Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Sehemu ya Watumishi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, pamoja na Mfuko wa Fidia kwa
Wafanyakazi (WCF), wanakutana mjini Kibaha kuandaa taarifa ya kitaalaam ya
mafunzo awamu ya kwanza kuhusu fidia kwa Wafanyakazi yaliyofanyika nchi nzima
kwa nyakati tofauti.
Mafunzo hayo yalifanyika mfululizo
Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia Bagamoyo tarehe 09-10 Juni 2023, Mwanza
tarehe 15-16 Agosti 2023, Arusha tarehe 01-02 Desemba 2023, Songea tarehe 09-12
Februari 2024, Kigoma tarehe 19-20 April 2024, Zanzibar tarehe 19-20 Julai 2024
na Arusha tarehe 07-08 Oktoba 2024.
Akizungumza wakati
anafungua kikao kazi hicho cha siku nne leo tarehe 23 Februari, 2026, Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, amesema
kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu ya kuongeza uelewa miongoni mwa Majaji, Naibu
Wasajili, Wasuluhishi, Waamuzi, Watendaji wa Mahakama na Maofisa wengine wa
Mahakama nchi nzima, kuhusu namna bora ya kushughulikia masuala ya fidia kwa
wafanyakazi kwa mujibu wa sheria.
Huku akinukuu Wanazuoni
mbalimbali, Jaji Mfawidhi amebainisha kuwa kukusanya elimu na kuiweka katika
mfumo wa compendium si jambo la kawaida, bali ni jukumu la kitaaluma na la hali
ya juu na kwamba ni mahali pa kupata taarifa kuhakikisha kuwa Hakimu, Mwanasheria,
au mtoa huduma hafanyi kazi kwa njia ya makisio, bali ana rejea thabiti.
Miongoni mwa Wanazuoni
hao ni James Boswell katika kitabu cha The Life of Samuel Johnson, Oxford
World’s Classics, Ukurasa wa 1071, Blaise Pascal katika Kitabu cha The
Provincial Letters, letter 16 na Francis Bacon aliandika katika kitabu cha The
Essays of Counsel, Civil and Moral Studies Uk. 50.
‘Naamini itatumika kama
rejea mahakamani, kwenye shughuli za WCF na Wizara kwa ajili ya mabadiliko ya
sera na sheria, Vyuo na Vyuo Vikuu mbalimbali, Shule ya Sheria, Kikanda ikiwa
ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na sehemu mbalimbali Duniani
kama chachu ya mabadiliko ya sheria,’ Mhe. Dkt. Mlyambina amesema.
Jaji Mfawidhi amebainisha
kuwa kuwa juhudi hii ya kuandaa compendium ni sehemu ya kuwapa silaha watumishi
wa sheria, wakiwemo Majaji, Manaibu Wasajili, Wasuluhishi, Waamuzi na Watendaji
ili waweze kubadilisha dunia ya kazi na kutoa haki kwa ufanisi zaidi kwa
wafanyakazi wanaopata madhira au magonjwa wakiwa kazini.
Amemnukuu Rais wa Afrika
Kusini na Mshindi wa Tuzo ya Nobel, kwa sasa Marehemu Nelson Mandela kama alivusema:
'Education is the most powerful weapon which you can use to change the world.'
(Elimu ni silaha kali unayoweza kuitumia kubadilisha dunia).
Mhe. Dkt. Mlyambina
amewakumbusha maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliyeasisi
umuhimu wa kuandika vitabu kwa ajili ya uhifadhi wa ukweli. Mwalimu alisema:
'What is written is permanent; it can be referred to, ‘akimaanisha kuwa; ‘Kilichoandikwa
ni cha kudumu; kinaweza kurejelewa).
‘Kupitia compendium hii,
tunajenga uhakika kwamba mafunzo yetu ya fidia hayatapotea kwenye mawazo ya
muda mfupi, bali yatakuwa kumbukumbu ya kudumu itakayowalinda wafanyakazi na
kuongoza watoa haki kwa miaka ijayo,’ amesema.
Ameendelea kumnukuu Mwalimu
Nyerere alipokuwa anaelezea kwa nini aliamua kukusanya na kuichapisha hotuba
zake za awali (1952–1965) aliwahi kusema katika kitabu chake cha Freedom and
Unity: katika utangulizi (Preface), toleo la Oxford University Press (1966),
ukurasa wa xvii.
Mwalimu alisema, "I
have put these speeches together... primarily because I want to leave a record
of the growth of our nationalist movement... We must write our own history. If
we don't, others will write it for us..."
Kwa tafsiri isiyo rasmi
ni; ‘Nimekusanya hotuba hizi... hasa kwa sababu nataka kuacha rekodi ya ukuaji
wa harakati zetu za kitaifa... Tunapaswa kuandika historia yetu wenyewe. Kama
hatutaandika, wengine wataandika kwa ajili yetu...’
‘Kwa msingi huo, kikao
hiki kinabeba umuhimu mkubwa katika kuunganisha fikra, uzoefu na ushahidi wa
wahanga walioshiriki katika vikao kazi, ili tuweze kuandaa rejea ya kitaalamu
yenye ubora, inayostahili hadhi ya Mahakama na WCF kama Taasisi tegemeo katika
utoaji wa haki na ustawi wa wafanyakazi nchini,’ Jaji Mfawidhi amesema.
Ameeleza kuwa compendium
hiyo itaweka vema kumbukumbu juu ya yote yaliyojiri kabla ya mafunzo (msimamo
wa sheria kufika Juni 09-10, 2023), wakati wa mafunzo (mapendekezo ya washiriki
ama maamuzi ya kesi mbalimbali yaliyopelekea mabadiliko ya sheria ama kanuni
wakati mafunzo yanaendelea) na nini wanapendekeza.
Mhe. Dkt. Mlyambina, kwa
niaba ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, ametoa shukrani za dhati kwa WCF kwa
ufadhili na ushirikiano thabiti uliowezesha kufanyika kwa mafunzo hayo na sasa
kikao hiki cha kuandaa compendium.
Amesema kuwa wataanza na
compendium ya Kingereza kisha kuaitafsiri kwa Kiswahili kama alivyoagiza Jaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania wakati anafungua Kikao Kazi kati ya Majaji wa Mahakama
ya Rufani na Mfuko wa Fidia uliofanyika jijini Arusha ili Watanzania wote
waweze kufaidika nayo.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni