- Mtendaji Mkuu asema bajeti iakisi dira, kuimarisha msingi wa utoaji haki
- Asisitiza nidhamu ya matumizi, ulinzi wa Mahakama za Mwanzo
Na HALIMA MNETE-Mahakama, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel, amesema maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 yanapaswa
kwenda sambamba na mipango ya kimkakati ya Mahakama na kulenga kuimarisha
utoaji wa haki kwa ufanisi zaidi.
Prof. Ole Gabriel alisema hayo wakati anafungua kikao cha
mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya 2025/26 na uchambuzi wa maoteo ya bajeti ya
2026/27 kilichofanyika tarehe 16 Februari 2026 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya
Mahakama jijini Dodoma.
Alikumbusha kuwa Julai Mosi 2025, wakati utekelezaji wa
bajeti ya 2025/26 ulipoanza, alitoa waraka ulioelekeza masuala ya msingi ya
kuzingatia, ikiwemo kudhibiti ulimbikizaji wa madeni, kuzingatia Sheria ya
Bajeti Na. 11 ya Mwaka 2015 na kutohamisha fedha kutoka vifungu vya Mahakama za
Mwanzo na Wilaya kwenda Mahakama za juu. Alisema maelekezo hayo yalilenga
kuimarisha nidhamu ya matumizi na kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa mujibu
wa sheria.
“Kuna wakati unaweza kutamani kufanya malipo fulani, lakini
kama ni nje ya utaratibu na nje ya sheria huwezi kufanya, kwa sababu itatuletea
hoja za ukaguzi. Majukumu yetu tunapaswa kuyafanya kwa mujibu wa sheria na si
vinginevyo,” alisema, akitoa shukrani kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Fedha na
Uhasibu kwa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha Mahakama inaendelea kuwa kinara
wa Taasisi za umma zenye hati safi ya hesabu.
Alisema mafanikio hayo ni matokeo ya mipango madhubuti na
usimamizi thabiti wa fedha, akisisitiza kuwa rasilimali fedha huwa hazitoshi,
hivyo upangaji sahihi ni muhimu ili kufikia matarajio na Dira ya Mahakama.
Alieleza kuwa mapitio ya nusu mwaka yanatoa fursa ya kujitathmini kama
utekelezaji unaendana na mipango na kama Taasisi iko katika mwelekeo sahihi.
Akigusia suala la Mahakama za Mwanzo, Prof. Ole Gabriel
alisema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mashauri huanzia katika ngazi hiyo, hivyo
ni lazima zilindwe na kuimarishwa. Alibainisha kuwa katika bajeti ya sasa,
Mahakama za Mwanzo zimeongezewa fedha kwa asilimia 100 kwa makusudi maalum, na
akaelekeza fedha hizo ziende moja kwa moja katika ngazi hiyo.
“Haikuwa kwa bahati mbaya. Tulimaanisha kulinda Mahakama za
Mwanzo kwa sababu ndizo msingi wa utoaji haki kwa wananchi wengi,” alisema.
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/27, Mahakama
inapanga kuongeza uwekezaji katika ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama
za Mwanzo ili kuboresha mazingira ya utoaji haki na kuongeza imani ya wananchi.
Kuhusu rasilimali watu, alisema Mahakama imeendelea kuiomba
Serikali kuongeza watumishi kwa kuwa bila rasilimali watu ya kutosha, utoaji
haki unaweza kukwama. Alieleza kuwa tayari kibali cha ajira 642 kimepatikana na
mchakato wake umekamilika kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama, akiwashukuru
watendaji wote waliohusika katika zoezi hilo.
Aidha, aliwahimiza washiriki kutoa ushiriki wa dhati katika
maandalizi ya Mpango Mkakati wa Tatu wa Mahakama, akibainisha kuwa mafanikio ya
mpango huo yatategemea tathmini ya mafanikio na changamoto zilizojitokeza
katika mipango iliyopita na ushiriki wa pamoja katika kuweka mikakati mipya
inayopimika.
Alieleza pia umuhimu wa kuunganisha udhibiti wa vihatarishi
katika maandalizi na utekelezaji wa bajeti ili kuhakikisha mipango inayowekwa
inatekelezeka bila kuathiri malengo makuu ya Taasisi.
Prof. Ole Gabriel aliwataka wasimamizi wa bajeti katika
kanda na divisheni kuandaa bajeti zinazoakisi uhalisia wa mahitaji na kuongeza
thamani katika utoaji wa haki.
“Jiulizeni kila wakati: Shughuli hii ninayoipangia fedha
inatusaidiaje kufikia malengo yetu makuu. Tuwekeze kwenye maeneo yenye matokeo
makubwa na yanayoakisi uhalisia,” alisisitiza.
Alisema maandalizi ya bajeti ni mchakato wa kimkakati
unaobeba mustakabali wa Mahakama na kwamba uwajibikaji, ushirikiano na nidhamu
ya matumizi ni nguzo muhimu za kuendelea kuimarisha Taasisi hiyo na kulinda
imani ya wananchi.
Kwa upande wake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Eva Nkya, alisema bajeti ni nyenzo ya kimkakati inayopaswa kuakisi dira na
dhamira ya Taasisi katika utoaji wa haki.
Alisisitiza kuwa maandalizi ya bajeti ya 2026/27 yanapaswa
kuendana na maandalizi ya Mpango Mkakati wa Tatu wa Mahakama ili kuhakikisha
mipango inayowekwa inatekelezeka na inapimika.
“Haki inapaswa kutolewa kwa wakati na kwa usawa. Hilo
linahitaji mipango madhubuti na usimamizi makini wa rasilimali,” alisema.
Mhe. Nkya pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kupunguza mlundikano
wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama, pamoja na kuimarisha matumizi ya
mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano [TEHAMA] katika usimamizi wa
mashauri ili kuongeza uwazi na ufanisi.
Kikao hicho kimeweka msingi wa mchakato wa upangaji wa rasilimali kwa mwaka wa fedha 2026/27, kikionesha dhamira ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha utendaji, uwajibikaji na utoaji wa haki kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, akizungumza wakati anafungua kikao cha mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya 2025/26 na uchambuzi wa maoteo ya bajeti ya 2026/27 kilichofanyika Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni