- Zaidi ya asilimia 93 ya mashauri yaliyopangwa yamalizwa
- Yarejesha kwenye mzunguko wa fedha trioni 13 kwa muda mfupi
Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dodoma
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya,
leo tarehe 23 Februari, 2026, amekutana na Waandishi wa Habari katika Makao
Makuu ya Mahakama jijini Dodoma na kuelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana,
ikiwemo kumaliza mashauri ya kimkakati yanayohusu biashara, uchumi na kodi yenye
thamani ya Shilingi za Kitanzania Trioni 13.1 katika kipindi kifupi.
Mhe. Nkya amebainisha kuwa mashauri hayo 2,973 yalisikilizwa
katika ngazi mbalimbali za Mahakama kuanzia tarehe 3 Novemba hadi 15 Desemba, 2025.
Amekumbusha kuwa Oktoba 8, 2025, Mahakama iliitisha kikao maalum cha wadau wa
masuala ya biashara na uchumi kwa lengo la kuweka mikakati ya kusikiliza
mashauri 2,128 ya kiuchumi yaliyokuwa tayari kwa usikilizaji katika ngazi
mbalimbali za mahakama.
Kwa mujibu wa Msajili Mkuu, wakati huo Mahakama ya Rufani
ilikuwa na mashauri 405, Mahakama Kuu mashauri 1,673, Mahakama za Hakimu Mkazi
mashauri 17 na Mahakama za Wilaya mashauri 33. Jumla ya mashauri hayo yalikuwa
yameshikilia kiasi cha shilingi trilioni 4.4 za kitanzania.
Amefafanua kuwa usikilizaji wa mashauri hayo ulianza Novemba
3 hadi Desemba 15, 2025, kupitia vikao maalum pamoja na utaratibu wa kawaida wa
Mahakama. Kutokana na baadhi ya mashauri kumalizika mapema, Mahakama ilipata
fursa ya kuongeza mashauri mengine 1,068, yakiwemo 256 yaliyohusu masuala ya
hifadhi ya jamii na kufanya jumla ya mashauri yaliyosikilizwa kufikia 3,196.
“Tuliweza kumaliza mashauri 2,973, sawa na zaidi ya asilimia
93 ya mashauri tuliyokuwa tumepanga kuyasikiliza. Hili ni jambo la kujivunia
kwa Mahakama na Wadau wote walioshiriki,” amesema Mhe. Nkya.
Alieleza kuwa thamani ya fedha iliyohusika katika mashauri
yaliyomalizika ilifikia shilingi trilioni 13.1, kiwango ambacho ni kikubwa
zaidi ya kile kilichokuwepo awali. Mafanikio hayo, yanaendana na kaulimbiu ya
Siku ya Sheria ya mwaka 2026 iliyosisitiza mchango wa Mahakama katika ustawi wa
jamii na maendeleo ya nchi.
Katika kuimarisha utatuzi wa migogoro, Msajili Mkuu ameeleza
kuwa Mahakama pia ilitumia njia ya usuluhishi ambapo mashauri 18 yalimalizika
kupitia utaratibu huo, huku mashauri 25 yakiombwa na Wadaawa kupelekwa kwenye
usuluhishi nje ya Mahakama.
Mhe. Nkya alibainisha kuwa vikao maalum vya Wadau
vimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mlundikano wa mashauri, ambapo hadi
kufikia mwisho wa mwaka 2025, mashauri yaliyokuwa yamelundikana yalikuwa
asilimia tano ya mashauri yote. Aidha, amesema kuwa wastani wa muda wa
usikilizaji ulipungua kutoka siku 96 hadi 30 katika Mahakama za Mwanzo, ambazo
hushughulikia zaidi ya asilimia 70 ya mashauri yote.
Alieleza kuwa vikao hivyo hushirikisha Taasisi mbalimbali za
kiserikali na binafsi zikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya
Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha, Benki Kuu, Tume ya Mipango, Baraza la
Ushindani, Baraza la Rufani la Kodi, Umoja wa Mabenki, Chemba ya Taifa ya
Biashara, Mamlaka ya Uwekezaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi, Chama cha
Wanasheria Tanganyika, pamoja na Wadau wengine wanaohusika na masuala ya
kiuchumi na biashara.
Msajili Mkuu ameeleza kuwa mkutano wa leo wa Wadau hao ni
mwendelezo wa kikao kilichofanyika tarehe 8 Oktoba, 2025, ambapo walikubaliana
kukutana mara nne kwa mwaka ili kufuatilia utekelezaji wa mikakati
waliyojiwekea.
Aliongeza kuwa mbali na mashauri ya kiuchumi na biashara,
Mahakama pia inaendelea kufanya tathmini ya mashauri ya haki jinai, na kikao
kingine cha Wadau wa sekta hiyo kinatarajiwa kufanyika ili kupima mafanikio ya
mikakati iliyowekwa awali.
Kwa ujumla, Mahakama imeonesha dhamira ya kuendelea
kuboresha utoaji haki kwa wakati, kupunguza gharama kwa Wadaawa na kuimarisha
mchango wake katika kukuza uchumi na maendeleo ya Taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni