Na HALIMA MNETE – Mahakama, Dodoma
Mahakama ya Tanzania
imeendelea kutekeleza kwa kasi miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama katika Mikoa
na Wilaya mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha
upatikanaji wa haki kwa wananchi na kuboresha mazingira ya utoaji huduma za
kimahakama.
Hayo yalibainishwa jana
tarehe 25 Februari, 2026 na Mkurugenzi wa Uendelezaji na Matengenezo ya Majengo
wa Mahakama, Mhandisi Moses Lwiwa, wajati anawasilisha Taarifa ya Miradi ya
Majengo ya Mahakama katika Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu
kilichofanyika Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Akiwasilisha taarifa hiyo
mbele ya Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Mahakama Tanzania, Mhe. George Masaju, na Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt Mustapher Mohmed Siyani, ambaye
ni Mwenyekiti wa kikao hicho, Mhandisi Lwiwa alieleza kuwa Mahakama inaendelea
na utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Vituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJCs)
katika Mikoa mbalimbali pamoja na majengo ya Mahakama za Mwanzo na Wilaya
(SBCs), kwa lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kupunguza
changamoto za miundombinu.
Kwa upande wa miradi ya
IJCs, alibainisha kuwa miradi katika Mikoa ya Geita, Njombe, Simiyu, Songea,
Pemba, Singida, Songwe na Lindi ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji,
ambapo baadhi ya majengo tayari yamekamilika na yanafanya kazi, huku mengine
yakiwa katika kipindi cha uangalizi baada ya kukamilika (Defect Liability
Period).
Alieleza kuwa Mahakama
imeweka mkakati wa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo kwa
kushirikiana na Washauri Elekezi ili kuhakikisha mapungufu yote yanayojitokeza
yanarekebishwa kwa wakati.
“Mwelekeo wetu ni
kuhakikisha kila jengo linalokabidhiwa kwa Mahakama linakidhi viwango vya ubora
vinavyotakiwa na linaweza kutumika kikamilifu katika utoaji wa huduma za haki,”
alisisitiza.
Kwa upande wa miradi ya
SBCs, Mhandisi Lwiwa alieleza kuwa miradi mingi iliyopo katika vifurushi
mbalimbali (Packages na Lots) imekamilika kwa kiwango kikubwa na ipo kwenye
kipindi cha uangalizi. Miradi hiyo inahusisha Mahakama za Mwanzo na Wilaya
katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kigoma, Mtwara, Manyara, Katavi, Rukwa, Mbeya,
Dar es Salaam na Mikoa mingine.
Alifafanua kuwa miradi
hiyo inatekelezwa kwa awamu na kwa mikataba maalum inayosimamiwa kwa karibu na
Mahakama, kwa kushirikiana na Washauri Elekezi, ili kuhakikisha thamani ya
fedha inaonekana na majengo yanakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya watumishi
na wananchi.
Katika hatua za mbele, amesema
Mahakama imepanga kuimarisha usimamizi wa kiufundi katika miradi yote
inayoendelea, kuweka msisitizo wa uwajibikaji kwa Wakandarasi pamoja na
kuhakikisha kuwa marekebisho ya kasoro zozote zinazobainika katika kipindi cha
uangalizi yanafanyika kwa wakati.
Utekelezaji wa miradi
hiyo ya majengo unaenda sambamba na jitihada za Mahakama katika kufanya mageuzi
ya kiutawala na kidijitali, kwa lengo la kujenga Mahakama imara yenye
miundombinu ya kisasa, inayowezesha utoaji wa haki kwa ufanisi, uwazi na kwa
wakati.




Hakuna maoni:
Chapisha Maoni