- Malengo yote ya Mradi wa Maboresho wa Mahakama yamefikiwa kwa asilimia 100
Na JAMES BUSANYA-Mahakama, Dodoma
Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha utendaji na
upatikanaji wa huduma za haki kwa wananchi, ikifikia kiwango cha juu katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Mahakama katika mageuzi ya kisheria.
Hayo yamesemwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
na Mkuu wa Kitengo cha Maboresho (JDU), Mhe. Dkt. Angelo Rumisha, tarehe 25
Februari, 2026 Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma, wakati
anawasilisha taarifa ya maboresho kwenye Kikao cha Mwaka cha Majaji Wfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mhe. Dkt. Rumisha alieleza kuwa malengo yote 12 ya maendeleo ya
mradi (PDO) yamefikiwa au
kuzidi matarajio, huku kiwango cha kuridhika kwa wananchi kikiongezeka kwa asilimia
kubwa, ukilinganisha na awali, jambo ambalo ni ishara kubwa ya mafanikio katika kuboresha ufanisi, uwazi na upatikanaji wa haki katika
ngazi zote za Mahakama nchini.
Katika kuimarisha miundombinu na upatikanaji wa huduma, Jaji Rumisha alieleza kuwa Mradi wa Maboresho ya Mahakama umejikita katika kuunda miundombinu
ya kisasa kwa kujenga Mahakama za Mwanzo 94 na Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) 18.
“Hatua hizi zimeleta mapinduzi makubwa
kwa wananchi, kwani sasa huduma za kisheria zinapatikana karibu na maeneo yao,
kupunguza vikwazo vya kijiografia na gharama kubwa za usafiri ambazo zilikuwa
changamoto kubwa kabla ya mwaka 2015,” alisema.
Mhe. Dkt.
Rumisha alibainisha kuwa kupungua kwa muda wa mashauri na kuongeza ufanisi, mageuzi ya kimkakati, kidijitali na uboreshaji wa usimamizi wa kesi umepunguza muda wa kusubiri kupata
haki kwa kiasi kikubwa.
Alitoa mfano wa kesi za biashara, ambapo katika Mahakama Kuu kuna punguzo la asilimia 64, kesi za familia Mahakama za Mwanzo
zimepungua kutoka siku 120 hadi 35, punguzo la asilimia 71, na kesi Mahakama ya Wilaya
zimepungua kutoka siku 40 hadi 15, punguzo la asilimia 63.
“Punguzo hili limefanikiwa kutokana na
matumizi ya TEHAMA, Mahakama tembezi (Mobile Courts), upanuzi wa Mahakama na kuanzishwa kwa IJCs katika Mikoa mbalimbali. Hii imesaidia wananchi kupata haki kwa haraka,” alisema.
Mhe. Dkt.
Rumisha alieleza kuwa katika mageuzi ya kidijitali na uboreshaji wa utendaji, Mradi umejikita
pia katika mabadiliko ya kidijitali ya mfumo wa Mahakama. Alieleza kuwa
mfumo wa mapitio na tathimini ya
utendaji Maofisa wa Mahakama (JOPRAS) hutoa uchambuzi wa muda halisi wa
utendaji.
Aidha,
alisema kuwa uchapishaji
wa uamuzi mtandaoni
umeongezeka kutoka asilimia 3 hadi 88, jambo linaloongeza uwazi, uwajibikaji na
uelewa wa wananchi kuhusu mfumo wa kisheria.
Alieleza kuwa
kiwango cha kuridhika
kwa huduma za Mahakama kwa wananchi kimeongezeka kutoka asilimia 61 hadi
asilimia 88 kutokana na kupungua kwa muda wa
mashauri, hasa ya biashara na familia.
Kuhusu mlundikano wa mashauri, Mhe. Dkt. Rumisha alieleza
kuwa kesi zilizokuwa
zinasubiri zimepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2021 hadi asilimia 5 mwaka 2025, hivyo kesi zote zenye umri zaidi ya miezi 24
ni asilimia 5 pekee. Alisema kuwa punguzo hilo limefanikiwa kupitia usimamizi makini wa mtiririko wa kesi,
upanuzi wa Mahakama tembezi, na kuanzishwa kwa IJCs katika maeneo mbalimbali.
Alibainisha athari za kiuchumi na kijamii kupitia Mahakama tembezi na IJCs, ambapo gharama kwa wananchi zimepunguzwa kwa
kiasi kikubwa, jambo ambalo inawawezesha
wananchi kupata haki bila kero za kifedha, huku akiba ya Taifa ikifikia mabilioni ya shilingi.
Mhe. Dkt. Rumisha
alieleza kuwa Mahakama imeendelea kudumisha imani ya wananchi kupitia uwajibikaji
thabiti na mifumo ya maoni inayoruhusu michango ya umma na kwamba njia mbalimbali za maoni, ikiwemo sanduku la mapendekezo na maoni ya mtandaoni,
zimeimarisha uhusiano na wananchi na kuleta uwazi katika utendaji wa Mahakama.
Alihitimisha kwa kusema kwamba mageuzi hayo ya kimkakati, kidijitali na kiutawala yameonesha wazi kwamba mfumo wa Mahakama unaweza kubadilika na kuendeshwa kwa ufanisi, uwazi, uwajibikaji na upatikanaji wa haki karibu na wananchi.
Mafanikio hayo ni ishara tosha kwamba Tanzania ina
mfumo wa Mahakama wa
kisasa, unaojali wananchi, unaotumia teknolojia na mbinu za kisasa za usimamizi
wa mashauri na unaendelea kuboresha maisha ya raia kwa kuharakisha upatikanaji
wa haki, kupunguza gharama na kuongeza kuridhika kwa umma.





Hakuna maoni:
Chapisha Maoni