Jumatano, 4 Februari 2026

TEHAMA YAONDOA MLUNDIKANO WA MASHAURI MAHAKAMANI GEITA

Na DOTTO MKAJA-Mahakama, Geita

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameiwezesha Mahakama Kuu Kanda ya Geita kuondoa mlundikano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama kwa mwaka 2025.

Hayo yamebainishwa jana Februari 2, 2026 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, wakati akitoa hotuba yake katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini yaliyofanyika katika Uwanja wa Kituo Jumuishi Geita (Jengo Jipya).

Mhe. Mhina alisema Mahakama ni chombo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kulinda amani ya wananchi, akibainisha kuwa bila uwepo wa Mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama, Magereza na Serikali, hata siku moja haviwezi kupita bila kutokea uvunjifu mkubwa wa amani.

Akizungumza kuhusu utendaji wa Mahakama Kanda ya Geita, alisema kuwa kwa mwaka 2025 Mahakama zote zilifanikiwa kumaliza mashauri kwa wakati, huku wastani wa umalizaji wa mashauri katika Mahakama za Wilaya tano ukiwa siku 35.

Aliongeza kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita ilikuwa na wastani wa siku 60, Mahakama Kuu siku 46 na Mahakama za Mwanzo siku 15. Alisema kuwa wastani wa muda wa usikilizaji mashauri kwa mwaka 2025 umepanda kulinganisha na mwaka 2024.

Akifafanua mafanikio hayo, alisema yameleta ongezeko la ufanisi katika usikilizwaji wa mashauri, kupungua kwa muda wa mashauri kusikilizwa na kuamuliwa, pamoja na kuondolewa kabisa kwa mlundikano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama Kanda ya Geita.

Aidha, alisema Mahakama ilisikiliza na kumaliza mashauri yote ya kimkakati yaliyokuwa yameshikilia uchumi, hali iliyosababisha fedha zilizokuwa zimezuiwa kurejeshwa katika mzunguko wa uchumi na kuhamasisha uwekezaji.

Mhe. Mhina alisema mafanikio hayo yametokana na matumizi ya TEHAMA, akieleza kuwa teknolojia hiyo imeongeza uwazi kwa wadau wa haki na kuimarisha ushirikiano kati ya Taasisi mbalimbali kupitia mifumo inayosomana, ikiwemo NIDA, RITA, Magereza na taasisi nyingine.

Aliwasihi wadau wa sheria kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, weledi na ushirikiano.

Kwa upande wake, Mgeni Mwalikwa katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigela, aliipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Geita kwa kumaliza mashauri kwa wakati na kwa haki, akisema hali hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko kutoka kwa wananchi.

“Sipokei malalamiko kutoka mahakamani, jambo linaloonesha kuwa haki inatendeka kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji,” alisema Mhe. Shigela.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Geita, Mhe. Kevin Mhina, akitoa hutuba Siku ya Sheria katika uwanja wa Mahakama Kuu Geita (Jengo Jipya).

Mchungaji kutokKanisa la KKKT akitoa maombi ya kufungua Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika katika Uwanja wa Kituo Jumuishi Geita (IJC - Geita).

Meza kuu katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria iliyofanyika katika kituo Jumuishi Geita (IJC – Geita).

Mahakimu wakikiwa katika picha ya pamoja Siku ya Sheria nchini katika uwanja wa Kituo Jumuishi Geita(IJC - Geita).

Maofisa kutoka ofisi ya Mwendasha Mashitaka wakiwa katika picha ya pamoja.

Mawakili wa Kujitegemea wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu kwenye Maadhimisho ya Siku ya Sheria.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina, akikagua gwalide Siku ya Sheria katika uwanja wa kituo Jumuishi Geita.

 

Watumishi wanawake Mahakama Kuu Geita na Mahakama ya Wilaya Geita katika picha ya pamoja wakiadhisha Siku ya Sheria 2026 katika Kituo Jumuishi Geita.

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni