Jumatano, 4 Februari 2026

MAHAKAMA IWE KIMBILIO LA WANYONGE NA NGAO YA HAKI; JAJI MAHIMBALI

Na SETH KAZIMOTO, Mahakama -Arusha

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha na Mgeni Rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa Kanda hiyo, Mhe. Frank Mahimbali amesema kuwa lazima Mahakama iwe thabiti na imara kiasi cha kuaminiwa na wananchi na hatimaye kuwa kimbilio la wanyonge.

Jaji Mahimbali aliyasema hayo tarehe 02 Februari, 2026 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

“Tuendelee kuimarisha Mahakama zetu ili ziwe chombo cha kuaminika, kuheshimika, chenye uadilifu na mchango wa moja kwa moja katika ustawi wa Taifa letu” aliongeza Jaji Mahimbali.

Jaji Mfawidhi aliwakumbusha Viongozi wa Serikali wanaohusika na utekelezaji wa amri za Mahakama kuhakikisha wanatekeleza amri hizo bila kuweka vikwazo ili kuwapatia haki wananchi husika mapema ipasavyo na hatimae kuharakisha maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla.

Mhe. Mahimbali aliahidi kuwa, hatakuwa na uvumilivu kwa Kiongozi yeyote ndani ya Kanda ya Arusha atakayedharau amri za Mahakama na kushindwa kuzifanyia utekezaji wakati ni wajibu wake kufanya hivyo.

Maadhimisho hayo yaliyokuwa na Kaulimbiu isemayo, ‘Mchango wa Mahakama katika Ustawi wa Maendeleo ya Taifa,’ Jaji Mahimbali aliongeza kuwa, mchango wa Mahakama katika maendeleo ya Taifa ni wa msingi na wa kudumu kwani Mahakama ni nguzo ya haki, demokrasia na utawala bora pia ni chombo kinacholinda amani, kukuza uchumi na kulinda haki za kiraia hivyo, alisisitiza kwamba, ni muhimu kwa Mahakama nchini kuwa taa ya mwanga katika giza la dhuluma.

Akizungumzia kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Jaji Mahimbali alisema kuwa,Mahakama ni nguzo muhimu kwa kuhakikisha kuwa upo utawala wa sheria, haki na uwajibikaji ambavyo ni msingi wa uchumi imara, amani ya kijamii na maendeleo jumuishi na kwamba bila Mahakama huru, inayoheshimika na yenye ufanisi, malengo ya Dira ya Maendeleo hayawezi kufikiwa.

Katika hotuba ya Mwanasheria wa Serikali mkoani Arusha, Bi. Veritas Mlay alisema kuwa Siku ya Sheria nchini ni siku muhimu na ya kipekee ya kufanya tafakuri ya kitaifa ambapo wanakumbushwa dhima na wajibu wao wa pamoja katika kulinda haki, amani, usawa na utawala wa sheria kama nguzo na nyenzo katika kufikia ustawi na maendeleo ya Taifa.

Mwanasheria huyo wa Serikali aliongeza kuwa, Tanzania imejikita katika kufanya maendeleo yanayodhihirishwa na uwepo wa miradi mikubwa ambayo imekamilika na ile ambayo ipo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji katika Sekta mbalimbali ikiwemo uchumi, ujenzi, nishati, madini na huduma za jamii.

Bi. Mlay alisisitiza kuwa, uwepo wa miradi hiyo ya maendeleo ni ushahidi tosha wa ushirikiano baina ya Serikali, Mahakama na Bunge, na kwamba Serikali imeweka mazingira rafiki na ya kuvutia uwekezaji na hivyo kukuza uchumi na maendeleo ya nchi kupitia uingizaji wa mitaji na teknolojia na upatikanaji wa ajira. 

Kadhalika Mwanasheria huyo alisema kuwa, Mahakama kama mlinzi wa Katiba, haki na utawala wa sheria, ni nguzo muhimu katika kukuza na kuendeleza ustawi na maendeleo ya Taifa.

“Mahakama iliyo huru na inayoheshimika na kuaminika huhakikisha utekelezaji thabiti wa mikataba, ulindaji wa haki za mali na kudhibiti matendo ya matumizi mabaya ya madaraka na hatimaye kukuza imani ya wawekezaji na hivyo kuwezesha ukuaji imara na endelevu wa uchumi wa Taifa,” alisema Bi. Mlay.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Hamisi Mkindi alisema kuwa, Kaulimbiu ya Siku ya Sheria mwaka huu inaakisi ukweli kwamba hakuna maendeleo ya kweli bila ulinzi wa haki, utawala wa sheria na utawala bora hivyo Mahakama ndicho chombo pekee ambacho huamua mwelekeo wa haki, uaminifu na utulivu wa kitaifa.

“Taifa linapokuwa na mfumo wa utoaji haki unaoaminika, unaofanya kazi kwa ufanisi na unaoweka mbele maslahi ya wananchi bila upendeleo, dhuluma wala hiyana na kuleta hali ya watu kuwa na matumaini, basi ustawi wa kiuchumi, kijamii na kisiasa huimarika na maendeleo ya kweli huonekana,” alisisitiza Wakili Mkindi.

Aliongeza kuwa, ni wajibu wa Mahakama kulinda na kusimamia haki za binadamu na kwamba jukumu hilo si la Mahakama pekee bali ni pamoja na Wadau wote wa Mahakama ambao ni Wadau wa haki. Alisema kwamba, haki inapaswa kutolewa bila ubaguzi kama ilivyoainishwa na Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania toleo la 1977.

Naye mgeni maalum wa Maadhimisho hayo mkoani Arusha ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makalla alisisitiza kuwa ipo haja kwa Wadau wa Sheria kutoa elimu kwa wananchi juu ya majukumu ya Mihimili ya Serikali ili wajue ni aina gani ya lalamiko au huduma inatakiwa kuwasilishwa kwenye Mhimili gani ili suala hilo liweze kupatiwa ufumbuzi.

Vilevile, Mhe. Makalla aliwaasa Mawakili wa Kujitegemea kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu ambavyo vinaleta migogoro na usumbufu kwa wananchi.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa wa Arusha ameahidi kutoa ushirikiano kwa wadau wote wa haki, hususani katika kuhakikisha amri za Mahakama zinaheshimika na kutekelezwa kama taratibu zinavyoelekeza.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yahudhuriwa na Viongozi wa Taasisi mbalimbali mkoani Arusha zikiwemo vyombo vya Ulinzi na Usalama, Vyuo, Shule, TAKUKURU, Vyama vya Kiraia, Viongozi wa Dini na Sekta Binafsi.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali akizungumza na Watumishi, Wadau na Wananchi waliohudhuria katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha akikagua gwaride maalum kuashiria uzinduzi wa mwaka mpya wa Mahakama wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo kwa upande wa Arusha yalifanyika katika viwanja vya  Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 02 Februari, 2026.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mgeni Maalum wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini mkoani humo, Mhe. CPA Amos Makalla akiwasalimia Wadau wa Sheria na wananchi waliohudhuria kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) mkoani Arusha, Wakili Msomi Hamisi Mkindi akisoma hotuba ya Chama hicho wakati wa sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini zilizofanyika tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha.

Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Arusha, Bi. Veritas Mlay akisoma hotuba ya Ofisi ya MwanAsheria Mkuu wa Serikali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 02 Februari, 2026.




Wadau na wananchi waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 02 Februari, 2026.

Naibu Wasajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mhe. Amir Msumi na Mhe. Elia Mrema wakishiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha tarehe 02 Februari, 2026.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama  Kuu ya  Tanzania Kanda ya Arusha, Mhe. Frank Mahimbali (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu Arusha (walioketi) pamoja na Majaji wastaafu (waliosimama) wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika tarehe 02 Februari, 2026 katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Arusha. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla.






Picha za pamoja za makundi mbalimbali ya washiriki waliohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini kwa upande wa Arusha.

(Habari hii imehaririwa na MARY GWERA, Mahakama-Dodoma)

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni