Alhamisi, 26 Februari 2026

MAHAKAMA YA TANZANIA KUJENGA MAHAKAMA DIJITALI KWA KUZINGATIA DIRA YA TAIFA 2050

Na HALIMA MNETE – Mahakama, Dodoma

Uboreshaji wa kidijitali unaoendelea ndani ya Mahakama ya Tanzania unalenga siyo kuimarisha mifumo ya ndani ya Mahakama pekee, bali pia kuendana moja kwa moja na mipango na dira ya maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Hayo yalisemwa jana tarehe 25 Februari, 2026 na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA], Bw. Kalege Enock, wakati akiwasilisha taarifa ya matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri kwenye Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi kinachofanyika Makao Makuu ya Mahakama, jijini Dodoma.

Kikao hicho kinahudhuriwa na Majaji Wafawidhi wa Kanda zote za Mahakama Kuu, kikiongozwa na Jaji Kiongozi wa Mahakam Kuu ta Tanzania, Mhe. Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, kama Mwenyekiti wa kikao hicho huku Mgeni Rasmi akiwa ni Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju.

Katika taarifa yake, Bw. Kalege alieleza kuwa safari ya Mahakama kuelekea Mahakama Dijitali (Smart Court) imejengwa juu ya misingi ya kimkakati inayojumuisha Mpango Mkakati wa Mahakama, Sera ya Taifa ya TEHAMA, Mkakati wa Serikali Mtandao, pamoja na Mfumo wa Kimkakati wa Uchumi wa Kidijitali na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akisisitiza mwelekeo huo wa kitaifa, alisema: “uboreshaji wote unaofanyika mahakamani katika eneo la kidijitali tunazingatia siyo tu mipango ya Mahakama, bali pia mipango ya nchi, tukianzia na Mfumo wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Hii yote tunaitumia kama dira ya kutuongoza katika kufikia maono mapana ya nchi yetu.”

Alifafanua kuwa mageuzi hayo yanalenga kuboresha usimamizi wa mashauri, kupunguza mrundikano wa mashauri, kuongeza uwazi na uwajibikaji, pamoja na kuwezesha maamuzi yanayotegemea takwimu sahihi.

Aidha, alieleza kuwa Mahakama imeendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki ikiwemo mfumo wa usimamizi wa mashauri (e-Case Management System), huduma za Mahakama Mtandao, pamoja na matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI) katika kunakili na kutafsiri mwenendo wa mashauri kwa Kiswahili na Kiingereza, uchambuzi wa takwimu za mashauri na utafiti wa kisheria.

Kuhusu maadili na usalama wa taarifa, Bw. Kalege alisisitiza kuwa Mahakama inazingatia kikamilifu matakwa ya Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022, pamoja na kuimarisha mifumo ya usalama wa mtandao ili kulinda kumbukumbu na ushahidi wa kimahakama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho, Mhe. Dkt. Siyani alieleza umuhimu wa Viongozi wa Mahakama katika ngazi za kanda kuhakikisha mifumo hiyo inatumika ipasavyo ili kuleta matokeo chanya katika utoaji wa haki.

Naye Jaji Mkuu alisisitiza dhamira ya Mahakama kuendelea kuwa Taasisi inayoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani, akieleza kuwa katika zama hizi, utoaji wa haki unahitaji kuungwa mkono na mifumo imara ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama.

 

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA], Bw. Kalege Enock [juu na chini], akiwasilisha taarifa ya matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa mashauri kwenye Kikao cha Mwaka cha Majaji Wafawidhi Makao Makuu ya Mahakama, jijini Dodoma.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi, akichangia mada kwenye kikao hicho. Picha chini ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Joachim Tiganga.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt. Ntemi Kilekamajenga, akichangia mada kwenye kikao hicho. 

Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni