Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dodoma
Mahakama ya Tanzania
imetekeleza kwa mafanikio makubwa jukumu lake la utoaji haki nchini kwa mwaka
2025. Kiwango cha uondoshaji wa mashauri kimeongezeka kutoka asilimia 83 hadi 88 na kiwango cha umalizaji kikiongezeka kutoka asilimia 101 hadi 105.
Hayo yamebainishwa jana
tarehe 25 Februari, 2026 na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri ya Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha, wakati anawasilisha taarifa ya Utendaji wa
Mahakama kwa Mwaka 2025 kwenye Kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu
kinachofanyika jijini Dodoma.
Mhe. Kamugisha aliwaeleza
Majaji hao kuwa mashauri yaliyofunguliwa kwa mwaka 2025 yalikuwa 243,848, sawa na
ongezeko la asilimia 0.6 ya mashauri ya mwaka 2024. Mashauri hayo yanajumuisha 105,480
ya madai na 138,368 ya jinai.
Alibainisha kuwa, mashauri
yaliyofunguliwa katika Mahakama ya Rufani yalikuwa 3,214, Mahakama Kuu yalikuwa
21,518, Mahakama za Hakimu Mkazi 6,033, Mahakama za Wilaya 35,144, Mahakama za
Watoto 1,225, na Mahakama za Mwanzo 176,687, hivyo kufanya jumla ya 243,848.
‘Mashauri yaliyoamuliwa na
Mahakama ya Rufani kwa mwaka 2025 yalikuwa 4,405, Mahakama Kuu zilikuwa 22,164,
Mahakama za Hakimu Mkazi 5,967, Mahakama za Wilaya zilikuwa 40,367, Mahakama za
Watoto 1,372 na Mahakama za Mwanzo 180,518, hivyo kufanya jumla ya 254,793,’
alisema.
Kwa upande wa mashauri yanayoendelea,
Mhe. Kamugisha alieleza kuwa Mahakama ya Rufani ni 5,039, Mahakama Kuu 10,381,
Mahakama za Hakimu Mkazi 2,303, Mahakama za Wilaya 8,214, Mahakama za Watoto
202 na Mahakama za Mwanzo 7,240, hivyo kufanya jumla ya 33,379.
Aidha, alibainisha kuwa kiwango cha jumla cha umalizaji wa mashauri kwa 2025 kilikuwa asilimia 105, huku Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, ikiongoza kwa asilimia 141, wakifuatiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara kwa asilimia 111.
Kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, Mhe. Kamugisha alieleza kuwa Iringa iliongoza kwa asilimia176, wakifuatiwa na Mtwara kwa asilimia 168, huku upande wa Mahakama za Wilaya, Newala ilikuwa ya kwanza baada ya kuzoa asilimia 156, wakifuatiwa na Geita iliyopata asilimia 142.
'Kiwango cha jumla cha uondoaji wa mashauri kwa mwaka huo kilikuwa asilimia 88.4, huku Mahakama Kuu Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke kikiongoza kwa asilimia 94, wakifuatiwa na Geita iliyopata asilimia 90,' alisema.
Aliongeza kuwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, walioongoza ni Simiyu kwa asilimia 97, wakifuatiwa na Mahakama ya Watoto Temeke kwa asilimia 92, huku upande wa Mahakama za Wilaya, Kilolo iliongoza kwa asilimia 99, wakifuatiwa kwa karibu na Newala wenye asilimia 98.
Alibainisha pia mafanikio
yaliyopatikana kwa mwaka 2025 kuwa malengo
yote ya Mpango Mkakati wa Mahakama na mradi wa kupeleka huduma karibu na mwananchi
yalifikiwa kikamilifu.
Mhe. Kamugisha aliongeza
kuwa, kumekuwa na ongezeko la kiwango cha umalizaji mashauri kwa asilimia nne
kutoka asilimia 101 kwa mwaka 2024 hadi asilimia 105 kwa mwaka 2025.
Kadhalika, alisema, kumekuwa
na ongezeko la kiwango cha uondoshaji wa mashauri kwa asilimia tano kutoka
asilimia 83 kwa mwaka 2024 hadi asilimia 88 kwa mwaka 2025.
Mhe. Kamugisha alibainisha pia kuwa muda wa wastani wa kuamua mashauri ulipungua
kwa siku 12 kutoka wastani wa siku 78 kwa mwaka 2024 hadi siku 66 kwa mwaka
2025 na wastani wa mzigo wa kazi ulipungua kwa asilimia 2.6 kutoka 228 kwa mwaka
2024 hadi 222 kwa mwaka 2025.
‘Matokeo haya chanya yanaonesha utayari wa Mahakama ya Tanzania kukidhi
mahitaji yanayokuwa ya haki kwa kuongeza nguvu kazi na kutekeleza mikakati
madhubuti ya usimamizi wa mashauri, ikijumuisha mapitio ya kimkakati ya kanuni
za taratibu na matumizi makubwa ya teknolojia,’ alisema.








Hakuna maoni:
Chapisha Maoni