Alhamisi, 12 Februari 2026

MTENDAJI MKUU AMETOA WITO KWA MAAFISA USAFIRIRSHAJI KUONGEZA UMAKINI WANAPOTEKELEZA MAJUKUMU YAO

Na. HABIBA MBARUKU & INNOCENT KANSHA - Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka madereva kuongeza umakini wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ili kupunguza ajali zisizokuwa za lazima pamoja na kupunguza uharibifu wa vyombo vya usafiri na kulinda afya za wateja wao.

Pro. Ole Gabriel ameyasema hayo wakati alipotoa mafunzo elekezi kwa madereva wote wa Mahakama ya Tanzania nchini waliohudhuria ana kwa ana na wengine kwa njia ya mahakama Mtandao, leo terehe 12 Februari, 2026, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Aidha, Prof. Ole Gabriel, amesema mafunzo hayo maalum kwa madereva wote wa Mahakama, yamelenga kuimarisha huduma kwa mteja, kuzingatia maadili ya kazi na kuongeza usalama barabarani, mafunzo hayo yaliyoandaliwa chini ya mada ya Huduma kwa Mteja kwa kada ya madereva au maafisa usafirishaji yamesisitiza nafasi muhimu ya dereva katika mnyororo wa huduma za utoaji haki ndani ya taasisi, huku akibainisha kuwa kila mtumishi ana mchango wa moja kwa moja katika taswira na ufanisi wa Mahakama.

“Kuna mambo mengi yanachangia utulivu wa mawazo na kufanya kazi kwa timu kama vile kupata stahiki bora ni msingi wa mafanikio katika taasisi yoyote, uzembe wa kada moja unaweza kuathiri kada nyingine, hivyo ni muhimu kila mmoja kutimiza wajibu wake kwa umakini na weledi,” amesisitiza Prof. Ole Gabriel.

Akizungumzia dhana ya mteja, Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, mteja ni yeyote anayenufaika na huduma inayotolewa, akiwemo kiongozi anayeendeshwa, watumishi wa Mahakama pamoja na wadau wengine barabarani. Amesisitiza kuwa utoaji wa huduma haupimwi tu kwa kutekeleza jukumu, bali kwa namna huduma hiyo inavyotolewa.

Vilevile katika mada ya matarajio ya mteja, madereva wamekumbushwa kuzingatia mambo kumi muhimu ikiwemo usahihi na umahiri katika kazi, usafi wa gari na muonekano binafsi, kutunza muda, usalama, utulivu barabarani na kutunza siri za kikazi na binafsi za viongozi wanaowahudumia.

Kadhalika, Prof. Ole Gabriel ameainisha sehemu ya changamoto zinazowakabili maafisa usafirishaji wa Mahakama nchi nzima, zikiwemo usimamizi wa bajeti binafsi, msongo wa mawazo ya kifamilia, bajeti finyu za matengenezo ya magari na wakati mwingine kukosa heshima kutoka kwa baadhi ya viongozi. Hata hivyo, amewataka madereva hao kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi licha ya changamoto hizo.

Prof. Ole Gabriel ameongeza kuwa, katika kuimarisha maadili ya kazi, Itifaki ya Dereva Bora, inajumuisha mavazi ya heshima, kuepuka kupiga honi ili kumuita kiongozi badala yake dereva anaweza kuwasiliana na kiongozi  wake kwa  njia ya ujumbe mfupi wa maandishi au kumpigia simu baada ya dakika kumi ikiwa ujumbe hautajibiwa, kuweka simu katika hali ya ukimya wanapoendesha, kutoingia katika mabishano barabarani, kufika mapema kabla ya muda wa safari walau dakika kumi kabla ya safari na kuepuka matumizi ya pombekabla ya safari na wakati wa safari.

Akizungumza kuhusu usalama, Mtendaji Mkuu amewakumbusha kuwa dereva anakabidhiwa chombo cha thamani kubwa pamoja na uhai wa abiria na uhai wake mwenyewe, hivyo ni lazima kuhakikisha gari liko katika hali nzuri kabla ya safari, dereva asikubali kuendesha gari bovu lisilokaguliwa kabla ya safari, ahakikishe yuko kwenye afya njema ili kuepuka uzembe unaoweza kusababisha ajali na kuleta hasara kubwa kwa taasisi.

Mafunzo hayo pia yaligusia tabia tano za kuepuka ili kutoleta usumbufu kwa kiongozi, zikiwemo kuanza safari bila kukagua gari, kubishana na kiongozi, uzembe katika mapokezi, kutoa taarifa za siri na kufokeana na wadau wengine wa barabara.

Aidha, Prof. Gabriel amesisitiza kuwa, mteja ndiye sababu ya ajira ya mtumishi, hivyo madereva wanapaswa kushirikiana kwa pamoja, kuepuka majungu na kuweka kipaumbele katika utunzaji wa magari pamoja na maisha ya wanaowahudumia.

Mafunzo hayo ni juhudi za Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha utendaji kazi na kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa umma zinazingatia viwango vya juu vya taaluma na maadili.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akifanya wasilisho wakati alipotoa mafunzo elekezi kwa madereva wote wa Mahakama ya Tanzania nchini waliohudhuria ana kwa ana na wengine kwa njia ya mahakama Mtandao, leo terehe 12 Februari, 2026, katika ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (katika mstari wa mbele) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya Maafisa Usafirisha wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya mafunzo elekezi kwa huduma kwa mteja.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Beatrice Patrick (kushoto) wakati wa mafunzo hayo elekezi kwa Maafisa Usafirishaji (hawapo pichani) 

Sehemu ya Maafisa Usafirishaji wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia mafunzo hayo.

Sehemu ya Maafisa Usafirishaji wa Mahakama ya Tanzania wakifuatilia mafunzo hayo.

(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni