- Wadau nao waipa Kongole Mahakama kwa uondoshaji wa mashauri hayo yanayochochea ukuaji uchumi
Mhe. Masaju ameyasema hayo leo tarehe 23 Februari, 2026 wakati wa Mkutano wa Utekelezaji wa Mikakati na Hatua zinazochukuliwa na Wadau Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika kwenye ukumbi wa Mkutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
“Natambua na kuthamini mchango wa kila mmoja,” amesema Jaji Mkuu huku akiwataka Wadau hao kila mmoja kwa nafasi yake kuifanyia kazi mikakati waliokubaliana katika mkutano huo.
Kadhalika, Mhe. Masaju amewasisitiza Wadau wa Mahakama kuendelea kudumisha Utawala wa Sheria, huku akitoa angalizo kwamba bila kufanya hivyo migogoro itazidi kushamiri katika jamii.
Mhe. Masaju ameeleza kuwa, Mahakama inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha huduma ya utoaji haki inatolewa mapema ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua ya kugatua huduma za Mahakama ya Rufani katika mikoa mbalimbali huku akitaja kuwa kwa kuanzia itakuwa Dar es Salaam, Arusha na baadhi ya Mikoa mingine.
“Mpango wa kugatua Mahakama ya Rufani bado upo palepale na unaendelea vizuri, matarajio yaliyopo ni kwamba usikilizaji wa mashauri utaongezeka baada ya ugatuzi wa Mahakama ya Rufani,” ameeleza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Masaju amesema kwamba, katika kuhakikisha kuwa Mahakama inaendelea kutoka haki mapema ipasavyo kama ambavyo Dira yake inataka, mashauri yaliyobaki katika zoezi la usikilizwaji wa mashauri ya biashara, kodi, ushindani wa biashara yatapangwa kusikilizwa katika vikao vijavyo.
Jaji Mkuu ameongeza kuwa, Mahakama imepanga pia kuyapa kipaumbele kwa kuyasikiliza mashauri ya ardhi katikati ya mwezi Machi mwaka huu.
Akizungumzia kuhusu Wadau wa Mahakama, Jaji Mkuu ameipongeza Benki ya Tanzania kwa kuandaa Waraka unaotoa mwongozo kwa Taasisi za Kibenki. Vilevile amewataka Madalali wa Mahakama kuwa na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mhe. Masaju ameongeza pia kwa kukemea tabia ya baadhi ya Mawakili wa Serikali na wa Kujitegemea kuahirisha mashauri kwa visingizio mbalimbali, na kwamba Mahakama haitavumilia vitendo ambavyo vinalenga kurudisha nyuma jitihada za kuhakikisha haki inatolewa kwa wananchi mapema ipasavyo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Uondoshaji wa Mashauri yanayohusu biashara, uchumi na kodi uliofanyika kuanzia tarehe 03 Novemba, 2025 hadi tarehe 15 Desemba, 2025, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya amesema mkakati huyo umekuwa wa mafanikio makubwa.
“Tuliweza kumaliza mashauri 2,973, sawa na zaidi ya asilimia 93 ya mashauri tuliyokuwa tumepanga kuyasikiliza. Hili ni jambo la kujivunia kwa Mahakama na Wadau wote walioshiriki,” amesema Mhe. Nkya.
Msajili Mkuu ameeleza kuwa, usikilizaji wa mashauri ulifanyika kupitia vikao maalum pamoja na utaratibu wa kawaida wa Mahakama na kwamba kutokana na baadhi ya mashauri kumalizika mapema, Mahakama ilipata fursa ya kuongeza mashauri mengine 1,068, yakiwemo 256 yaliyohusu masuala ya hifadhi ya jamii na kufanya jumla ya mashauri yaliyosikilizwa kufikia 3,196.
Ameongeza kwamba, thamani ya fedha iliyohusika katika mashauri yaliyomalizika ilifikia shilingi trilioni 13.1, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya kile kilichokuwepo awali.
Katika kuimarisha utatuzi wa migogoro, Msajili Mkuu ameeleza kuwa Mahakama pia ilitumia njia ya usuluhishi ambapo mashauri 18 yalimalizika kupitia utaratibu huo, huku mashauri 25 yakiombwa na Wadaawa kupelekwa kwenye usuluhishi nje ya Mahakama.
Kadhalika, Mhe. Nkya amesema kuwa, vikao maalum vya Wadau vimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mlundikano wa mashauri, ambapo hadi kufikia mwisho wa mwaka 2025, mashauri yaliyokuwa yamelundikana yalikuwa asilimia tano ya mashauri yote.
Katika Mkutano huo Wadau mbalimbali wa Mahakama waliohudhuria wamepata fursa ya kuwasilisha kwa kueleza kuhusu utekelezaji wa uondoshaji wa mashauri hayo katika Ofisi zao, ambapo kwa ujumla wao wamepongeza jitihada zilizofanywa na Mahakama nchini kufuatia uondoshaji wa mashauri hayo ambayo yameachilia Shilingi cha Kitanzania Trilioni 13.1 na kusema kwamba zitachangia kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Blandina Kilama ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.
Wadau wengine waliyowasilisha taarifa za utekelezaji wa mikakati ya uondoshaji wa mashauri hayo ni pamoja na Baraza la Ushindani, Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Chama cha Madalali wa Mahakama Tanzania na wengine.
Mkutano huo wa Wadau uliofanyika leo ni mwendelezo wa kikao kilichofanyika tarehe 08 Oktoba, 2025, ambapo pamoja na mambo mengine Wadau hao pamoja na Mahakama walikubaliana kukutana mara nne kwa mwaka ili kufuatilia utekelezaji wa mikakati waliyojiwekea.
Mikakati waliokubaliana katika kikao kilichofanyika leo ni pamoja na Ushirikiano unaotolewa katika usikilizwaji wa mashauri ya ardhi, biashara, mabenki na ushindani wa kibiashara utolewe pia katika utekelezaji (execution) wa hukumu.
Mahakama na wadau wa mnyororo wa haki waimarishe mawasiliano na mahusiano miongoni mwao, kwa lengo la kuchukua hatua za haraka pale changamoto zinazoathiri upatikanaji haki mapema zinapojitokeza.
Wadau wa mnyororo wa haki wapatiwe elimu kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazoratibu uendeshaji wa mashauri ya ardhi, biashara, ushindani wa kibiashara, kodi na mabenki na uwekezaji ili kupata uelewa wa pamoja.
Kila taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa haki Mahakamani iwajibike ipasavyo kutekeleza jukumu lake kwa kuzingatia Katiba, sheria na maadili ya utumishi wa taasisi husika.
Mkakati mwingine ni Wadau wote wa Mahakama wenye mashauri mbele ya Mahakama wanapaswa kuhudhuria na kuyaendesha mashauri yao kikamilifu ili kuwezesha upatikanaji wa haki mapema ipasavyo.
Mwingine ni kila taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa haki iimarishe ufuatiliaji wa mashauri na uwajibikaji kwa kutoa taarifa sahihi na za mara kwa mara kuhusu utekelezaji wa mikakati tuliojiwekea na kutumia mifumo inayosomana ili kuimarisha mawasiliano na mahusiano.
Aidha, Mkakati mwingine ni kila taasisi ambayo ni mdau wa mnyororo wa haki Mahakamani iweke utaratibu mahususi wa ndani ya taasisi utakaofanikisha utekelezaji wa mikakati tunayojiwekea na kadhalika.
Wadau waliohudhuria katika Mkutano huo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha, Benki Kuu, Tume ya Mipango, Baraza la Ushindani, Baraza la Rufani la Kodi, Umoja wa Mabenki, Chemba ya Taifa ya Biashara, Mamlaka ya Uwekezaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi, Chama cha Wanasheria Tanganyika, pamoja na Wadau wengine wanaohusika na masuala ya kiuchumi na biashara.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro , na Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani (FCT), Mhe. Rose Ebrahim akiwasilisha taarifa ya namna walivyoshughulikia mashauri ya biashara, kodi wakati wa Mkutano wa Utekelezaji wa Mikakati na Hatua zinazochukuliwa na Wadau Kushughulikia Mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki na Ushindani wa Kibiashara uliofanyika leo tarehe 23 Februari, 2026 kwenye ukumbi wa Mkutano wa Jaji Mkuu Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo akiwasilisha taarifa ya namna ofisi hiyo ilivyoshughulikia mashauri ya Kodi, Biashara, Mabenki na Ushindani wa Kibiashara katika mkutano uliofanyika




















Hakuna maoni:
Chapisha Maoni