Jumatano, 25 Februari 2026

JAJI KIONGOZI AHIMIZA UTEKELEZAJI WA MIKAKATI YA VIKAO

  • Ataka mashauri ya rushwa, uhujumu uchumi kupewa kipaumbele

Na HABIBA MBARUKU- Mahakama Dodoma

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustepher Mohamed Siyani, amewasisitiza Majaji, Mahakimu na Wakurugenzi wa Mahakama ya Tanzania kuhakikisha wanatekeleza mikakati inayowekwa na vikao mbalimbali pamoja na kuwasilisha utekelezaji wake kwa wakati.

Mhe. Dkt. Siyani ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Februari, 2026 kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju, kufungua kikao cha mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kwa mwaka 2026, kinachofanyika katika ukumbi wa Mahakama, Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Jaji Kiongozi amesema kuwa lengo na shabaha ya vikao hivyo ambavyo hufanyika walau mara moja kila mwaka ni kupata fursa ya kujipima na kujitathmini juu ya utendaji kazi wa Mahakama, sambamba na utekelezaji wa Dira na Dhima ya Mahakama.

“Kwa hiyo, lengo la vikao hivi ni kujitathmini wapi tumefanya vizuri lakini pia maeneo gani hatukufanya vizuri, matokeo ya tathmini hii ni kuboresha mchakato mzima wa utoaji haki nchini, jukumu ambalo Mahakama imekasimiwa na umma kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Mhe. Dkt. Siyani.

Ameeleza kuwa siyo vema hata kidogo kwa Viongozi kusubiri maelekezo ili kutekeleza mikakati inayowekwa. Amemtambua kwa namna ya pekee Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Alvin Mgeta, ambaye amekua akitekeleza mikakati ya vikao mbalimbali bila kusubiri barua au maelekezo kutoka Mahakama Kuu.

“Ninalolisema kwa Waheshimiwa Majaji nalisema pia kwa Wakurugenzi wengine ambao kwa nafasi zao wanahudhuria vikao hivi na hivyo wana wajibu wa kutekeleza mikakati na yale ambayo yanaelekezwa, siyo vema hata kidogo kwa Viongozi kusubiri maelekezo ili kutekeleza mikakati inayowekwa,’amesisitiza Jaji Kiongozi.

Akitoa taswira ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu na Mahakama zilizopo chini yake, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa Mahakama ya Tanzania ilivuka mwaka 2024 kukiwa na mashauri yaliyobaki 38,121.

Jaji Kiongozi amebainisha kuwa mwaka 2025, jumla ya mashauri 240,607 yalipokelewa na mashauri 250,388 yalimalizika, huku kiwango cha uondoshaji wa mashauri kikiongezeka kutoka asilimia 83 mwaka 2024, hadi kufikia asilimia 88 mwaka 2025.

Mhe. Dkt. Siyani ameeleza kuwa mafanikio hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 5.4 kwa Mahakama Kuu na Mahakama za chini. Ameeleza pia kuwa wastani wa muda wa shauri kukaa mahakamani umeendelea kupungua kutoka siku 78 mwaka 2024 hadi siku 66 mwaka 2025.

Ameongeza kuwa pamoja na ongezeko la mashauri yaliyopokelewa mwaka 2025, mzigo wa mashauri kwa kila Jaji au Hakimu umeendelea kupungua, ambapo wastani kwa mwaka 2024 ulikuwa mashauri 228 kwa kila Jaji au Hakimu na umepungua hadi kufikia 222 kwa mwaka 2025.

Kadhalika, Jaji Kiongozi amebainisha kuwa uimarishaji wa Mahakama Inayotembea umeendelea, ambapo kwa mwaka 2025 Mahakama hiyo imewafikia wananchi 9,069 na hivyo kuvuka shabaha ya mwaka 2024 ambayo ilikuwa kufikia watu 5,833.

Ameongeza kuwa kwa mwaka 2025 mchakato wa uchaguzi mkuu ulisababisha kufunguliwa kwa mashauri 15 kabla ya uchaguzi, na kwamba ni shauri moja pekee ambalo limesalia Mahakama Kuu kwa sababu ya uwepo wa shauri la marejeo katika Mahakama ya Rufani.

Aidha, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, jumla ya mashauri 12 ya kupinga matokeo ya ubunge na mashauri madogo 11 yanayotokana na mchakato huo yalifunguliwa kwenye Masjala mbalimbali za Mahakama Kuu, huku Mahakama za Hakimu Mkazi zikipokea mashauri 29 ya kupinga matokeo ya udiwani na mashauri ya maombi madogo 24 yanayohusiana na mashauri hayo, hiyo kufanya jumla ya mashauri yote yaliyotokana na matokeo ya uchaguzi kuwa mashauri 76.

Jaji Kiongozi amesema kuwa usikilizaji wa mashauri hayo unaendelea na hadi kufikia tarehe 25 Februari, 2026, mashauri matatu ya msingi na madogo mawili pekee yamebaki kati ya mashauri 23 ya Mahakama Kuu,  huku upande wa Mahakama ya Hakimu Mkazi yakiwa yamesalia mashauri matatu peke kati ya mashauri 53 yaliyofunguliwa.

Sambamba na hayo, Mhe. Dkt. Siyani ameeleza kuwa mkakati wa kusikiliza mashauri yanayochochea ukuaji wa uchumi, uliwekwa katika vikao vilivyofanyika mwezi Septemba na Oktoba, 2025 na utekelezaji wake ulifanyika, ambapo Mahakama Kuu na Mahakama za Hakimu Mkazi zilifanikiwa kusikiliza mashauri 2,675 yaliyowezesha kuachilia kiasi cha shilingi za Kitanzania 11,940,395,000,000.

Vilevile, ameeleza kuwa, ugatuzi uliofanywa kwa wasimamizi wa mashauri ya uhujumu uchumi,kupitia uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa kwenda kwa Majaji wote wa Mahakama Kuu, umechangia kufanikisha usikilizaji wa mashauri 28 chini ya usimamizi wa Masjala mbalimbali nchini.

Jaji Kiongozi ameeleza kuwa Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ikimaliza mashauri 16 kati ya 88 yaliyokuwepo wakati hati hiyo inatolewa. Ameongeza kuwa pamoja na uwepo wa hati hiyo, bado kuna wastani wa mashauri 133 yanayoendelea kwenye Masjala mbalimbali za Mahakama Kuu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Siyani amewataka Majaji kuyapa kipaumbele mashauri ya rushwa na uhujumu uchumi kama ambavyo wanayapa kipaumbele mashauri mengine ambayo yapo katika Masjala zao.

“Nichukue fursa hii kuwataka Waheshimiwa Majaji kuyapa kipaumbele mashauri haya kama mnavyoyapa mashauri mengine yaliyopo katika Masjala zao” amesisitiza Jaji Kiongozi.

Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa hatua imepigwa katika eneo la usimamizi wa mashauri ya mirathi, hususan ulipaji wa fedha za mirathi na utekelezaji wa kanuni mpya za mirathi.

Amesema kuwa kumbukumbu zilizopo zinaonesha kati ya tarehe 01 Oktoba, 2025 na tarehe 17 Februari, 2026, fedha za mirathi zilizokuwa kwenye akaunti za Mahakama zimepungua kutoka wastani wa shilingi Kitanzania 53 bilioni hadi bilioni 36.

Jaji Kiongozi amesisitiza kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa bado Mahakama ina kazi kubwa ya kufanya katika eneo hilo, huku akiwasihi Majaji kutumia kikao hicho kama fursa ya kubadilishana uzoefu ili kuimarisha usimamizi wa mashauri.

“Takwimu hizi zinaonesha kuwa bado tuna kazi ya kufanya katika eneo hili, ni matumaini yangu kuwa Waheshimiwa Majaji watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na hivyo kuimarisha usimamizi wa mashauri haya, hususan ulipaji wa fedha za mirathi zilizopo kwenye akaunti za Mahakama,” amesema Jaji Kiongozi.

Akizungumza kuhusu matumizi ya mifumo mbalimbali ya kieletroniki mahakamani, Mhe. Dkt. Siyani amesema kuwa Mahakama inaendelea kutilia mkazo matumizi hayo kwa lengo la kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo, pamoja na matumzi ya mifumo mingine ya TEHAMA kama Mfumo wa Kuratibu na Kusikiliza Mashauri (ESMS).

Jaji Kiongozi ameongeza kuwa mwaka 2025, Mahakama ilianza rasmi kutumia mfumo wa kieletroniki wa upimaji na utendaji kazi kwa Maofisa wa Mahakama.

Kadhalika, amesema kuwa Mahakama imeendelea kuimarisha ukaguzi wa Mahakama na Magereza kama sehemu ya kupima na kupata mrejesho wa ubora, ufanisi pamoja na kubaini changamoto za utoaji haki.


Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani [juu na chini], akizungumza kwenye Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 25 Februari, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.


Sehemu ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania [juu na chini] ikiwa kwenye kikao hicho.




Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, akizungumza kabla ya ufunguzi wa kikao hicho.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju [juu na chini] ikiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.



Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni