Na. Halima Mnete & James Busanya - Mahakama
Maafisa Usafirishaji wa Mahakama ya Tanzania nchini wamehimizwa
kuongeza umakini, nidhamu na kuzingatia kwa kina misingi ya udereva wa kujihami
ili kupunguza ajali zinazotokea wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya
kimahakama.
Wito huo umetolewa leo tarehe 12 Februari, 2026 Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodma katika kikao maalum kilichowakutanisha
madereva hao na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel, kilicholenga kujadili masuala ya usalama barabarani, ustawi wa
madereva pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika utendaji wa kazi zao za
kila siku.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Kitengo cha
Usafirishaji cha Mahakama ya Tanzania , Bw. Shedrack Bambaganya, amesema kuwa, katika
kipindi cha hivi karibuni kumekuwepo na ajali kadhaa zilizowakumba madereva wa
Mahakama wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, hali iliyosababisha madhara ya
kibinadamu pamoja na uharibifu mkubwa wa magari ya Taasisi.
Ameeleza kuwa, ajali hizo zimeongeza gharama kubwa kwa
Mahakama, zikiwemo gharama za matengenezo ya magari, ucheleweshaji wa ratiba za
shughuli za kimahakama na hatari ya kupoteza maisha ya watumishi pamoja na
wananchi wanaohudumiwa.
“Haya ni matukio ya bahati mbaya, lakini ni wajibu wetu
kuongeza tahadhari zaidi barabarani. Tunapaswa kuzingatia kanuni za usalama,
kutumia udereva kwa kujihami na kuwa makini muda wote tunapokuwa barabarani.
Usalama wa maisha ya wateja wetu na watumiaji wengine wa barabara ni
kipaumbele,” amesisitiza Bw. Bambaganya.
Aidha, ameongeza kuwa, zipo changamoto ambazo madereva
hukutana nazo, zikiwemo ajali zinazosababishwa na uzembe au mwendo kasi wa
madereva wa Taasisi nyingine na watumiaji wengine wa barabara. Akitolea mfano;
ajali iliyotokea Nzega mkoani Tabora katika msafara wa Jaji Kiongozi, alisema
kuwa msafara huo ulikuwa katika upande sahihi wa barabara, lakini dereva wa Taasisi
nyingine ya Umma aliendesha kwa mwendo kasi bila kuchukua tahadhari, hali
iliyomfanya ashindwe kudhibiti gari na kusababisha ajali.
Aidha, Bw. Bambaganya amefafanua kuwa, kutokana na umakini,
uzoefu na ustadi wa dereva wa Jaji Kiongozi, aliweza kulidhibiti gari kwa
haraka na kuokoa maisha ya waliokuwamo ndani ya gari hilo, licha ya gari
kuharibika vibaya na kuhitaji matengenezo ya gharama kubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,
Bi. Beatrice Patrick aliwashukuru madereva kwa kuitikia wito wa kikao hicho na kutoa
maoni yao kwa uwazi na pia kuwasilisha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo
kazini. Mkurungenzi huyo ameahidi kuwa, uongozi wa Mahakama unatambua mchango
mkubwa wa madereva katika kuhakikisha shughuli za kimahakama zinafanyika kwa
wakati na kwa usalama.
Vilevile, miongoni mwa changamoto zilizotajwa na madereva ni
suala la kupanda vyeo kwa waliopo katika madaraja ya chini, pamoja na uhitaji
wa mafunzo ya mara kwa mara ya usalama barabarani. Bi. Beatrice aliahidi kuwa
uongozi utayafanyia kazi masuala hayo kwa kushirikiana na kitengo cha ndani cha
malalamiko cha kuwahudumia watumishi (Judiciary Internal Customer Services) ili
kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza motisha kwa madereva hao.
Kikao hicho kimetajwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha
mawasiliano na ushirikiano kati ya uongozi na madereva kwa lengo la kuongeza ufanisi
na kuboresha usalama barabarani, kulinda rasilimali za Mahakama na kuhakikisha
utekelezaji wa majukumu ya kimahakama unafanyika kwa ufanisi, uwajibikaji na
weledi.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Beatrice Patrick akijibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa na Maafisa Usafirishaji kwenye mafunzo elekezi yaliyoendeshwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani)
Mkuu wa Kitengo cha Usafirishaji cha Mahakama ya Tanzania Bw. Shedrack Bambaganya akifafanua jambo wakati wa mafunzo elekezi kwa Maafisa Usafirishaji wa Mahakama ya Tanzania.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni