Jumatano, 11 Februari 2026

MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI WAPO MUSOMA KUSIKILIZA MASHAURI

Na FRANCISCA SWAI-Mahakama, Musoma

Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wapo mjini Musoma kwa ajili ya usikilizaji wa mashauri 48 kwenye kikao kitakachofanyika kwenye masjala ndogo iliyopo katika jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma.

Kikao hicho kilichoanza tarehe 09 Februari, 2026 kitahitimishwa tarehe 06 Machi, 2026.  Kinaongozwa na Mhe. Dkt. Gerald Ndika ambeye ni Mwenyekiti. Majaji wengine wanaounda jopo hilo ni Mhe. Patricia Fikirini na Mhe. Mustapha Ismail.

Usikilizaji wa mashauri hayo ulitanguliwa na kikao cha maandalizi (Pre Session), huku Majaji wakisisitiza Wadau kukamilisha maandalizi yao mapema, kuzingatia muda ili kuhakikisha mashauri yanasikilizwa kama ilivyopangwa.

Kwenye kikao hicho, kwa mujibu wa Naibu Msajili, Mhe. Omary Kingwele, mashauri yatakayosililizwa ni rufaa mbili za madai na mengine yanahusu jinai.

Kabla ya kuanza kikao hicho, Jopo la Majaji hao lilipata nafasi ya kusalimiana na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma. Watumishi hao waliwakaribisha Majaji hao na kuahidi kuwapa ushirikiano.

Sehemu ya wadau walioshiriki katika kikao cha maandalizi (Pre Session) kilichofanyika Mahakama Kuu Musoma na kuongozwa na Jaji Patricia Fikirini na Jaji Mustapha Ismail.

Watumishi wa Mahakama Kuu Musoma pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma wakisikiliza kwa makini wakati wa mapokezi ya Jopo la Majaji hao.

Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, akisalimiana na Viongozi na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma pamoja na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma.


Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Mbeya.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni