Na HABIBA MBARUKU, Mahakama-Dodoma
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
George Masaju amewataka Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo kuzingatia
usalama, maadili na umoja katika kutimiza majukumu yao huku wakimtanguliza
Mungu mbele kama walivyoapa katika viapo vyao.
Mhe. Masaju ametoa wito huo leo tarehe 23
Februari, 2026 mara baada ya kuwaapisha Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo
wapya 90 katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mahakama, Makao Makuu ya Mahakama
ya Tanzania jijini Dodoma.
“Ninyi ambao mmeapishwa leo hamkuapa mbele
yangu mimi, mlikuwa mnaapa kwa Mwenyezi Mungu, nimeona huwa mmebeba hivyo
vitabu wengine walishikilia Biblia wengine Quran Takatifu, mlivyokuwa mnaapa
sikusikia mkisema eee Jaji Mkuu nisaidie, kila mmoja alisema Ee Mwenyezi Mungu
nisaidie kwa kadri mlivyokula hivyo viapo njooni mviishi, yale maneno
mliyokuwa mnakula yapo kwenye Ibara ya 107A (1) na Ibara ndogo ya kwanza na Ibara
ndogo ya pili a na b lakini yapo pia katika Ibara ya 107B nendeni
mkayaishi,”amesisitiza Jaji Mkuu.
Akizungumza baada ya zoezi la uapisho, Mhe.
Masaju amesisitiza kuwa dhamana ya utoaji haki ni jukumu zito linalohitaji
nidhamu, uaminifu na weledi wa hali ya juu na kueleza kuwa Mahakimu hao
wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya sheria, kuepuka upendeleo na
kuhakikisha kuwa yale wanayotaka kutendewa nao wawatendee wengine vivyo hivyo.
Akizungumza kuhusu uadilifu katika kazi,
Mhe. Masaju amewaasa Mahakimu hao kutopokea wala kutoa rushwa kwa
sababu rushwa huchangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha maadili ya utumishi na
kwamba sifa kubwa ya Mahakimu hao inapaswa kuwa unyenyekevu na kuongeza kuwa
kadri wanapokuwa na ukubwa wa madaraka ndivyo hivyohivyo kiwango chao cha
unyenyekevu kinapaswa kuongezeka na wawe watumishi wa watu wote.
“Kwenye Quran Tukufu Sura ya pili Aya ya
188 inasema hivi wala msiliane mali zenu kwa batili kinyume cha haki na
kuzipeleka kwa Mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa shamba na
hali mnajua, amesisitiza Jaji Mkuu.”
Katika hatua nyingine, Mhe. Masaju ameweka
wazi kuwa, watumishi wanapaswa kuwa mfano kwa watu wengine hasa kwa kukiishi
kiapo cha maadili ya kazi na kwamba yeyote atakayekiuka maadili na sheria za
kazi Mahakama haitasita kumchukulia sheria na kumuwajibisha Mahakamani huku akieleza
wazi kuwa, sifa ya Mahakama inaharibika pale tu watumishi wanapokiuka maadili ya
utumishi na wanaposhiriki katika vitendo vya rushwa hivyo wajue kuwa Serikali
inawatazama lakini Mungu pia anawatazama.
Kadhalika Jaji Mkuu amewataka Mahakimu
hao kutofungwa na Masharti ya kiufundi kupita kiasi hali ambayo itadhoofisha
utendaji wao wa kazi huku akiwasisitiza kwamba wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao
kama nguzo ya kutoa haki kwa jamii inayowatazama na kuwategemea.
Sambamba na hayo, Mhe. Masaju amewaasa
Mahakimu hao kutotumia vibaya uhuru wa Mahakama kwa kuingiza uzembe na kukiuka
Katiba na Sheria huku akiwataka wafanye tafiti za kutosha kabla ya kufanya
maamuzi.
Kuhusu suala la mlundikano wa mahabusu,
Jaji Mkuu ameeleza kuwa mshtakiwa ana haki ya kupata dhamana hivyo mtu anaweza
kupata dhamana kwa kudhaminiwa au kujidhamini mwenyewe.
Aidha Jaji Mkuu amebainisha kwamba, Mahakama
ni Mhimili muhimu wa Dola unaosimamia haki na kudumisha amani katika jamii,
hivyo kila Hakimu ana wajibu wa kulinda heshima, hadhi na taswira ya Mahakama mbele
ya wananchi.
Katika hatua nyingine Mhe. Masaju amewataka Mahakimu
hao kujenga umoja na mshikamano katika maeneo yao ya kazi na kuwahimiza kujifunza
kwa watumishi watakaowakuta katika maeneo watakayopangiwa kazi, huku akisisitiza
kuwa nguvu ya Mahakama ipo katika ushirikiano, uwajibikaji na kufanya kazi kwa
kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa.
Ameongeza kuwa, kila Hakimu anapaswa kuwa mfano wa
kuigwa katika jamii kwa matendo na maamuzi yake, huku akitumia maarifa na
uzoefu wake katika kuchambua masuala na kutoa maamuzi sahihi kwa kuzingatia
sheria.
Akisisitiza kuhusu utumiaji wa Mahakama,
Jaji Mkuu amewashauri Mahakimu hao kutoruhusu Mahakama kutumia vibaya wala
kukubali mahairisho ya kesi yasiyo na msingi, pia wahakikishe mashauri yaliyo
mbele yao yanahitimishwa mapema ipasavyo kwa kuzingatia sheria.
“Sasa nina ushauri mwingine ninapoenda
kumaliza moja msiruhusu Mahakama zitumike vibaya kupitia mashauri yaliyopo
mbele yenu, mbili msikubali mahairisho ambayo hayana msingi yasiyokuwa na
sababu za msingi, tatu hitimisheni mashauri yaliyoko mbele yenu mapema
iwezekanavyo kwa kuzingatia Katiba na sheria sio kulipua” amesisitiza.
Mhe. Masaju amezungumzia pia kuhusu watu wa makundi maalumu katika jamii kama watoto, wajane na yatima katika jamii. Pamoja na hayo ameeleza kuwa, katika kupunguza urasimu kwenye masuala ya mirathi, kuleta uwazi na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za mirathi na kuweka udhibiti dhidi ya wasimamizi wa mirathi wenye dhamira ya kutumia vibaya fedha na mali za marehemu, kunahitajika kinga mahsusi kuhusu makundi hayo.
“Katika kanuni ya tano katika kesi za makundi maalum tumetunga kanuni hapo… tumeweka mwongozo unaosimamia mashauri
haya yanayowahusu watu wenye mahitaji maalumu ni yatima, ni mjane hana mtetezi,
ni watoto ni wanawake katika jamii nyingine ambayo wanawake wanapuuzwa, Jaji au
Hakimu anayesikiliza shauri linalohusiana na hao watu katika makundi hayo
katika hatua zote anapokuwa anasikiliza mashauri hayo ikijumuisha wakati wa
usajili wa shauri lake wakati wa kusikiliza na kuliamua anapaswa ayape
kipaumbele mashauri ya aina hii na hata sisi tunafanya hivyo,” amesisitiza.
Aidha, Jaji Mkuu amewasisitiza Mahakimu hao kuhusu umuhimu wa kuwa na uadilifu pamoja na kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu kwa ufanisi, akieleza kuwa, wananchi wanatarajia kuona mashauri yakisikilizwa na kuamuliwa mapema ipasavyo bila ucheleweshaji usio wa lazima huku akiweka wazi kuwa kuchelewa kwa haki kunaweza kuathiri imani ya wananchi kwa Mahakama.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi Wapya wa
Mahakama za Mwanzo, wakila kiapo cha uaminifu mbele ya Jaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya uapisho wao iliyofanyika leo tarehe 23 Februari, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya
Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Sehemu ya Mahakimu Wakazi Wapya wa
Mahakama za Mwanzo, wakisaini viapo vyao vya uadilifu mbele ya Jaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya
uapisho iliyofanyika leo tarehe 23 Februari, 2026 katika ukumbi wa Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akisaini viapo vya Mahakimu Wakazi Wapya wa Mahakama za Mwanzo, aliowaapisha leo tarehe 23 Februari, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania Jijini Dodoma. Aliyesimama kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju akizungumza na Mahakimu Wakazi Wapya wa Mahakama za Mwanzo mara baada ya kuwaapisha leo tarehe 23 Februari, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
George Masaju (aliyesimama mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na
sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Mahakimu Wakazi Wapya wa Mahakama za Mwanzo mara baada ya zoezi la
uapisho lililofanyika leo tarehe 23 Februari, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu
ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Wa pili kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher, Mohamed Siyani, wa tatu kushoto wa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Amidi wa Mahakama hiyo, Mhe. Imani Abood, wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, wa pili kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya na wa kwanza kulia ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wazazi na walezi waliohudhuria katika Hafla ya Uapisho wa Mahakimu Wakazi Wapya wa Mahakama za Mwanzo iliyofanyika leo tarehe 23 Februari 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Dini waliohudhuria katika hafla ya uapisho wa Mahakimu Wakazi wapya wa Mahakama za Mwanzo iliyofanyika leo tarehe 23 Februari, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
Sehemu nyingine ya Mahakimu Wakazi Wapya wa Mahakama za Mwanzo wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. George Masaju (aliyesimama mbele katikati) mara baada ya zoezi la uapisho lililofanyika leo tarehe 23 Februari, 2026 kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)









Hakuna maoni:
Chapisha Maoni