Rufani tayari hatua zimechukuliwa ambapo mashauri 68 ya mirathi yaliyoiva kusikilizwa yamepangwa kwenye kikao cha Mahakama ya Rufani cha Mwezi Februari, 2026.

 

“Haya ni mashauri yanayohitaji kushughulikiwa kwa uharaka ili wanufaika wake ambao mara nyingi ni wanawake na watoto wapate haki zao mapema ipasavyo,” amesema Mhe. Masaju.

 

Ameongeza kuwa, ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri hayo husababisha changamoto nyingi hasa kwa wananwake na watoto, pia fedha nyingi huzuiliwa kuingia kwenye uchumi.

 

Jaji Mkuu amesema hakuna sababu ya kuyaweka mashauri hayo kwenye utaratibu wa kawaida wa kupanga mashauri (FIFO). Mashauri mengine ya kuyapa kipaumbele ni mashauri yanayogusa Wanawake na Watoto ni takwa la kisheria kupitia Kanuni ya 5 (Rule 5) ya The Judicature and Application of Laws (Practice and Procedure in Cases Involving Vulnerable Groups) Rules, 2019 GN No. 110 of 2019).

 

Aidha, Mhe. Masaju ametoa rai kwa Majaji hao kutoa mapendekezo ya uboreshaji wa sheria na kanuni mbalimbali na kuzitumia ipasavyo katika kuharakisha jukumu la utoaji haki mapema ipasavyo. Amesema tangu Juni hadi Desemba, 2025 kanuni mbalimbali zipatazo 22 zimetungwa na kuboreshwa.

Akizungumzia kuhusu viwanja na ujenzi, Jaji Mkuu amewataka Majaji kuwa sehemu ya ufuatiliaji na upatikanaji wa Viwanja vya Ujenzi wa Mahakama za Mwanzo na Nyumba za Mahakimu.

 

“Kila mmoja awe sehemu ya mkakati huu, tumeieleza Serikali kuwa, jukumu la ujenzi wa Mahakama za Mwanzo katika kila Kata ni jukumu lao na ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu lao la kikatiba kwa mujibu wa Ibara 146(2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wamelikubali na kulichukua jukumu hilo,” amesema Mhe. Masaju.

 

Jaji Mkuu ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaelekeza kuwa TAMISEMI itekeleze jukumu hilo, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa, kwenye kanda yake kila Kata inapata kiwanja chenye ukubwa usiopungua hekari mbili  kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo na nyumba za Mahakimu.

 

Sambamba na hilo, Mhe. Masaju ametoa rai kwa Majaji  hao kusimamia utunzaji wa Majengo ya Mahakama ambapo amesisitiza kwa kusema, “Jitihada za ujenzi wa Mahakama majengo ya ya Mahakama ziende sambamba na utunzaji wa majengo hayo.”

 

Amesema Rais Samia alipozindua jengo la Makao Makuu ya Mahakama alielekeza Watumishi wa Mahakama kutunza majengo ya Mhimili huo.

 

“Kwa sasa tunayo majengo mengi na mazuri na mengine yanakamilika mwezi Machi mwaka huu. Natoa rai kwa watumishi wote wa Mahakama na wadau wanaotumia majengo hayo kuyatunza, na pia kuweka mpango endelevu wa kuyatunza majengo hayo,” amesisitiza.

 

Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu amewataka Majaji Wafawidhi na Viongozi wengine wa Mahakama kuzingatia na kutekeleza ipasavyo maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Viongozi, huku akiwakumbusha maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Mahakama  na Wadau aliyoyatoa katika hotuba yake ya Siku ya Sheria Nchini tarehe 02 Februari, 2026 ambayo ni pamoja na Kutoa haki kwa kuzingatia masharti yaliyoainishwa kwenye ibara ya 107A(2)(a)-(e) na 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kuheshimu na kuulinda uhuru wa Mahakama bila kuutumia vibaya.

 

Maelekezo mengine ni Kutotumia uhuru huo kama kichaka cha kuficha uzembe na vitendo visivyo vya haki, Kutenda kwa uadilifu na uwazi na mengine.

 

Vilevile, amewataka kutekeleza na kuisimamia mikakati ya Mkutano wa Wadu wa Kutathmini kuhusu Mikakati ya Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki, Ardhi na Ushindani wa Kibiashara na pia Mikakati ya Mkutano wa Mahakama na Wadau Kuhusu Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani.

 

“Pamoja na kwamba mikakati ya mikutano yote miwili ilichapishwa katika tovuti ya Mahakama,  nimeona ni vyema nikawakumbusha tena mikakati hiyo, nikianza na mikakati ya Ushirikiano na Mahusiano katika Utekelezaji wa Majukumu ya Utoaji Haki Mahakamani; ambapo Kila taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa utendaji haki mahakamani iwajibike ipasavyo kutekeleza jukumu lake kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya utumishi yanayosimimamia taasisi husika, Wadau wote waheshimu na kulinda hadhi na ukuu wa Mahakama. Aidha, Mahakama kwa upande wake, isimamie ipasavyo sheria na kanuni zilizopo, ikiwemo sheria inayohusu kosa la kuidharau Mahakama (contempt of court) ili kulinda hadhi na ukuu wake,” amesema.

 

Lengo la Kikao hicho ni Kutathmini taarifa za utendaji kazi kwa mwaka 2025 – Taarifa ya Mashauri, Ukaguzi wa Mahakama, Maboresho ya Huduma za Mahakama, TEHAMA, Utekelezaji wa bajeti 2025/2026 na mipango ya 2026/2027 na miradi ya majengo ya Mahakama.

 

Lengo lingine ni kubaini mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa majukumu hayo, kutafuta ufumbuzi kwa pamoja, kuweka mikakati ya utekelezaji wa majukumu yetu kwa mwaka 2026, kupata taarifa fupi kutoka kwa kila Jaji Mfawidhi kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mahakama katika eneo lake na Kubadilishana uzoefu kupitia mawasilisho hayo.


Aidha, Katika kuyaenzi maisha ya marehemu Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kikao hicho, Jaji Mkuu aliwaongoza Majaji Wafawidhi na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania walioshiriki kusimama kwa dakika moja ikiwa ni Ishara ya kumkumbuka mtumishi huyo wa Mungu aliyetangulia mbele za haki.


Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju [juu na chini], akizungumza wakati anafungua Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 25 Februari, 2026 katika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya, akitoa utambulisho wa Majaji mbalimbali wanaohudhuria kikao hicho.

Sehemu ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania [juu na chini] ikiwa kwenye kikao hicho.

Sehemu nyingine ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania [juu na chini] ikiwa kwenye kikao hicho.



Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi hao.
(Picha na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma)







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni