Jumatano, 4 Februari 2026

HAKI MSINGI MKUU WA USTAWI WA MAENDELEO YA TAIFA; JAJI MFAWIDHI MTWARA

Na OBADIA KAWONGA-Mahakama, Mtwara

Utawala bora na unaozingatia sheria ni msingi wa haki wa kufikia ustawi wa maendeleo ya Taifa, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki, amesema.

Akizungumza kwenye Maadhimsho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika kikanda tarehe 2 Februari, 2026 katika Viwanja vya Mahakama Kuu Mtwara, Mhe. Kakolaki alisema kuwa Mahakama kwa kushirikiana na Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha utoaji haki kwa wakati kwa Taasisi, mashirika na jamii kwa ujumla.

'Utawala bora na wa sheria unazingatia misingi ya haki na ndio msingi mkuu wa kufikia ustawi wa maendeleo ya Taifa.' aliongezea Mhe. Edwin Kakolaki.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, alihimiza utoaji haki kwa wananchi mapema ipasavyo ili kudumisha amani na utulivu katika Mkoa na Taifa kwa ujumla.

'Nchi yenye amani na utulivu inakaribisha wawekezaji kwa kuwa hawana mashaka ya kupoteza mali zao. Wito wangu tuendelee kuitunza amani yetu,' alisema.

Aidha, Mhe. Sawala alitoa rai kwa wadau wote wa haki jinai na madai kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu ili kuisaidia Mahakama kustawisha maendeleo ya Taifa kupitia utoaji haki bila ucheleweshaji.

Naye Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mtwara, Bi. Nunu Mangu, alibainisha kuwa Mahakama inalinda amani katika jamii na kuzuia wananchi kuangukia kwenye kutafuta haki kwa njia zisizo rasmi.

'Nchi imeshuhudia mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa utoaji haki ikiwemo ongezeko la Majaji na Mahakimu, matumizi ya mifumo ya kisasa pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kazi,' Bi. Mangu alisema.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, wadau wa sekta ya Sheria: Wakili wa Serikali wa Kujitegemea, Mahakimu kutoka Wilaya ya Mkoa wa Mtwara, Viongozi wa Dini, Wanafunzi wa Vyuo mbalimbali pamoja na Wananchi kwa ujumla.

Kabla ya kuhitimisha Maadhimisho hayo kulikuwepo na gwaride maalum lilioandaliwa na Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Mtwara ambalo lilikagua na Jaji Mfawidhi kuashiria mwanzo wa shughuli za kimahakama kwa mwaka 2026.

Sambamba na maadhimisho hayo, kulikuwepo na burudani mbalimbali zilizotolewa na wachezaji wa ngoma za asili pamoja na Kwaya ya Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu, ambao waliweza kufurahisha na kuburudisha nyoyo za waliohudhuria kwa uchezaji mzuri na ujumbe ulioakisi Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo.

Baada ya Maadhimisho hayo, kulifanyika bonanza katika Viwanja vya Nangwanda lililoongozwa na Jaji Mfawidhi ambaye alishiriki kikamilifu katika mazoezi na michezo mbalimbali pamoja na watumishi wa Mahakama.

Akizungumza wakati wa bonanza hilo, Mhe. Kakolaki alisisitiza umuhimu wa michezo na mazoezi kwa watumishi wa Mahakama, akisisitiza kuwa shughuli hizo zinaleta afya imara na kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

'Mtumishi mwenye afya njema ni rasilimali muhimu kwa Taifa. Tunapofanya mazoezi tunajenga miili yetu na akili zetu, na hivyo tunakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma bora kwa wananchi,' alisema Mhe. Kakolaki.

Bonanza hiyo iliyojaa shangwe na furaha ilihusisha michezo mbalimbali ikiwemo mbio, kuvuta kamba, mpira wa miguu pamoja na wa kikapu. Watumishi Pamoja na wadau mbalimbali walishiriki kwa hamasa kubwa huku wakiimarisha udugu na ushirikiano miongoni mwao.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki, akikagua gwaride.

Wadau pamoja na wananchi katika maandamano kuelekea viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Seraphine Nsana, akitoa utambulisho wa Viongozi pamoja na kukaribisha wageni.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Sheria mkoani Mtwara.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Kanali Patrick Sawala, akitoa salamu katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.

Wachezaji wa ngoma za asili wakitoa burudani kwa wageni waalikwa wa hafla hiyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (katikati), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Saidi Ding’ohi (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Martha Mpaze (kulia), Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Partick Sawala (w apili kushoto) pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe, Abdallah Mwaipaya (kushoto) katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Edwin Kakolaki (wa tatu kushoto) katika uzinduzi wa bonanza lililoandaliwa baada ya hafla ya maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama Dodoma

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni